JE WAISLAMU WANAABUDU MASHETANI NA MAJINI??
Kuna mambo mengi ya uongo yanazuliwa Uislamu na Waislamu hata uislamu hauhusiki nayo, na uzushi huu unaenezwa na madui wa Uislamu kwa kujua au kutojua katika makala haya napenda kujibu madai hayo ya uzushi na kuonesha yakwamba mambo hayo yanayozushwa ni uongo mtupu kwa dalili za wazi kutoka kwenye Qur'ani na Hadithi za Bwana Mtume ﷺ
Wanaeneza wasiokua waislamu ya kwamba Waislamu dini yao ni ya Masheitani na ni wachawi najibu uzushi huu kwa kusema Uislamu ni dini ya Mungu kwa wanaadamu na majini na hakuna hata siku moja Waislamu wamewahi kua na mahusiano na majini wala kuwaabudu majini, majini ni Viumbe wa Mungu kama binaadamu wapo wazuri na waovu, na wao pia wameumbwa kwa ajili ya kumuabudu Mwenyezi Mungu kama alivyo sema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ} الذاريات:56}
[Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.] [Adh-dhaariyaat:56]
na Uislamu ni Dini inatolingania Tawheed kumpwekesha Mwenyezi Mungu kwa Ibaada na kwamba hakuna anaefaa kuabudiwa kwa hali ila Mwenyezi Mungu na hii ndio nguzo ya kwanza ya Uislamu, Vipi tena uzuliwe Uislamu kwa jambo hili la kuwa waislamu wanabudu Majini na Mashetani??
na Mwenyezi Mungu ameliweka wazi jambo hilo,na siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atasema:
{أَلَمْ أَعْهَدْ إِلَيْكُمْ يَا بَنِي آدَمَ أَن لَّا تَعْبُدُوا الشَّيْطَانَ ۖ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ وَأَنِ اعْبُدُونِي ۚ هَٰذَا صِرَاطٌ مُّسْتَقِيمٌ}
[Je! Sikuagana nanyi, enyi wanaadamu, kuwa msimuabudu Shet'ani? Hakika yeye ni adui dhaahiri kwenu.Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.] [Ya-sin:60-61]
Ama madai ya kuwa Wailsmau wanabudu Shetani, hayo ni madai ambao hayaingi akilini hata kwa Mtoto mdogo.
nikinukuu katika Qur'ani Mwenyezi Mungu Mungu anatuambia katika sura ya 35 aya ya 6
{إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمْ عَدُوٌّ فَاتَّخِذُوهُ عَدُوًّا ۚ إِنَّمَا يَدْعُو حِزْبَهُ لِيَكُونُوا مِنْ أَصْحَابِ السَّعِيرِ}
[Hakika Shet'ani ni adui yenu, basi mfanyeni kuwa ni adui. Kwani yeye analiita kundi lake liwe katika watu wa Motoni.]
Kwa hivyo sheitani ni adui yetu na wala hatuwezi kumuabudu kiumbe ama kuhusu Waislamu kua wachawi nasema uchawi na uganga katika Uislami ni haramu ni katika Madhambi makubwa mno katika Qur'ani Mwenyezi Mungu anatuambia katika sura ya 2 aya ya 102
{وَاتَّبَعُوا مَا تَتْلُو الشَّيَاطِينُ عَلَىٰ مُلْكِ سُلَيْمَانَ ۖ وَمَا كَفَرَ سُلَيْمَانُ وَلَٰكِنَّ الشَّيَاطِينَ كَفَرُوا يُعَلِّمُونَ النَّاسَ السِّحْرَ}
[Na wakafuata yale waliyo zua mashet'ani kuuzulia ufalme wa Su leiman. Na wala Suleiman hakukufuru, bali mashet'ani ndio walio kufuru, wakiwafundisha watu uchawi,]
katika aya hii tunaona wazi yakwamba Masheitani wamekufuru kwa sababu wanawafundisha watu uchawi. Na Mtume Muhammad anasema ﷺ:
اجتنبوا السبع الموبقات]، قالوا: يا رسول الله، وما هن؟ قال: [الشرك بالله، والسحر] متفق عليه]
[Epukeni madhambi saba yenye kuangamiza] Masahaba wakamuliza ni yapi Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ Akasema: [Kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kufanya uchawi] [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Hivyo basi Muislamu yeyote anaefanya kazi ya uchawi na uganga sio katika sisi na ameshaasi Uislamu na Uislamu uko mbali na yeye, hata ikiwa anaefanya hivyo anajiita Shekhe
Makala haya yameandikwa na
Mahamd Fadhil El Shiraziy
NI NINI UISLAMU?
Uislamu ni dini ya mwisho ambayo amekuja nayo bwana Mtume Muhammad S.A.W na Uislamu umekuja kukamilisha sheria zote zilizopita. Na uislamu ni dini ya Mitume wote kwanzia Adam mpaka Mtume Muhammad ﷺ.
Uislamu ni kunyenyekea na kujisalimisha kwa mungu na kumuabudu Mungu mmoja mwenye Nguvu alie Mbinguni.
MWENYEZI MUNGU NI NANI ?
Mungu au ALLAH ndie Mungu mmoja alieumba kila kitu na ndie anaeendesha kila kitu katika ulimwengu ni mungu mmoja anaejitegemea mwenye nguvu hakuzaa wala hakuzaliwa wala hafanani na kitu chochote wala haonekani kwa utukufu wake.
Mwenyzi Mungu anasema katika Qur'ani Tukufu Sura 112 Aya 1-4
[Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee.Mwenyezi Mungu MkusudiwaHakuzaa wala hakuzaliwaWala hana anaye fanana naye hata mmoja.]
UISLAMU UNAFUNDISHA NINI?
Uislamu unafundisha kumuabudu mungu mmoja na kuacha kuabudu Masanamu na vitu vingine , Uislamu unafundisha Tabia njema, kuishi na Majirani vizuri, kuwatendea wema wawili, na kuwafanyia wema watu wote hata wasiokua Waislamu imekuja katika Qur'ani Mwenyezi anasema:
[Hawakatazi Mwenyezi Mungu kwa wale wasiowapiga vita katika dini yenu na hawajawatoa katika majumba yenu kuwafanyia wema na kuwafanyia uadilifu hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wenye kufanya uadilifu]. [60:8]
YESU NI NANI KWA WAISLAMU?
Yesu ama Nabii (Issa) ni binadamu kama binadamu wengine na ni Mtume katika Mitume wa Mwenyezi Mungu wala sio mungu wala mwana wa mungu na kuzaliwa kwake bila ya baba ilikua ni Miujiza katika miujiza ya mungu kwani yesu ni kama Nabii (Adam) ambae aliumbwa bila ya Baba wala Mama.
[Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam; alimuumba kwa udongo kisha akamwambia: Kuwa! Basi akawa] [3:59]
Na Nabii Issa au yesu kama Manabii wengine alipewa Miujiza ya kufufua maiti na kuwaponya wagonjwa sio kwa uwezo wake bali ni kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho atawakana wanaomuabudu na sisi Waislamu tunaamini yakwamba yesu hakuuwawa wala hakusulubiwa bali alipaishwa Mbinguni kwa mwenyezi Mungu,na atashuka mwisho wa Dunia na kufariki.
[Na kwa kusema kwao: Sisi tumemuuwa Masihi Isa, mwana wa Maryamu, Mtume wa Mwenyezi Mungu - nao hawakumuuwa wala hawakumsalibu, bali walifananishiwa tu. Na hakika walio khitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo. Wao hawana ujuzi nayo wowote, ila ni kufuata dhana tu. Wala hawakumuuwa kwa yakini Bali Mwenyezi Mungu alim- tukuza kwake, na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.] [4:157-158]
WAISALMU NA QADHIA YA MASJIDUL AQSWA
Kadhia ya msikiti mtukufu wa masjidul Aqswa ni kadhia ya kila muislamu ulimwenguni wala si kadhia ya waarabu na waisraeli wala wapalestina na mayahudi kama waislamu wengi wanavyodhania kwa sababu ya kutojua umuhimu wa msikiti wa Aqswa katika Uislamu.
Msikiti wa Aqswa ulioko katika mji wa Qudsi ni Kibla cha kwanza cha waislamu na ni haram ya tatu takatifu,na ni katika misikiti mitatu ambayo anaruhusiwa muislamu kufunga safari kwa ajili ya kuyazuru. Mtume MUHAMMAD ﷺ amesema:
لا تشد الرحال إلا إلى ثلاث مساجد المسجد الحرام ومسجدي هذا والمسجد الأقصى] رواه البخاري ومسلم]
[Haifungwi safari (kwa ajili ya ziara) ila kwenda katika misikiti mitatu Masjidul Haram na Msikiti wangu huu na Masjidul Aqswaa] [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Na Mtume wetu ﷺ kama tunavyo jua alipo pelekwa miraji safari yake aliianzia masjidul Aqswa baada ya kutoka Makkah kisha kupelekwa mbinguni,Mwenyezi Mungu anasema:
{سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ}
[SUBHANA, Ametakasika aliye mchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyo uzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona.] [Al israa:1]
Aya hii inaonesha wazi mafungamano ya misikiti hii miwili, Mwenyezi Mungu alikuwa anaweza kumpaleka Mtume wake ﷺ kutoka makkah moja kwa moja hadi mbinguni lakini kwanza alimpeleka masjidul Aqswa na huku nikuonyesha wazi kuwa msikiti huu ni miongoni mwa misikiti muhimu kwa waislamu.
Na Mwenyezi Mungu alipowa faradhia waislamu kuswali Swala tano kwa kila siku waislamu walikua wakiswali kuelekea masjidul Aqswa kwa mda wa miezi 16 mpaka mwenyezi mungu alipo muamrisha mtume MUHAMMAD ﷺ kuelekea upande wa msikiti wa Makkah,kwa hivyo msikti huu ndicho kibla cha kwanza kwa waislamu.
KUKOMBOLEWA MASJIDUL AQSWAA.
Alipo shikilia Ukhalifa Umar Ibnul Khatab radhi za Allah ziwe juu yake alimpa uongozi wa kwenda kuikomboa miji ya Shaam Swahaba Mtukufu Abuu Ubayda Aamir Ibnul Jarraah badala ya Khalid Ibnul Waleed radhi za Allah ziwe juu yao, na jeshi likaelekea kwenda kuukomboa mji wa Quds ambao ulikua ukiitwa (Alyaa), alipofika katika mji huo na kupambana na warumi ambao ndio waliokuwa wakiutawala mji huo katika zama hizo,wakashindwa kuingia kwa sababu ya kujihami watu wake katika ngome madhbuti ambazo walikua ndani yake,waislamu wakawazunguka na kuwazingira kwa mda,mpaka walipotaka suluhu na waislamu na wakashurutisha ni lazima aje khalifa wa Wailsamu achukuwe funguo za mji huo,ndipo alipofunga safari Amirul Mu’minina Umar Ibnul Khatwab kutoka Madina hadi katika mji wa Quds na kuchukuwa fungua za mji huo na akaingia katika msikiti huu mtukufu na kachukuwa ahadi kuwapa Amani wakazi wa mji huo na kuandika ahadi hiyo iliyojulikana kama (Al’ahdul Umariyya) na hayo yalitokea katika mwaka wa 15 Hijriyya sawa na mwa wa 636 miladia,na ukabaki msikiti huo katika mikono ya Waislamu mpaka katika vita vya msalaba ambavyo wazungu walikuja na kuuteka tena mji huo wa Quds kwa mara ya pili mwaka wa 1099 miladia na kuuvunja msikiti huo wa Aqswa na kuujenga vingine na kuuita (Haykal Sulayman),mpaka katika mwaka 1187 ndipo waislamu walipoandaa jeshi liliongozwa na Swalahuddin Al Ayyubiy na kuuzingira mji huo na kisha kuukomboa kutoka katika mikono ya wakiristo na kubaki katika mikono ya Wailsamu mpaka ilipokuja dola ya kizayuni dola ambayo iliwekwa na wazungu na kuwaondosha na kuwafukuza wenyeji wapalestina na badala yake kuwaleta Mayahudi kutoka nchi mbali mbali na kuwaweka katika miji hiyo Mwaka wa 1948, na katika mwaka 1967 kulipotokea vita baina ya dola za Kiarabu na Israel ulivamiwa mji wa Qudsi na kubaki chini ya utawala wa Israel hadi leo.
Tanabahisho.
Jambo la kusikitisha ni kuwa waislamu wengi hawajui historia ya msikiti huu mtukufu kwa sababu vijana wetu hawafundishwi historia kama hizi katika mashule wanayosoma kwa lengo la kuwafanya waislamu wasiijue historia na tarehe ya msikiti kama huu,badala yake vijana wetu wanafundishwa historia ya watu wasiokua na maana , na waislamu wengi wanona yakwamba kadhia ya masjidul Aqswa haiwahusu bali ni kadhia ya Waarabu na Israel na hivi ndivyo wanavyotaka makafiri ili waislamu wasijihusishe kabisa na kadhia kama hii, na sasa hivi mayahudi wanaenda mbio kuifanya kadhia hii iwe ni kadhia ya wapalestina na mayahudi , na pia waarabu wajitoe na wabaki wapalestina peke yao lakini ukweli wa mambo ni kuwa kadhia kama hii inawahusu waislamu wote duniani na ni wajibu wa kila muislamu kuuhami na kuulinda msikiti wa Aqswa ,na watakapo acha kuuhami msikiti huu basi watakwenda kuulizwa na Mwenyezi Mungu siku ya kiyama.
JE UNATAKA HUSNUL KHAATIMAH (MWISHO MWEMA)?
Je, unataka Husnul-Khaatimah (mwisho mwema )? Basi Ishi maisha mema!
Ee binaadamu! Mche Mwenyezi Mungu na jiandae kukutana na Mola wako kwa maandalizi ya waja wema. Hakika hali ya (kila) mwanadamu ni kama Anavyosema Mwenyezi Mungu ﷻ:
{يَا أَيُّهَا الْأِنْسَانُ إِنَّكَ كَادِحٌ إِلَى رَبِّكَ كَدْحاً فَمُلقِيهِ}
[Ewe mtu! Hakika wewe unajikusuru kwa juhudi kumwendea Mola wako Mlezi, basi utamkuta] [Al-Inshiqaaq 84:6]
Ewe Muislamu, hakika binaadamu hajui wapi atafariki wala hajui lini atafariki kama Anavyosema Mwenyezi Munguﷻ
{وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَاذَا تَكْسِبُ غَداً وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ}
[Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari.] [Luqmaan: 34]
Ikiwa hatujui tutakachokichuma kesho, jambo ambalo ni katika matendo yetu, basi hakika hatujui pia lini tutakufa kwani hilo ni katika matendo ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa hatujui nchi (au mahali) gani tutakufa juu ya kwamba mtu anakwenda nchi (au mahali) anayoichagua mwenyewe, basi hakika yeye hajui lini atakufa. Kwa hivyo basi, mahali pa kufariki na wakati wa kufariki haujulikani! Tunamuomba Mwenyezi Mungu Aturuzuku husnul-khaatimah (mwisho mwema)
Na si muhimu mtu kujua kufariki lini wala kufariki wapi. Hakika hakuna la muhimu isipokuwa jambo la muhimu ni katika hali gani mtu atafariki? Hili ndilo la muhimu; atafariki katika hali gani? Je, utafariki ukiwa katika Imani na ikhlaasw na Tawhiyd? Tunamuomba Mwenyezi Mungu Atujaalie hayo yote (kufariki katika hali hizo za Imani, ikhlaasw na Tawhiyd). Au je utafariki katika shaka na shirki na kufuru na ukanushaji? Hili ndilo muhimu, hili ndio! Lakini anayetaka kufariki kifo kizuri, basi afanye kheri kwani Mwenyezi Mungu ni Mkarimu mno na Mpaji mno Hatomwacha mja Wake katika dhiki ikiwa mja atakuwa ni mwenye kumkumbuka (na kumdhukuru) Mwenyezi Mungu wakati anapokuwa katika hali ya raha. Mtume ﷺ amesema:
تَعَرَّفْ إلَى اللَّهِ فِي الرَّخَاءِ يَعْرِفُك فِي الشِّدَّةِ] رواه أبو القاسم بن بشران في أماليه]
[Mjue Mwenyezi Mungu katika (hali ya raha) Atakujua ukiwa katika shida (au dhiki)] [Imepokewa na Abuul Qaasim bin Bishraan]
Imetajwa kutoka kwa Salaf (Maswahaba na wema waliotangulia) kwamba binaadamu yanapomfikia mauti, Shetani humdhihirishia dini ya Kiyahudi, ya Kinaswara (Kikristo) na ya Kiislamu, na kwamba shetani hujifafanisha sura ya baba yake huyo mtu. Kisha husema: “Ee mwanangu! Usiache dini ya Kiyahudi, usiache dini ya Kinaswaara!” (Huendelea kumshawishi) mpaka mtu hufariki katika mojawapo wa dini hizo mbili batili, zilizofutwa ambazo Mwenyezi Mungu Hazikubali! Wa-Allaahi (naapa kwa Allaah!) hii hakika ni fitnah kubwa kabisa! Lakini kwa neema ya Allaah, na kama alivyosema Shaykhul-Islaami Ibn Taymiyyah (Mungu amarahamu) kwamba dini hazidhihirishwi kwa kila anayefariki. Ikiwa anayefariki ni mwenye niyyah nzuri, na ni mtu aliyenyooka katika ‘ibaadah, basi Allaah humuokoa katika fitnah hii. Ndio maana Maulamaa wengi wamefasiri kuhusu fitnatul-mamaat (fitnah ya kifo) ambayo tunajikinga nayo katika kila Swala kuwa ni fitnah hii (ya Shetani kumjia mtu anapofariki na kumdhihirishia dini mbili. Mtume ametuamrisha kuwa tunapomaliza tashahhud zetu za mwisho katika Swalaah tuseme:
اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ عَذَابِ جَهَنَّمَ وَمِنْ عَذَابِ الْقَبْرِ وَمِنْ فِتْنَةِ الْمَحْيَا وَالْمَمَاتِ وَمِنْ شَرِّ فِتْنَةِ الْمَسِيحِ الدَّجَّالِ] رواه مسلم]
Allaahumma inniy a’uwdhu Bika min ‘adhaabi jahannam wa min ‘adhaabil qabri, wamin fitnatil mahyaa wal mamaati, wamin sharri fitnatil-Masiyhid-dajjaal
[Ee Mwenyezi Mungu hakika mimi najikinga Kwako na adhabu ya (moto) na adhabu za Kaburi, na fitnah ya uhai, na (fitnah) ya kifo, na shari ya fitnah ya Masiyhi-Dajjaal] [Imepokewa na Muslim]
Ulamaa wengi wakafasiri fitnatul-mamaat kwamba ni fitnah wakati wa mtu anapofariki kwa sababu ndio fitnah kubwa kabisa katika maisha ya mtu kwa vile kuna mzunguko na kugeuka:
إِنَّ الرَّجُلَ لَيَعْمَلُ عَمَلَ أَهْلِ الْجَنَّةِ حَتَّى مَا يَكُوْنُ بَيْنَهُ وَبَيْنَهَا ِ إِلاَّ ذِرَاعٌ، فَيَسْبِقُ عَلَيْهِ الكِتَابُ فَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ النَّارِ فَيَدْخُلُهَا] رواه البخاري ومسلم
[…Hakika mtu hufanya ‘amali ya watu wa Peponi, mpaka ikawa hapana baina yake na Pepo ila dhiraa, akatanguliwa na aliloandikiwa (majaaliwa yake) akafanya ‘amali ya watu wa Motoni, akaingia Motoni] [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Imehadithiwa kwamba Imaam Ahmad (Mungu amrahamu) alipokuwa anakaribia kufariki, akisema: “Bado, bado!” Akaulizwa: “Kwanini unasema bado bado?” Akasema: “Shetani yuko mbele yangu anajitafuna vidole vyake akiniambia: “Umenikwepa sijaweza kukupoteza ee Ahmad”. Ndio nikawa namjibu: Bado bado!” Ina maana; madamu roho ya binaadamu bado ipo mwilini mwake, basi hakika anaigopa fitnah.
Bali hakika Siku ya Qiyaamah itakapofika, itakuwa kama kwamba hawakuishi isipokuwa saa moja katika mchana (wa siku moja) kama Anavyosema Mwenyezi Mungu ﷻ:
كَأَنَّهُمْ يَوْمَ يَرَوْنَ مَا يُوعَدُونَ لَمْ يَلْبَثُوا إِلَّا سَاعَةً مِنْ نَهَارٍ} الأحقاف:35}
[Siku watakayoyaona yale waliyoahidiwa itakuwa kama kwamba hawakukaa (duniani) isipokuwa saa moja (tu) ya mchana] [Al-Ahqaaf 46: 35]
Allah Atujaalie Mwisho Mwema na tufe na Kalimatu Tawhiid
Imeandikwa na
Ustadh Yusuf Abubakar
☎+25422671024
Eldoret Kenya
HARAMU ( 1 )
يقول رب العزة سبحانه : {قل إنما حرم ربي الفواحش ما ظهر منها وما بطن والإثم والبغي بغير الحق وأن تشركوا بالله ما لم ينزل به سلطانا وأن تقولوا على الله ما لا تعلمون} الأعراف:33
Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu
[Sema (uwaambie): "Mola wangu ameharimisha (Haya: Ameharimisha) mambo machafu, yaliyodhihirika na yaliyofichika, na dhambi na kutoka katika taa (ya wakubwa) pasipo haki, na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na ambacho hakukiteremshia dalili (ya kusema kishirikishwe naye) na (ameharimisha) kusema juu ya Mwenyezi Mungu msiyoyajua.] [Al Araaf: 33]
Tambua kwamba Mwenyezi Mungu mtukufu hajahalalisha ila jambo jema na hajaharamisha ila jambo baya.
Aliulizwa mmoja katika waarabu kwanini umesilimu, akasema “ sijaona kitu katika maneno au vitendo vinavyopendeza katika akili na utu wa mwanadamu isipokuwa uislamu umelihalalisha jambo hilo na umelisisitiza kufanyiwa kazi , na sijaona kitu katika maneno au vitendo vinavyochukiza katika akili na utu wa mwanadamu isipokuwa uislamu umeharamisha na kukemea jambo hilo.
Ni nini haramu ?
Ni zipi athari za haramu ?
Ni vipi vigawanyo vya haramu ?
Kwanini tunatumbukia katika matatizo ya haramu ?
Ni upi msimamo wa muislamu juu ya haramu ?.
MAANA YA HARAMU
Haramu kilugha ni kinyume cha halali na ni kile ambacho haifai kukiendea. Imam Arraazy.
Na Haramu kisheria ni kila alichokitaka Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa waja wake wakiache kwa ulazima na adhabu kali kwa yule atakayekwenda kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu Subhanahu wata'ala.
Kuhalalisha na kuharamisha ni haki ya Mwenyezi Mungu Mtukufu peke yake na haifai kiumbe chochote kuingilia au kujihusisha na haki hii ya ALLAH Jalla jalaaluh.
دخل عدي بن حاتم وكان نصرانيا على النبي عليه الصلاة والسلام، وسمعه يقرأ قول الله تعالى: اتخذوا أحبارهم ورهبانهم أربابا من دون الله
قال: يا رسول الله ما اتخذناهم أربابا، لم نسجد لهم، قال: [ألم يحلوا لكم الحرام ويحرموا عليكم الحلال فأطعتموهم؟ قال: بلى، قال: فذلك عبادتكم إياهم] مختصر ابن كثير مجلد 2 ص 137
Siku moja alikuja Udeyy bin Haatim (alikuwa mnaswara) kwa bwana Mtume MUHAMMAD ﷺ akamsikia anasoma Qur’ani aya hii akasema ewe Mtume ﷺ hatujawafanya miungu na wala hatujawasujudia, akasema Mtume ﷺ je hawajahalalisha haramu na hawajaharamisha halali ? akasema naam, akasema Mtume ﷺ basi hiyo ndio ibada yenu juu yao. [Mukhtasar wa Ibn Kathiir , Mjeledi wa 2 , ukurasa wa 137 ] .
Kila unayemtii katika jambo ambalo ndani yake kuna maasia basi ujue umemshirikisha Mwenezi Mungu mtukufu.
Kila kinachopelekea katika haramu ni haramu , zinaa ni haramu ALLAH Subhanahu wa Ta'ala ameseme katika Qur’ani:
وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَا ۖ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا} الإسراء:32}
[Wala mskikaribie zinaa. Hakika hiyo(zinaa) ni uchafu (mkubwa) na ni njia mbaya (kabisa).] [Al Israa: 31]
Na wala hajasema na musifanye uzinifu , ni wajibu wa kila mtu kujiweka mbali na kila njia yenye kupelekea katika uzinifu kama picha chafu , kumgusa mwanamke asiyekuwa halali yako na mengineyo …
Halali iko wazi na haramu iko wazi na haramu iko wazi , na likikuchanga baina ya halali na haramu basi jiepusheni kuhofia kuingia katika haramu .
Uislamu umekataza kuuza kitu chochote cha haramu au kukitoa zawadi maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akiharamisha jambo anaharamisha na thamani yake.
جاء رجل إلى النبي وذكر للنبي عليه الصلاة والسلام أن عنده خمرا، وأنه يعلم بتحريم الله عز وجل له فقال: يا رسول الله أفلا أكارم بها اليهود (أي أهديها إلى اليهود) فاليهود يشربون الخمر، فقال عليه الصلاة السلام: [إن الذي حرمها حرم إهداءها] رواه الحميدي في مسنده
Alikuja mtu mmoja kwa bwana mtume Muhammad ﷺ akamueleza kuwa ana pombe nymbani kwake na anajuwa kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kaharamisha , akasema kumwambia mtume ﷺ je naweza kuwakirimu mayahudi kuwapatia zawadi ? kwani mayahudi wanakunywa pombe , akasema Mtume ﷺ hakika yule aliyeharamisha pombe ndiye aliyeharamisha kuitowa zawadi . [Imepokelewa na Al Humaydiy katika Musnad yake].
Inaendelea
©Abu-Khalfan Assarawi
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it. / This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
+255656333678
03/03/2017
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.