SOMO LA FIQHI
Suali: Ni yapi masharti ya mtu kuwajibika kutoa zaka za mali ya biashara?
Jawabu: Masharti ya kulazimika mtu kutoa zaka ya Mali ya biashara.
1. Kiwango chake kifikie nisabu, na nisabu inakadiriwa kwa kipimo cha dhahabu na fedha.
2. Ikamilishe mzunguko wa mwaka mzima.
3. Iwe imekusudiwa kwa lengo la biashara; na hii ni kwamba iwe imekusudiwa kama kuchuma; kwa kauli ya Mtume ﷺ:
إنما الأعمال بالنيات] رواه البخاري ومسلم]
[Hakika ya matendo ni kwa niya ya mtu] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
Mtu atakapobadilisha niya yake kutoka kwa biashara na kutumia bidhaa hizo basi hukatika hisabu ya mzunguko (mwaka), na akirudia niya ya biashara ataanza tena upya kuhisabu mzunguko mpya, ila akiwa amekusudia kufanya udanganyifu kwa lengo la kuondosha jukumu la kutoa zaka, basi hapa mzunguko haukatiki.
- Mfano: mtu anunue ardhi mwezi wa mfungo nne kwa nia ya kufanya biashara kisha alipofika shabani akageuza nia na akakusudia kujenga nyumba ya kukaa, hapa mwaka utakatika, kisha mfungo mosi akamua kuifanyia biashara mwaka wake utahisabiwa mfungo mosi ila kama alifanya hivyo kwa njia ya hila na kukimbia asitoe zaka basi mwaka hautakatika.
FAIDA
ZAKA YA RASLIMALI
Kinachotolewa zaka katika mali za biashara ni raslimali ambayo kwamba imekusudiwa kwa lengo la kununua na kuuza ili mtu apate faida, ama raslimali ambayo kwamba ni ya mali za kukaa hazizunguki katika biashara yaani si za kununuliwa ili ziuzwe, basi raslimali kama hii haihisabiwi wakati wa kuhisabu bidhaa za biashara wala haitolewi zaka, mfano wake ni kama makabati, na jokofu/firiji ambazo zinahifadhi bidhaa za kuuzwa, na magari yanayobeba bidhaa, na vyombo vya kubebea bidhaa, na mfano wake.
SOMO LA FIQHI
Suali: Ni nini Maana ya Mali ya biashara?
Jawabu: Mali ya biashara ni kila kilichoandaliwa kwa lengo la kuuzwa na kununuliwa ili mtu apate faida.
Na bidhaa za biashara zimekusanya vitu vyote vya sampuli zote za mali ambayo sio pesa zinazotumika kununulia vitu, kama vile magari, nguo, vitambaa, vyuma, mbao, na vyenginevyo vilivyoandaliwa kwa biashara.
Suali: Ni ipi Hukumu ya zaka ya Mali ya biashara.?
Jawabu: Hukmu ya zaka ya mali ya biashara ni lazima; kwa kauli ya Mwenyezi Mungu mtukufu:
أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنفِقُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا كَسَبْتُمْ وَمِمَّا أَخْرَجْنَا لَكُم مِّنَ الْأَرْضِ} البقرة:267}
[Enyi mlioamini! Toeni katika vile vizuri mlivyovichuma, na katika vile tulivyokutoleeni katika ardhi] [Al-Baqarah: 267].
Jumla ya wanavyuoni wametaja kwamba makusudio ya aya hii ni: Zaka ya mali ya biashara, na kwa kauli ya Mwenyezi Mungu mtukufu:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً} التوبة:103}
[Chukua kutoka kwa mali zao sadaka] [At-Tawbah: 103] ,
Na mali ya biashara ni katika mali zilizo dhahiri, basi Kwa ajili hii ikawajibika kutolewa zaka.
SOMO LA FIQHI
Maana ya Dhahabu na Fedha
Dhahabu na fedha, na chochote kinachosimamia nafasi ya vitu hivi viwili miongoni mwa pesa za karatasi zinazotumiwa siku hizi.
Suali: Ni ipi Hukumu ya Zaka ya Dhahabu na Fedha?
Jawabu: Hukmu ya zaka ya Dhahabu na Fedha ni lazima, kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukuf:
وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ} التوبة:34}
[Na wale wanaokusanya dhahabu na fedha wala hawazitoi katika njia ya Mwenyezi Mungu, wape habari za adhabu inayoumiza] [ At-Tawbah 34]
Na kwa kauli ya Mtume ﷺ:
مَا مِنْ صَاحِبِ ذَهَبٍ وَلَا فِضَّةٍ لَا يُؤَدِّي مِنْهَا حَقَّهَا إِلَّا إِذَا كَانَ يَوْمُ الْقِيَامَةِ صُفِّحَتْ لَهُ صَفَائِحَ مِنْ نَارٍ فَأُحْمِيَ عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَيُكْوَى بِهَا جَنْبُهُ وَجَبِينُهُ وَظَهْرُهُ كُلَّمَا بَرَدَتْ أُعِيدَتْ لَهُ فِي يَوْمٍ كَانَ مِقْدَارُهُ خَمْسِينَ أَلْفَ سَنَةٍ حَتَّى يُقْضَى بَيْنَ الْعِبَادِ فَيَرَى سَبِيلَهُ إِمَّا إِلَى الْجَنَّةِ وَإِمَّا إِلَى النَّارِ رواه مسلم
[Mtu yeyote atakae kuwa na Dhahabu na fedha na wala haitolei Haki yake (zaka) itajaaliwa kama vinoo ambavyo atapigwa navyo kwenye migongo na vipaji kila akipata ubaridi (yakipoa makali ya moto) anaregelewa tena (kupigwa navyo), mpaka Allaah Amalize kuhukumu waja wake siku ambayo ni sawa na miaka elfu khamsini. Kisha ndio ataoneshwa njia yake ikiwa kama ni ya peponi au motoni] [Imepokewa na Muslim.]
Suali: Ni yapi Masharti ya kuwajibika kutolewa kwa zaka ya Dhahabu na Fedha?
Jawabu: Masharti yanayo wajibika kutolewa zaka za Dhahabu na Fedha ni haya yafuatayo:
1. Kupitiwa na mwaka.
2. Kuzimiliki kiukamilifu.
3. kufika nisabu ya zaka.
Suala: Ni ngapi Nisabu ya zaka ya Dhahabu na Fedha?
Jawabu:
1. Nisabu ya dhahabu ni Dinari ishirini (85gms)
2. Na Dinari moja ya dhahabu = (ina dhahabu) gramu nne na robo, hivyo basi inakuwa nisabu ya dhahabu kwa gramu 4.25 x 20 = 85gms za dhahabu safi (ambayo haikuchanganywa na kitu).
3. Nisabu ya fedha ni Dirham mia mbili (595 gms)
Na Dirham moja ya fedha = (ina fedha) 2.975gms, hivyo basi inakuwa nisabu ya fedha kwa gramu = 2.975 x 200 = 595gms za fedha safi.
Mfano: Ikiwa gramu moja ya dhahabu = inauzwa Dolari 30, basi inamlazimu mtu kutoa zaka ikiwa amefikisha 85 x 30 = Dolari 2550 dolari.
Suali: Ni kiwango kinachofaa kutolewa zaka ya Dhahabu na Fedha
Jawabu: Kiwango kinachomlazimu mtu kutoa zaka katika dhahabu na fedha na stakabadhi za kiashirio cha pesa ni robo ushuri = 2.5%.
Basi kwa kila Dinari ishirini ya dhahabu atatoa zaka nusu Dinari, na itakayozidi (zaidi ya Dinari ishirini) itapigiwa hisabu, iwe imezidi kidogo au sana.
Na kwa kila Dirhamu mia mbili za fedha atatoa zaka Dirhamu tano, na kitakachozidi atakipigia hisabu; kwa kauli ya Mtume ﷺ: (Ikiwa unamiliki Dirhamu mia mbili, na zimekamilisha mwaka, basi yatakiwa utoe Dirhamu tano, na si juu yako kutoa chochote – yaani – katika dhahabu mpaka umiliki Dinari ishirini, basi ukiwa na Dinari ishirini, na umemaliza nazo mwaka, basi itakulazimu utoe nusu ya Dinari, na zitakazozidi utafanya kwa hisabu hii) [Imepokewa na Abu Daud.]
MFANO WA KUFAHAMISHA:
Mtu anamiliki Dolari 9000, na imepita mwaka mzima hali ya kuwa anazimiliki hizo pesa, je analazimika kutoa zaka?
Kwanza: Tutahisabu nisabu ya zaka kwa mtizamo wa dhahabu au fedha kama ifuatavyo:
Nisabu = Gramu thamanini na tano katika dhahabu safi = 85 x bei ya gramu moja ya dhahabu safi (inavyouzwa) siku ile ya kulazimika kwake kutoa Zaka, na tukisie kwamba gramu moja yauzwa = Dolari 30.
= 85 x 30 = Dolari 2550.
Kwa hivyo Nisabu yake = Dolari 2550, hivyo basi itakuwa mali ya mtu huyu imefika nisabu, na imekamilisha mwaka mzima, kwa hivyo inamlazimu kutoa zaka.
Pili: Tutahisabu kiwango anachofaa kutoa zaka kama ifuatavyo: -
Kiwango cha kutolewa zaka = 2.5%.
= 9000 x 2.5/100 = Dolari 225.
Kwa hivyo huyu mtu yafaa atoe kutoka kwa mali yake Dolari 225 kama zaka.
Suala: Je mtu anafaa kuchanganya Dhahabu na Fedha pamoja ?
Jawabu: Mtu anapo miliki dhahabu na fedha lakini zikawa hazifikii kiwango cha kutolewa zaka, kauli yenye nguvu ni kuwa hatowajibika kutoa zaka, wala hata zikikusanywa pamoja ili zifikiye kiwango, kwani uwajibu ni kutoa dhahabu pekeyake na fedha pekeyake kwa sababu ni vitu viwili tofauti, na hakuna dalili ya kuzikusanya pamoja ili ifikie kiwango, na kwa neno lake Mtume:
لَيْسَ فِيمَا دُونَ خَمْسِ أَوَاقٍ صَدَقَةٌ] رواه البخاري ومسلم]
[Hakuna chini ya wakiya tano zaka] [Imepokewa na Bukharin a Muslim]
Na atakae zikusanya dhahabu na fedha itakuwa amewajibisha zaka chini ya wakia tano.
SOMO LA FIQHI
Mapambo ya wanawake yako sampuli mbili: Mapambo ya dhahabu na fedha, na mapambo yasiyokuwa ya dhahabu wala fedha.
1. Mapambo ya dhahabu na fedha.
Kitengo cha kwanza: Mapambo yaliyokusudiwa kwa lengo la kuhifadhiwa au kuwekwa kama akiba ya baadaye kunapotokea jambo, au imenunuliwa kwa nia ya kufanya biashara, basi zaka hapa ni lazima kutoa.
Kitengo cha pili: Mapambo yaliyokusudiwa kwa lengo la kutumiwa, basi uzuri zaidi ni kuitolea zaka ili kijiepusha na lawama,kwa Hadithi hii
وعَنْ عَمْرِو بْنِ شُعَيْبٍ عَنْ أَبِيهِ عَنْ جَدِّهِ أَنَّ امْرَأَةً أَتَتْ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَمَعَهَا ابْنَةٌ لَهَا ، وَفِي يَدِ ابْنَتِهَا مَسَكَتَانِ غَلِيظَتَانِ مِنْ ذَهَبٍ ، فَقَالَ لَهَا : أَتُعْطِينَ زَكَاةَ هَذَا ؟
قَالَتْ : لا
قَالَ : أَيَسُرُّكِ أَنْ يُسَوِّرَكِ اللَّهُ بِهِمَا يَوْمَ الْقِيَامَةِ سِوَارَيْنِ مِنْ نَارٍ ؟
قَالَ : فَخَلَعَتْهُمَا ، فَأَلْقَتْهُمَا إِلَى النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ، وَقَالَتْ : هُمَا لِلَّهِ عَزَّ وَجَلَّ وَلِرَسُولِهِ رواه أبوداود
Kutoka kwa Amru bin Shuayb kutoka kwa baba yake kutoka kwa Babu yake kwamba mwanamke mmoja alimjilia Mtume ﷺ pamoja na binti yake, na mkononi mwa binti yake kuna bangili mbili nzito za dhahabu, (Mtume ﷺ) akamwambia: [ Je watolea zaka hizi bangili] Akasema: Hapana. Akasema (Mtume ﷺ): [Je utafurahia Mwenyezi Mungu akuvalishe bangili kwa hizi bangili mbili za moto?] Akasema: Yule binti akazivua, akampatia Mtume ﷺ, kisha akasema: “Hizo ni za Mwenyezi Mungu na Mtume wake” [Imepokewa na Abu Daud.]
Na kuna wanavyuoni ambao hawawajibishi mapambo ya wanawake kutolewa zaka, kwasababu hayo mapambo sio mali inayotarajiwa kukua, lakini ni pambo la mtu binafsi yuwatumia na kunufaika nayo kama vile nguo na fanicha na vyombo, na ni katika mahitajio ya mwanamke na virembesho vyake, na asili ya mali ni kukua au kuweza kukuzwa ndio ilazimike kutolewa zaka.
Na ubora wa hali ni mtu kutoa zaka kwa mapambo yaliyokusudiwa kwa matumizi ambayo si kinyume na sheria na kwa lengo la kujirembesha; kwasababu kauli hii iko katika hali nzuri zaidi na kujiondoa kwa lawama; kwa kauli ya Mtume ﷺ:
دع ما يريبك إلى ما لا يريبك] رواه البخاري]
[Wachana na linalokutia shaka na ufanye lile lisilokutia shaka] [Imepokewa na Bukhari].
2. Mapambo Yasiyo kuwa ya Dhahabu wala Fedha.
Kama vile almasi, yakut, lulu, na mfano wa hizi, basi vitu hivi havitolewi zaka hata vikawa vingi kiasi gani, isipokuwa vikikusudiwa kwa lengo la biashara vitatolewa zaka vitakuwa vimeingia katika mali ya biashara.
SOMO LA FIQHI
Suali: Madini ni nini? na inamanisha nini ya Hazina iliyozikwa ardhini?
Jawabu: Madini ni chochote kinachotolewa ndani ya ardhi ambacho kwamba sio sampuli ya ardhi kama vile dhahabu, fedha, vyuma, na vijiwe vya tunu kama vile almasi na rubi, na risasi, na vyenginevyo katika vitu asili vinavyotolewa ndani ya Ardhi.
Hazina iliyozikwa ardhini
Ni Mali iliyozikwa ndani ya ardhi kwa kuekwa na mtu, kutokana na dhahabu, na fedha, na mfano wa vitu hivi.
Suala: Ni ipi Hukumu ya zaka ya madini na hazina iliyozikwa ardhini
Jawabu: Hukmu yake ni lazima, kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنفِقُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا كَسَبْتُمْ وَمِمَّا أَخْرَجْنَا لَكُم مِّنَ الْأَرْضِ} البقرة:267}
[Enyi mlioamini! Toeni katika vile vizuri mlivyovichuma, na katika vile tulivyokutoleeni katika ardhi] [Al-Baqarah: 267]
Na kauli ya Mtume ﷺ:
وفي الركاز الخمس] رواه البخاري ومسلم]
[Na katika hazina iliyozikwa ardhini (toeni) khumusi (1/5))] [Imepokewa na Bukharin a Muslim.]
Sauli: Ni yapi Masharti ya kutoa zaka ya hazina iliyozikwa ardhini
Jawabu: Hakuna masharti yoyote ya zaka ya hazina iliyozikwa ardhini, basi atakapomiliki mtu hio hazina iliyozikwa ardhini anafaa kutoa zaka yake moja kwa moja.
Kiwango cha kuwajibika mtu kutoa zaka ya madini na hazina iliyozikwa ardhini
Ni wajibu mtu kutoa khumusu (1/5) kwa kichache au kingi atakachopata katika madini na hazina iliyozikwa ardhini, kwa jumla ya kauli ya Mtume ﷺ:
وفي الركاز الخمس] رواه البخاري ومسلم]
[Na katika hazina iliyozikwa ardhini (toeni) khumusi] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.