HUYU NDIYE YATIMA WA KIISLAMU
Dini ya kiislamu imetilia mkazo sana katika swala la wazazi kuwalea watoto wao katika maadili mema ya kiislamu sambamba na kuzishibisha akili zao ufahamu sahihi na kuzisafisha akili zao kwa kila aina ya propaganda zinazoenezwa juu ya uislamu .
Sio kila mtoto anabahatika kupata malezi mema kutoka kwa wazazi wake , bali kuna baadhi hukosa malezi haya pindi anapofariki baba mzazi na kubakia katika mgongo wa ardhi hii kwa jina la yatima .
Yatima kwa mujibu wa sheria ni mtoto ambaye alifiliwa na baba yake mzazi kabla ya kufikia umri wa baleghe , ama baada ya kubaleghe hatoitwa tena yatima
Mayatima ni sehemu katika jamii hivyo basi wanatakiwa kulelewa katika mazingira yanayokubaliana na sheria pamoja na kumuandaa msimamizi wa mayatima kimaadili , imani , elimu na huruma ili akifikishe kile kinachokusudiwa kwa mayatima kinyume na inavyofanyika leo katika baadhi ya vituo hatimaye unakuta katika jamii vijana wengi wasiokuwa na mwelekeo wa maisha yao , maadili mabaya ni wale ambao walilelewa katika baadhi ya vituo vya mayatima, je ni nani wa kulaumiwa ?
Uislamu umesisitiza kuwasimamia mayatima kwa wema , kuwakirimu kwa kila aina ya kheyri ambayo ipo ndani ya uwezo wa msimamizi , vile vile umekataza kuwadhalilisha kwa njia moja au nyengine jambo ambalo humpelekea yatima kukimbia katika kituo ambacho analelewa au nyumba ya jamaa zake wa karibu waliobeba majukumu ya kuzisimamia mali zake baada ya baba yake kufariki.
فأما اليتيم فلا تقهر } الآية 9 من سورة الضحى}
[Basi yatima usimwonee!] [Adh Dhuhaa:9]
Kumsimamia yatima sio kumsimamia katika kula yake tuu , bali ni kumsomesha elimu sahihi ya dini yake pamoja na dunia , kumtizama kiafya na kumuandaa katika mazingira ya kuja kukabiliana na mustaqbali wake inshaaALLAH , kuwa naye karibu katika mambo ya kheyri , kuishi naye kwa ukweli na ikhlaas , vile vile mlezi awe na pupa ya kumuona yatima huyu ana tabia njema na maadili mema kama vile mlezi alivokuwa na hamu ya kuwaona watoto wake wana mustaqbali mzuri .
Itaendele wiki ijayo inshaaaALLAH
©Abu-Khalfan Assarawi
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it. / This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
+255656333678
03/03/2017
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.