SOMO LA FIQHI
Maelezo kuhusu sijida ya kusahau
Sijida ya sahau
Ni sijida mbili ambzo mwenye kuswali anasujudu ili kuungaunga kasoro iliyopatikana katika Swala yake kwa ajili ya kusahau.
SABAU ZA SIJDA YA KUSAHAU.
Sababu za kusujudu sijida ya kusahau ni tatu: kuwa na shaka, kuongeza na kupunguza.
1- KUFANYA SHAKA
Nako ni kuwa na shaka baina ya vitu viwili, ni kipi kilichotokea.
Kufanya shaka katika Swala kuna gawanyika mara mbili:
1. Kufanya shaka baada ya kuswali:
Shaka hii haishughulukiwi.
Mfano wake: Mtu alifanya shaka baada ya kuswali Alfajiri, Ameiswali rakaa mbili au tatu? Shaka hii haishughulikiwi, mpaka awe na yakini, hapo atafanya kulingana na yakini yake.
2. Kufanya shaka akiwa ndani ya Swala:
Shaka hii ina hali mojawapo ya hali mbili:
A) Liwe na nguvu kwake yeye mojawapo ya mambo mawili:
Na hapa atafanya kile kilicho na nguvu kwake na atasujudu kwa kusahau baada Salamu.
Mfano wake: Mtu anaswali adhuhuri na akaifanyia shaka rakaa: je ni ya pili au ni ya tatu, lakini lililo na nguvu kwake ni kuwa ni ya tatu, hili litaifanya hiyo rakaa kuwa ni ya tatu na ataitimiza Swala yake, kisha atasujudu kwa kusahau baada ya Salamu.
Na dalili ya hilo ni kauli ya Mtume ﷺ: [Akifanya shaka mmoja wenu na ajitahidi kujuwa la sawa ni lipi, kisha atowe Salamu, kisha asujudu sijida mbili] [Imepokewa na Ibnu Hibbaan.].
Anatowa Salamu kisha Atasujudu sijida ya kusahau
B). Lisimdhihirikie katika mambo mawili, ni lipi lenye nguvu:
Huyu atajengea juu ya kichache, hivyo basi atatimiza Swala yake na atasujudu sijida ya kusahau kabla ya Salamu.
Mfano wake: Mtu anaswali Adhuhuru akaifanyia shaka ile rakaa anayoiswali: ni ya pili au ya tatu? Kusiwe na uzito wa jambo lolote kati ya haya mawili. Basi huyu atajengea juu ya uchache na ataihesabu kuwa ni ya pili, na atatimiza Swala yake na atasujudu sijida ya kusahau kabla ya Salamu.
Na dalili ya hilo ni kauli ya Mtume ﷺ:
إذا شك أحدكم في صلاته، فلم يدر كم صلى أثلاثاً أم أربعاً فليطرح الشك وليبن على ما استيقن، ثم يسجد سجدتين قبل أن يسلم رواه مسلم
[Akifanya shaka mmoja wenu katika Swala yake, asijue ameswali ngapi, tatu au nne, basi aitupilie mbali shaka yake na ajengee juu ya yakini yake kisha asujudu sijida mbili kabla hajapiga Salamu] [Imepokewa na Muslim.].
Anatowa Salamu kisha Atasujudu sijida ya kusahau
2. KUZIDISHA.
Nako ni kule kuongeza Rukuu au Sijida kwa mwenye kuswali…
Na kuzidisha kuko namna mbili
A) Awe mwenye kuswali ataikumbuka pale wakati wa kuzidisha.
Na hapo itamlazimu aiache ile ziada na atimize Swala yake kisha asujudu sijida ya kusahau baada ya kupiga Salamu.
Mfano wake: Mtu anaswali Adhuhuri, akasimama kuleta rakaa ya tano kisha akakumbuka katikati. Hapa itamlazimu akae haraka na atimize Swala, kisha asujudu sijida ya kusahau baada ya kupiga Salamu.
b. Awe mwenye kuswali akakumbuka baada ya kuifanya.
Huyu atatimiza Swala yake kisha atasujudu sijida ya kusahau baada ya kutowa Salamu. Na dalili yake ni hadithi ya Ibnu Mas'ud (Radhi za Allah ziwe juu yake) [Kwamba Mtume ﷺ aliswali Adhuhuri rakaa tano. Akaambiwa: “Je Swala imeongezwa?” Akasema: [Kwani kuna nini?] akaambiwa: “Umeswali rakaa tano”, akasujudu sijida mbili baada ya kuwa ashatowa Salamu] [Imepokewa na Bukhari.].
3. KUPUNGUZA.
Nako ni kupunguza mwenye kuswali nguzo au wajibu miongoni mwa nguzo au wajibu za Swala.
1. Kupunguza nguzo
Iwapo nguzo hiyo ni takbiri ya kufungia Swala, basi Swala inabatilika, kwa kuwa itakuwa haikufungika tangu mwanzo. Na iwapo nguzo hiyo si takbiri ya kufungia Swala, basi hapo pana mojawapo ya hali mbili:
A) Ni aikumbuke mwenye kuswali baada ya kufikia mahali pa hiyo nguzo kwenye rakaa ifuatayo:
Hii inafuta ile rakaa ambayo nguzo hii iliachwa na inasimamisha rakaa ifuatayo mahali pake.
Mfano wake: Mtu aliyesahau kurukuu katika rakaa ya kwanza, kisha akakumbuka naye yuko kwenye rukuu ya rakaa ya pili kuwa alisahau kurukuu kwenye rakaa ya kwanza.Mtu huyu ataizingatia rakaa ile kuwa ni rakaa ya kwanza na hataizingatia ile rakaa iliyotangulia, na atakamilisha Swala yake, kisha atasujudu kwa kusahau baada ya kutowa Salamu.
Anatowa Salamu kisha Atasujudu sijida ya kusahau
B) Aikumbuke mwenye kuswali kabla hajafikia mahali pa nguzo hiyo kwenye rakaa ifuatayo:
Hapa itamlazimu airudie ile nguzo iliyoachwa ailete na zile za baada yake, na ataikamilisha Swala yake, kisha atasujudu kwa kusahau baada ya Salamu.
Mfano wake: Mtu alisahau sijida ya pili na kikao cha kabla yake katika rakaa ya kwanza, akakumbuka hilo baada kuinuka kutoka kwenye rukuu katika rakaa ya pili. Yeye atarudi kukaa na kusujudu, kisha ataikamilisha Swala yake, kisha atasujudu kwa kusahau baada ya Salamu.
2. Kupunguza jambo la wajibu:
Akisahau mwenye kuswali jambo moja la wajibu miongoni mwa mambo ya Swala ya wajibu basi hapo pana hali tatu tu:
A) Aikumbuke kabla hajaondoka pale mahali pa wajibu huo katika Swalah.
Na hapa ataileta huo wajubu na hatolazimika na jambo lolote.
B) Aikumbuke baada ya kuondoka pale mahali pa nguzo hiyo katika Swala kabla hajafika kwenye nguzo ifuatayo.
Na hapa atarudi aifanye nguzo hiyo na asujudu sijida ya kusahau baada ya kutoa Salamu.
C) Aikumbuke baada ya kufikia kwenye nguzo inayoifuatia.
Na hapa ataendelea na Swala yake na hatairudia na atasujudu kwa kusahau kabla ya kutoa Salamu.
Mfano wake: mtu aliinuka kutoka kwenye sijida ya pili ya rakaa ya pili ili ainuke kwenda kwenye rakaa ya tatu hali ya kusahau kikao cha Atahiyatu ya kwanza. Kisha akakumbuka kabla ya kusimama kuwa yeye amesahau kikao cha Atahiyatu. Basi huyu atajituliza akae kwa kikao cha Atahiyatu, kisha ataikamilisha Swala yake, na hatolazimiwa na jambo lolote.
Akiwa atakumbuka baada ya kuinuka na kabla ya kulingana sawa katika kusimama, atarudi akae na asome Atahiyatu, kisha akamilishe Swala yake, na asujudu kwa kusahau kabla ya kutoa Salamu.
Akikumbuka baada ya kulingana katika kusimama, kikao cha Atahiyatu hakimlazimu na kwa hivyo hatakirudia, atakamilisha Swala yake na atasujudu sijida ya kusahau kabla ya kutoa Salamu.
Na dalili ya hilo ni hadithi ya Abdullah bin Buhainah (Radhi za Allah ziwe juu yak) [Kwamba Mtume ﷺ aliwaswalisha Adhuhuri akainuka katika rakaa mbili za kwanza bila ya kukaa, na watu wakainuka pamoja naye. Hata alipomaliza kuswali na watu wakamngojea kupiga Salamu, alipiga takbiri na hali yeye amekaa, akasujudu sijida mbili kabla ya kutoa Salamu, kisha akatoa Salamu] [Imepokewa na Bukhari].
Kwa yaliyotangulia inabainika kwetu sisi kwamba sijida ya kusahau inakuwa kabla ya kutoa Salamu na pia baada ya kutoa Salamu.
NAMNA YA KUSUJUDU SIJDA YA KUSAHAU.
Sijida ya kusahau ni kama sijida ya Swala, atapiga takbiri wakati wa kusujudu, na wakati wa kuinuka kutoka kwenye sijida, na atasema yale yanayo semwa katika sijida na kati ya sijida mbili.
MAELEZO.
1. Akipiga Salamu mwenye kuswali kabla ya Swala kukamilika na asikumbuke isipokuwa baada ya kipindi kirefu, basi atairudia Swala upya, na akikumbuka baada ya kipindi kifupi kama dakika mbili tatu, ataikamilisha Swala yake na atasujudu kwa kusahau baada ya Swala.
2. Inamlazimu maamuma kumfuata imamu katika sijida ya kusahau hata kama alimfuata baada kusahau.
3. Ikikusanyika kwa mwenye kuswli sahau mbili, mahali pa mojawapo ni kabla ya Salamu na mahali pa pili ni baada ya Salamu, basi yeye atasujudu sijida ya kusahau mara moja kabla ya kuleta Salamu.
SOMA LA FIQHI
Kumesuniwa katika adhana kufanya mambo yafuatayo:-
1. KUELEKEA QIBLAH:
Ni sunna kwa muadhini kuelekea Qiblah wakati wa kuadhini, kwa sababu bora ya pande za kuelekewa kwa ajili ya ibada ni upande uliyoko Qiblah.
Na isitoshe imethibiti kwamba waadhini wa Bwana Mtume Radhi za Allah ziwe juu yao walikuwa wakielekea Qiblah wakati wa kuadhini.
2. KUTWAHIRIKA KWA MUADHINI KUTOKANA NA HADATHI MBILI:
Ni suna mtu kuadhini hali ya kuwa yu katika hali ya twahara, yaani hana hadathi ndogo inayompasishia udhu wala ile kubwa inayompasishia josho.
Kwa Hadithi ya Ibnu Abbas Rahi za Allah ziwe juu yake amesema:
إن الأذان متصل بالصلاة فلا يؤذن أحدكم إلا وهو طاهر] تلخيص الخبير]
[Hakika Adhana imeunganishwa na Swala asiadhini mmoja wenu ila na yeye ni Twahara] [Talkhisul Khabir]
Na Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ:
إني كرهت أن أذكر الله إلا على طهر] رواه أبوداود وإبن ماجة]
[Nachukia (sipendi) kumdhukuru Allah Mtukufu ila niwe na twahara]. [Imepokewa na Abuu Daawoud na Ibnu Maajah]
3. KUADHINI HALI YA KUWA AMESIMAMA:
Ni sunna mtu kuadhini hali ya kuwa amesimama.
عن أبي قتادة أن النبي-صلى الله عليه وسلم- قال لبلال:[قم فأذن رواه البخاري ومسلم]
Amepokea Abuu Qatada radhi za Allah ziwe juu yake kwamba Mtume ﷺ Alimwambia Bilaali [Simama uadhini] [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Lakini Ikiwa mtu ana udhuru kama ugonjwa akisimama ataanguka au maumivu yatazidi, basi ataadhini kwa kukaa.
4. KUGEUZA SHINGO KULIANI NA KUSHOTONI:
Miongoni mwa suna za adhana kama zilivyothibiti kutoka kwa Bwana Mtume ﷺ. Ni muadhini kugeuza shingo yake kuliani wakati wa kusema: (Hayya alas-swalaah) na kushotoni anaposema: (Hayya Alal-falaah).
Imepokewa kwamba Abuu Juhayfah Radhi za Allah ziwe juu yake amesema:
وَأَذَّنَ بِلَالٌ قَالَ فَجَعَلْتُ أَتَتَبَّعُ فَاهُ هَا هُنَا وَهَا هُنَا يَقُولُ يَمِينًا وَشِمَالًا يَقُولُ حَيَّ عَلَى الصَّلَاةِ حَيَّ عَلَى الْفَلَاحِ] رواه البخاري]
[Na Bilali akiadhini asema, nikawa ninaufuatilia mdomo wake huku na huko. (Akageuka) kuliani na kushotoni (wakati wa kusema): Hayya Alal-swalaah, Hayya Alal-falaah]. [Imekewa na Bukhari]
5. MWADHINI AWEKE VIDOLE VYAKE VIWILI VYA SHAHADA MASIKIONI MWAKE.
Na hii imepokelea kuwa Bilal Radhi za Allah ziwe juu yake alikuwa akiweka vidole vyake vya Shahada alipokuwa akiadhini kama alivyo taja Imamu Al Bukhari Mungu amrahamu
6. ADHANA ITOLEWE KWA UTULIVU:
Ni katika jumla ya suna mtu kuadhini kwa “Tartiyli”. Yaani ayatamke maneno ya adhana kwa mtungo wa utulivu.
7. KULETA “TATH-WIYBU” KATIKA ADHANA YA ALFAJIRI:
“Tath-wiybu” ni muadhini kusema baada ya (Hayya alal-falaah mara mbili aseme); ASWALAATU KHAYRUN MINAN-NAUM, mara mbili.
Amepokea Annasai kutoka kwa Abii Mah'dhura radhi za Allah ziwe juu yake amesema:
قلت: يا رسول الله، علمني سنة الأذان، فذكره إلى أن قال بعد قوله حي على الفلاح: فإن كان في صلاة الصبح قلت: الصلاة خير من النوم مرتين، الله أكبر الله أكبر، لا إله إلا الله
[Nilimuliza Mtume ﷺ nikasema Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nifundishe na mimi Sunna za Adhana, akamtajia mpaka alipofika kwa tamko la hayya Alaal Falaah :(akamwambia) ikiwa ni Swala ya Asubuhi utasema Aswalaatu Khayrun mina Nnawm (Swala ni bora kuliko usingizi) Mara mbili (Kisha utasema) Allahu Akbar Allahu Akbar Laailaha illa allah]
8. MWADHINI AWE NA SAUTI NZURI YA NGUVU:
Ni sunna muadhini kuwa na sauti kali na nzuri itakayomudu kuulainisha moyo wa msikilizaji na kumpelekea kuuitika wito huo.
Suna hii inatokana na kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ alipomwambia Abdullah Ibn Zayd Radhi za Allah ziwe juu yake ambaye ndiye aliyeiona adhana usingizini:
فقم مع بلال فألق عليه ما رأيت به، فإنه أندى منك صوتاً] رواه أبوداود]
[Inuka pamoja na Bilali, umtamkishe (maneno) uliyoyaona (usingizini) Kwani yeye ana sauti kali kuliko wewe]. [Imepokewa na Abuu Daawoud]
9. MUADHINI AWE NI MUADILIFU MWENYE TABIA NJEMA:
Muadhini anapaswa kutangaa baina ya watu kwa tabia njema na uadilifu.
Hii ni kwa Hadithi iliopokelewa na Ibnu Abbas Radhi za Allah ziwe juu yake asema.
ليؤذن لكم خياركم ويؤمكم أقراؤكم] رواه أبوداود وإبن ماجة]
[Awaadhini nyinyi mbora wenu,na awasalisheni nyinyi msomi wenu] [Imepokewa na Abuu Dawud na Ibnu Maajah]
10. KUWE NA WAADHINI WAWILI:
Ni sunna msikiti kuwa na waadhini wawili kwa ajili ya swala ya alfajiri. Mmoja ataadhini kabla ya kuingia kwa alfajiri na mwingine baada ya alfajiri.
Sunna hii imethibiti kutokana na hadithi (riwaya) ya Abdullah Ibn Umar Radhi za Allah ziwe juu yake :
أَنَّ بِلالا كَانَ يُؤَذِّنُ بِلَيْلٍ فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : كُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّى يُؤَذِّنَ ابْنُ أُمِّ مَكْتُومٍ] رواه البخاري ومسلم]
Hakika Bilali huadhini usiku, Akasema Mtume ﷺ [basi kuleni na kunyweni mpaka muisikie adhana ya Ibn Ummu Maktuum]. [Imepkewa na Bukhari na Muslim]
Lakini kunatakikana kwa muadhini huyu anayeadhini nje ya wakati kuwa na wakati mmoja ili kuepuka kuwatatiza na kuwachanganya watu.
SOMO LA FIQHI
FADHILA ZA ADHANA
Zimepokelewa hadithi kadhaa kutoka kwa Mtume wa Allah ﷺ zinazofahamisha fadhila na thawabu kubwa zinazopatikana ndani ya adhana.
Miongoni mwa hadithi hizo ni kama zifuatavyo:
1. Imepokewa kutoka kwa Abuu Hurayrah radhi za Allah ziwe juu yake kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:
لو يعلم الناس ما في النداء والصف الأول ثم لم يجدوا إلا أن يستهموا عليه لاستهموا] رواه البخاري ومسلم]
[Lau watu wangelijua yaliyomo katika wito (adhana) na safu ya kwanza (ya swala ya jamaa) Kisha wasipate (fursa hizo) ila kwa kupiga kura, basi wangelipiga kura.] [Imepokewa na Bukhaari na Muslim]
2. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Said Al-khudriy Radhi za Allah ziwe juu yake amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ :
إني أراك تحب الغنم والبادية، فإذا كنت في غنمك وباديتك فأذنت بالصلاة، فارفع صوتك بالنداء، فإنه لا يسمع مدى صوت المؤذن جن، ولا إنس، ولا شيء، إلا شهد له يوم القيامة رواه البخاري
[Mimi nakuona unapenda (kuchunga) mbuzi na kukaa Baadiya (majangwani) utakapokuwa Badia na mbuzi wako ukaadhini kwa ajili ya Swala Basi inyanyue sauti yako kwa wito huo (adhana) kwani hakika haisikii sauti ya muadhini jini wala mwanadamu wala kitu cho chote ila (sauti hiyo) itamshuhudia siku ya kiyama.] [Imepokewa na Bukhari]
3. Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amewaombe Mungu wenye kuadhini na akaomba kwa kusema:
اللَّهُمَّ أَرْشِدِ الْأَئِمَّةَ، وَاغْفِرْ لِلْمُؤَذِّنِينَ] اخرجه أبوداود وصححه الألباني]
[Ewe Mwenyzi Mungu waongoze maimamu na na uwasamehe wenye kuadhini] [Imepokewa na Abuu Dawud na kusahihishwa na Al Baaniy]
SOMO LA FIQHI
MASHARTI YA KUSIHI KWA ADHANA
Ili adhana iweze kusihi na kuzingatiwa kisheria kuwa ni adhana kumeshurutizwa kupatikana sharti zifuatazo:-
1. Muadhini awe ni Muislamu, mwanamume, mwenye akili.
Haisihi Adhana ya Kafiri na wala haikubaliwi Adhana yake,na vile vile haisihi Adhana ya Mwanamke na Mtoto ndogo asiefikisha miaka ya kuweza kupambanuwa.
2. Adhana ilingane na mpango uliowekwa.
Ni sharti matamko ya adhana yaletwe kwa mtungo na utaratibu wake kama yalivyopokewa kutoka kwa Bwana Mtume ﷺ.
Hii ni kwa sababu kuacha utaratibu kunatuhumisha kufanya mchezo na kupunguza uzito wa tangazo hili la kuingia kwa wakati wa swala.
3. Iwe ni yenye kufuatanishwa, kusiwe na mwanya mrefu baina ya maneno yake.
Ni sharti upatikane mfululizo baina ya matamko ya adhana, kiasi cha kutopatikana mwanya mkubwa baina ya tamko la kwanza na lile la linalofuatia.
4. Iwe ni pale unapoingia wakati wa Swala.
Na hili linatokana na kauli ya Bwana Mtume ﷺ:
وإذا حضرت الصلاة فليؤذن لكم أحدكم] متفق عليه]
[Itakapohudhuria swala, basi na akuadhinieni mmoja wenu]. [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
5. Iwe ni kwa Lugha ya Kiarabu
Ni sharti matamko yote ya adhana yaletwe kwa lugha ya Kiarabu kama yalivyopokelewa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ.
Haijuzu kutolewa adhana kwa lugha nyingine yo yote isiyo Kiarabu, kwani hiyo haitakuwa adhana bali tarjamah (tafsiri ya neno kwa neno) ya adhana
TANBIHI:
Haikusuniwa adhana kwa jamaa ya wanawake, kwa sababu ya fitina inayoweza kupatikana kutokana na kusikilizika sauti zao na wanamume.
Iliyosuniwa kwao ni Iqaama tu, kwa sababu hekima yake ni kuwainua waliohudhuria swala kuswali. Na haina kuinua sauti kama ilivyo kwa adhana.
SOMO LA FIQHI
MAANA YA ADHANA
Adhana ni neno la Kiarabu lenye maana mbili; maana ya kilugha na maana ya kisheria Kilugha neno adhana lina maana ya “tangazo” kama lilivyotumika ndani ya Qur'ani Tukufu:
وَأَذَانٌ مِّنَ اللَّهِ وَرَسُولِهِ إِلَى النَّاسِ يَوْمَ الْحَجِّ الْأَكْبَرِ أَنَّ اللَّهَ بَرِيءٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ} التوبة:3}
[Na ni tangazo kutokana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa wote siku ya Hija Kubwa kwamba Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawana jukumu lolote kwa washirikina] [Tawba:3]
Ama maana ya adhana kisheria: Ni (dhikri) utajo maalum iliyowekwa na Uislamu kwa ajili ya kutangaza kuingia kwa wakati wa swala ya fardhi na kuwaita waislamu kuja kuswali
MAANA YA IQAAMA
Ni kujulisha kuanza kuswaliwa kwa kuleta utajo (dhikiri)maneno maalumu.
HUKMU YA KUADHINI NA KUQIMU
1. Katika Swala za jamaa:
Ni faradhi ya kutosheleza, kwa Swala tano za faradhi peke yake, sawa mtu akiwa safarini au mjini, kwa kuwa hizo mbili ni miongoni mwa alama za Uislamu za waziwazi, hivyo basi haifai kuziacha. Amesema Mtume ﷺ:
وإذا حضرت الصلاة فليؤذن لكم أحدكم، وليؤمكم أكبركم] متفق عليه]
[Ufikapo Wakati wa Swala, basi awaadhinie mmoja wenu, kisha awaswalishe mkubwa wenu] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
2. Katika Swala ya anayeswali peke yake:
Ni sunna. Amepokewa kutoka kwa Uqbah bin Amir akisema: Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ akisema:
يعجب ربكم من راعي غنم في رأس شظية بجبل يؤذن بالصلاة ويصلي فيقول الله عز وجل انظروا إلى عبدي هذا يؤذن ويقيم الصلاة يخاف مني قد غفرت لعبدي وأدخلته الجنة رواه أبوداود والنسائي
[Anamuonea ajabu Mola wako mchunga mbuzi aliye juu ya kilele cha jabali, anayeadhini kwa Swala kisha akaswali, hapo aseme Mwenyezi Mungu Aliyetukuka: “Mwangalieni mja wangu huyu, anaadhini kisha anakimu Swala, ananiogopa! Nishamsamehe mja wangu na nitamuingiza Peponi] [Imepokewa na Abuu Dawud na Annasai.]
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.