SOMO LA FIQHI
Suala: Ni zipi fadhila za kutawadha
Jabuwabu: Zimepokelewa hadithi kadhaa kutoka kwa Bwana Mtume ﷺ katika kutaja na kuonyesha ubora na fadhila za udhu. Miongoni mwa hadithi hizo ni hizi zifuatazo:
1. Ni sababu ya kupendwa na Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu aliyetukuka Anasema:
إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ} البقرة:222}
[Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wenye kutubia na anawapenda wenye kujitwahirisha] [Al Baqara: 222].
2. Ni alama ya umma wa Mtume Muhammad ﷺ kwa kuwa watakuja Siku ya Kiyama wakiwa weupe wa nyuso na viungo vya kutawadha
Amesema Mtume ﷺ:
إِنَّ أُمَّتِي يُدْعَوْنَ يَوْمَ القِيَامَةِ غُرًّا مُحَجَّلِينَ مِنْ آثَارِ الوُضُوءِ، فَمَنِ اسْتَطَاعَ مِنْكُمْ أَنْ يُطِيلَ غُرَّتَهُ فَلْيَفْعَلْ] متفق عليه]
[Hakika ya umma wangu wataitwa Siku ya Qiyama wakiwa weupe nyuso na viungo kutokana na athari ya kutawadha, basi yoyote miongoni mwenu anayeweza kurefusha weupe wake na afanye] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
3. Kunafuta dhambi na makosa
Amesema Mtume ﷺ:
مَنْ تَوَضَّأَ ، فَأَحْسَنَ الْوُضُوءَ خَرَجَتْ خَطَايَاهُ مِنْ جَسَدِهِ حَتَّى تَخْرُجَ مِنْ تَحْتِ أَظْفَارِهِ] رواه مسلم]
[Mwenye kutawadha akautengeza udhu wake, basi dhambi zake hutoka mwilini mwake mpaka hutoka chini ya kucha zake] [Imepokewa na Muslim.].
4.Huinua daraja
Amesema Mtume ﷺ:
ألا أدلكم على ما يمحو الله به الخطايا ويرفع به الدرجات ؟ قالوا : بلى يا رسول الله قال : إسباغ الوضوء على المكاره وكثرة الخطا إلى المساجد وانتظار الصلاة بعد الصلاة فذلكم الرباط رواه مسلم
[Je, nisiwajulishe nyinyi kile ambacho kwacho Mwenyezi Mungu hufuta dhambi na huinua daraja? Wakasema “Ndio, tuonyeshe” akasema: “Ni kueneza maji ya udhu kwenye viungo, na kukithirisha hatua za kwenga misikitini na kungojea Swala baada ya Swala. Hiyo ndiyo jihadi] [Imepokewa na Muslim.]
SOMO LA FIQHI
Suala: Ni nini Maana ya Udhu katika Luga na katika sheria?
Jawabu: Udhu katika lugha ni Uzuri na usafi
Na Maana ya Udhu katika Sheria:
Ni kutumia maji kwenye viungo maalumu kwa nia ya kujitwahirisha.
Ni ipi Hukumu ya kutawadha?
Jawabu: Kutawadha: ima ni lazima na ima inapendekezwa:
A. Ni lazima kutawadha kwa mambo matatu
1. KUSWALI.
Kwa neno lake Mwenyezi Mungu mtukufu aliposema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ فَاغْسِلُوا وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ وَامْسَحُوا بِرُءُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى الْكَعْبَيْنِ} المائدة:6}
[Enyi Mlioamini! Mnapo simama kwa ajili ya swala basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni] [Al Maaida: 6]
Na kwa hidithi iliyopokelea na Abuu Hurayra radhi za Allah ziwe juu yake asema kuwa Mtume amesema:
لا يقبل الله صلاة أحدكم إذا أحدث حتى يتوضأ] متفق عليه]
[Haikubali Mwenyezi Mungu swala ya mmoja wenu atakapokuwa na hadathi (atakapotengukiwa na udhu) mpaka atawadhe (tena) ] [Imepokewa na Bukhariy na Muslim.]
2. KUTUFU ALKA:
Kwa kauli yake Mtume ﷺ kumwambia mwanamke aliye katika hedhi siku za haji:
افعلي ما يفعل الحاج غير أن لا تطوفي بالبيت حتى تطهري] رواه البخاري]
[Fanya yote anayo fanya mwenye kuhiji isipokuwa usitufu mpaka utwahirike]
[Imepokewa na Bukhari.]
3. KUSHIKA MSAHAFU:
Kwa neno lake Mwenyezi Mungu mtukufu:
لَّا يَمَسُّهُ إِلَّا الْمُطَهَّرُونَ} الواقعة:79}
[Hawaigusi isipokuwa wale waliotwahiriwa] [Al Waaqia: 79]
B. Kutawadha kunapendekeza katika mambo mengine yasiyokuwa hayo
Kwa neno lake Mtume ﷺ aliposema:
ولا يحافظ على الوضوء إلا مؤمن] رواه أحمد وإبن ماجة]
[Na hajilazimishi na udhu isipokuwa mwenye Imani] [ Imepokewa na Ahmad na Ibnu Maajah].
Na kunapendekezwa zaidi kutawadha wakati wa kujadidisha udhu kwa kila Swala, kutawadha kwa kumtaja Mwenyezi Mungu na kuomba, wakati wa kusoma Qur’ani, kabla ya kulala, kabla ya kuoga, na kutokana na kumbeba maiti na baada ya kila tukio la kutangua udhu, hata kama hataki kuswali.
SOMO LA FIQHI
Dini ya uislamu imefunza kila kitu,hakuna jambo kubwa wala dogo ila limeelezewa,na katika yaliofunza ni adabu za kwenda haja,ni mambo gani awajibika afanye mwenye kutaka kwenda choni,na ni mambo gani ni haramu na ya chukiza kufanya yote hayo yamefundishwa katika uislamu,na hii ni kuonesha uzuri wa dini hii.
Suali: Ni mambo gani awajibika kufanya mwenye kutaka kwenda haja?
Jawabu: Mambo Yanayopasa kufanya wakati wa kwenda haja ni haya yafuatayo:
1. Kufunika uchi usionekane na watu wakati wa kwenda haja, kwa neno lake Mtume ﷺ:
ستر ما بين أعين الجن ، وعورات بني آدم ، إذا دخل أحدهم الخلاء أن يقول : بسم الله] رواه الترمذي]
[Kuweka kizuizi baina ya macho ya majini na uchi wa binadamu angiapo chooni mmoja wenu ni aseme “Bismillah”] [Imepokewa na Tirmidh.]
2. Kujiepusha asiingiwe na najisi nguoni mwake au mwilini mwake, na akiingiwa na najisi yoyote aioshe. Kwa hadithi iliyothubutu kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ alipita kwenye kaburi mbili na akasema:
وما يعذبان في كبير ؛ أما أحدهما فكان لا يستتر من البول ] رواه أبوداود]
[Hawa wawili wanaadhibiwa. Na hawaadhibiwi kwa jambo kubwa. Ama huyu hakuwa akijihifadhi na mkojo] [Imepokewa na Abu Daud]
3. Kujiosha kwa maji au kujipangusa kwa mawe, kwa hadithi ya Anas bin Malik t kuwa alisema:
كان رسول الله صلى الله عليه وسلم : يدخل الخلاء فأحمل أنا وغلام نحوي إداوة من ماء وعنزة فيستنجي بالماء] رواه البخاري ومسلم]
[Mtume ﷺ alikuwa akiingia chooni, na mimi nikimbebea, pamoja na mtoto kama mimi, chombo cha maji na bakora, akachukua maji akajisafishia nayo] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
Suali: Nimambo Yanayoharamishwa kufanya wakati wa kwenda haja?
Jawabu: Mambo yanayohamishwa kufanya wakati wa kwenda haja ni haya yafuatayo:
1. Kuelekea kibla au kukipa mgongo wakati wa kwenda haja jangwani. Ama kwenye majengo, lililo bora zaidi ni kuacha kujilazimisha na hilo, kwa kauli yake Mtume ﷺ:
إذا أتيتم الغائط فلا تستقبلوا القبلة بغائط ولا بول ، ولا تستدبروها ، ولكن شرقوا أو غربوا ] متفق عليه]
[Mkienda haja kubwa msielekee kibula, na msikipe mgongo kwa kukojoa wala kwa haja kubwa, lakini elekeeni mashariki au magharibi] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
2. Kuingia haja kwenye njia ya watu kupita au kwenye kiuvuli na sehemu za wao kukaa. Mtume ﷺ amesema:
اتَّقُوا اللاعِنَيْنِ " قَالُوا : وَمَا اللاعِنَانِ يَا رَسُولَ اللَّهِ ؟ قَالَ : الَّذِي يَتَخَلَّى فِي طَرِيقِ الْمُسْلِمِينَ وَفِي ظِلِّهِمْ] رواه مسلم]
[Ogopeni vitu viwili vinavyosababisha mtu kulaniwa. Wakasema: ni vitu gani hivyo ewe mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema: “Ni(kitendo cha) yule anayeingia haja kwenye njia ya watu kupita au kwenye kivuli cha watu kukaa] [Imepokewa na Muslim.]
3. Kuingia na Msahafu chooni, kwa kuwa kitendo hiko kinaonesha dharau kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.
Suali: Ni yapi Yanaopendekezwa kufanya wakati wa kwenda haja?
Jawabu: Yanayopendekezwa kufanya wakati wa kwenda haja ni haya yafuatayo:
1. Kujiepusha na watu wakati wa kwenda haja jangwani
Aseme angiapo chooni:
بسم الله ، اللهم إني أعوذ بك من الخبث والخبائث] رواه البخاري ومسلم]
[Kwa jina la Mwenyezi Mungu. Ewe Mwenyezi Mungu! Mimi najilinda kwako kutokana na Mashetani wa kiume na wa kike] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
2. Kutanguliza mguu wa kushoto angiapo chooni na mguu wa kulia atokapo.
Aseme anapotoka:
غفرانك] رواه أبوداود]
[Naomba msamaha wako.] [Imepokewa na Abu Daud.]
Suali: Ni yapi Yanao chukiza kufanya wakati wa kwenda haja:
Jawabu: Yanao chukiza kufanya wakati wa kwenda haja ni haya:
1. Kusema wakati wa kwenda haja (chooni) au kuzungumza na watu isipokuwa kwa haja (dharura).
عن ابن عمر قال " مر رجل على النبي صلى الله عليه وسلم وهو يبول فسلم عليه فلم يرد عليه] رواه مسلم]
Kutoka kwa Ibn Umar kwamba [mtu mmoja alipita kwa Mtume ﷺ naye yuwakojoa, akamsalimia Mtume, asimrudishie salamu] [Imepokewa na Muslim.]
2. Kuingia chooni na kitu chochote chenye utajo wa Mwenyezi Mungu aliyetukuka, isipokuwa akichelea kuwa kitaibwa na mfano wake, kwa kuwa Mtume ﷺ alikuwa akiingia chooni akiiweka pete yake.
3. Kushika tupu kwa mkono wa kulia au kutamba au kupangusa kwa mawe kutumia huo mkono, kwa kauli ya Mtume ﷺ:
لا يُمسِكن أحدكم ذكره بيمينه وهو يبول ، ولا يتمسح من الخلاء بيمينه ، ولا يتنفس في الإناء] رواه البخاري]
[Asishike mmoja wenu dhakari (tupu ya mbele) yake kwa mkono wa kulia wake akiwa yuwakojoa wala asijipanguse kwa mkono wake wa kulia baada ya kwenda haja wala asivuvie kwenye chombo] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
4. Kukojoa kwenye mpasuko na pango ili asidhuriwe na wadudu wanaotembea au adhuriwe na wao.
SOMO LA FIQHI
Suali: Ni nini Maana ya Kustanji?
Jawabu: Kustanji au Kutamba ni kusafisha na kuondoa najisi iliyotoka katika mojawapo ya tupu (uchi)mbili au zote mbili; tupu ya mbele na ya nyuma kwa kutumia maji twahara au kinachosimama mahala pa maji wakati wa kukosekana maji kama vile mawe, karatasi, kitambaa, majani na kadhalika.
Na anatakiwa mwenye kutamba ahakikishe amejisafisha vema kiasi cha kutobakia athari ya najisi iliyotoka; ikiwa ni mkojo au mavi.
Suali: Ni ipi Hukmu ya kutamba?
Jawabu: Hukmu ya kutamba baada ya kukidhi haja ni Wajibu kama tutakavyoona katika kauli za Mtume ﷺ katika maelezo yajayo.
Kwa hadithi ya Anas bin Malik radhi za Allah ziwe juu yake kwamba yeye alisema:
كان رسول الله صلى الله عليه وسلم يدخل الخلاء ، فأحمل أنا وغلام نحوي [ معي ] إداوة من ماء وعنزة ، فيستنجي بالماء] رواه البخاري ومسلم]
[Alikuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ akiingia chooni, na mimi nikibeba, na mvulana mwingine pamoja na mimi, chombo cha maji na bakora, akajisafisha na maji] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
Na kwa sababu mtu hakubaliwi Ibaada yake akiwa na najisi mwilini au kwenye nguo zake,kwa hivyo inakuwa ni lazima kuondosha najisi kwa kutamba.
Suali: Je inafaa kutamba kwa mawe peke yake?
Jawabu: Inafaa kutamba kwa mawe au kwa karatasi na kitambaa, kwa masharti mawili:
1. Mkojo au choo visipite zaidi ya mahali vinapotoka, vikipita basi itabidii atumie maji.
2. Kutamba kwa mawe kuwe ni kwa kufuta mafuto matatu mpaka kusafishika kwa tupu ya mbele au ya nyuma na iondoke athari ya najisi.
HIKMA YA KUTAMBA
Suali: Ni ipi hikma ya kutamba?
Jawabu: Hekima ya kutamba kwa maji na kwa mawe
1. Kujitwahirisha na kuondoa najisi.
2. Kuwa msafi na kujiepusha na visababisho vya magonjwa.
TANABAHISHO
Haihitajii kutamba kwa kutokwa na upepo,au mtu anapotoka usingizini,bali anaehitaji kutamba ni yule ambae amekwenda haja ndogo au kubwa,wala si Sunna kufanya hivyo kama wengi wanavyo dhania.
Na kutamba kwa maji ni bora kuliko kufuta kwa mawe, kwa kuwa huko kunatakasa zaidi na kutwahirisha zaidi.
Suali: Ni yapi masharti ya vitu vya kutambia?
Jawabu: Masharti ya kitu kifutio (jiwe au mfanowake) ni kama yafuatavyo:
1. Kiwe twahara. Kwani haifai kwa kitu najisi.
2. Kiwe chafaa kutumiwa, kwani haifai kwa kitu kilicho haramu.
3. Kiwe ni chenye kusafisha mahali pa najisi.
4. Kisiwe ni mfupa au choo.imepokewa na Salman al- Farisi radhi za Allah ziwe juu yake asema:
لَقَدْ نهَانَا رسولُ الله صَلّى الله عَلَيْهِ وَسَلّم: "أنْ نَسْتَقبلَ القبلَةَ بغائِطٍ أوْ بوْلٍ، أو أنْ نسْتَنْجيَ باليَمينِ، أو نَسْتَنْجِي بأقَلَّ منْ ثلاثَةِ أحْجارٍ، أو أن نَسْتَنْجيَ بِرَجيعٍ أوْ عَظْمٍ". رواهُ مسلمٌ
[Alitukataza Mtume ﷺ kuelekea upande wa kibla kwa kwenda haja kubwa au ndogo, kutamba kwa mkono wa kulia, au kutamba kwa mawe yasofikia matatu na kutamba kwa choo au mfupa.] [Imepokewa na Muslim.]
5. Kisiwe ni kitu kinachoheshimiwa kama chakula au karatasi iliyoandikwa vitu vinavyohishimiwa.
Kutamba kwa mfupaKutamba kwa kitambaaKutamba kwa chakulaKutamba kwa hanchifuKutamba kwa karatasi inayoheshimikaKutamba kwa mawe
Kutamba kwa mkono wa kulia
Haifai kutamba kwa mkono wa kulia kwa kauli ya Mtume ﷺ aliyesema:
لا يُمسِكن أحدكم ذكره بيمينه وهو يبول ، ولا يتمسح من الخلاء بيمينه ] رواه مسلم]
[Na asishike mmoja wenu dhakari yake (tupu ya mbele) kwa mkono wake wa kulia na asijifute choo kwa mkono wake wa kulia] [Imepokewa na Muslim.]
SOMO LA FIQHI
Suali: Ni zipi Aina za Najisi ?
Jawabu: Najisi kwa mtazamo wa sheria zimegawanywa katika aina tatu zifuatazo :
1. NAJISI NZITO:
Hii ni najisi ya mbwa na nguruwe na mnyama aliyezaliwa kutokana nao au mmoja wao (mbwa na nguruwe). Najisi hii imeitwa najisi nzito kutokana na uzito unaompata mtu katika kuiondosha
2. NAJISI KHAFIFU:
Hii ni mkojo wa mtoto mchanga wa kiume aliye chini ya miaka miwili na hali ila maziwa ya mama tu. Najisi hii imeitwa Najisi khafifu kwa sababu ya wepesi unaopatikana katika uiondosha.
3. NAJISI YA KATI NA KATI:
Hii imekusanya baki ya najisi nyingine ukiondoa najisi ya mbwa na nguruwe na mkojo wa mtoto mchanga wa kiume. Najisi hii imeitwa Najisi ya kati na kati kwa kuwa haiko kwenye uzito na wala haikufika kwenye ukhafifu.
NAMNA YA KUZIONDOSHA NAJISI HIZI
Ni muhimu tukakumbuka kuwa ni haramu kujipakaza najisi na ni wajibu kuiondosha mara tu inapoingia mwilini, nguoni au mahala pake mtu.
Hutwahirishwa mahala palipoingiwa na najisi ya mbwa na nguruwe kwa kupaosha mahala hapo paliponajisika kwa kupaosha mara saba na mojawapo wa mara saba hizo iwe kwa kusugua na mchanga. Bwana Mtume ﷺ amesema:
طُهُورُ إِنَاءِ أحَدِكُمْ إِذَا وَلَغَ فِيهِ الكَلْبُ أنْ يَغْسِلَهُ سَبْعَ مَرَّاتٍ أُولاَهُنَّ بِالتُّرَابِ.] رواه مسلم]
[Twahara ya chombo cha mmoja wenu atakapokiramba mbwa ni kukiosha mara saba, ya kwanza yake ( hizo mara saba) iwe ni kwa mchanga] [Imepokewa na Muslim]
Najisi khafifu hutwahirishwa mahala paliponajisika kwa kuimwagia maji sehemu hiyo, maji yaenee.
عن أم قيس بنت محصن الأسدية أنها أتت بابن لها صغير لم يأكل الطعام إلى رسول الله صلى الله عليه وسلم ، فأجلسه رسول الله صلى الله عليه وسلم في حجره ، فبال على ثوبه ، فدعا بماء فنضحه على ثوبه ولم يغسله
Imepokewa hadithi kutoka kwa Ummu Qays Bint Mihswan Radhi za Allah ziwe juu yake kwamba
[alimpeleka Mtume wa Allah mtoto wake mdogo wa kiume ambaye hajala chakula (ananyonya) akamkojolea (mtume) nguoni, akaagizia maji na kuyamiminia palipokojolewa na hakuiosha (nguo)]. [Imepokelewa na Bukhari na Muslim.]
Ama Najisi ya kati na kati, mahala paliponajisika kwa kuingiwa na najisi hii hutwaharishwa kwa kupaosha na maji twahara mpaka iondoke rangi, utamu na harufu ya najisi hiyo.
Haidhuru kubakia kimojawapo rangi au harufu ziloshindikana kuondoka.
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.