HUKMU YA KUJIPAKA MANUKATO KWA ALIEFUNGA
Suali : Assalam alykum warahmatullahi wabarakaatuhu. Ni ipi hukmu ya dini kuhusu mwanamume kujipaka manukato akiwa amefunga katika mwezi wa ramadhan au nje ya mwezi wa ramadhan na natarajia jawabu la swali hili kwa mujibu wa rai za maimamu wanne ikiwa kuna ikhtilafu baina yao pamoja na kutaja hoja zao na ALLAH awalipe kheri.
Jawabu :Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu na kumswalia Mtume Rehma na amani zimfikie yeye.Kutumia manukato kwa mwenye aliekufunga inafaa kwa madhehebu ya Imam Abu hanifah, na imam Maalik, kwa kauli mashhuri na pia jambo hili amelitaja Imam Shafi'i katika kitabu cha (Al Umm).Na pia Ibnu Qudama katika kitabu chake (Al Mughny) amedhihirisha yakwamba jambo hili linafaa kwa madhahabu ya Imam Ahmad bin Hanbal.Na wanasema baadhi ya wanazuoni wa madhehebu ya Imam Shafi'i yakwamba inapendeza kwa alifunga kuacha jambo hili la kujipaka manukato,na inachukiza kunusa ikiwa harufu ya manukato yale inafika katika ubongo kama ilivyokuja katika kitabu cha sheikh Zakariyya Al Answary (Sharhul bahjah).
Na pia wamesema hivyo baadhi ya wanazuoni wa madhehebu ya imam Ahmad bin Hanbal yakwamba jambo hili linachukiza.
Na dalili yakwamba jambo hili linafaa ni kuwa hakuna dalili iliyokuja kukataza kulifanya au kupendeza kuliwacha kwani jambo hili la kujipaka manukato sio kula wala kunywa wala sio katika maana ya kula na kunywa.
Ama wale waliosema inapendeza kuwacha kupaka manukato katika hali ya Saumu wamelifanya jambo hili ni katika kuwacha matamanio ambayo yanafaa kwa mwenye kufunga.na dalili ya kuwacha matamanio kwa aliefunga ni hadithi iliyopokelewa na Imamu Al bukhary
[والذي نفسي بيده لخلوف فم الصائم أطيب عند الله من ريح المسك، يترك طعامه وشرابه وشهوته من أجلي]
[Naapa kwa yule ambae nafsi yangu iko mikononi mwake harufu mbaya itokayo katika mdomo wa aliefunga inanukia zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kushinda harufu ya miski anawacha chakula chake na kinywaji chake na matamanio yake kwa ajili yangu]
Lakini matamanio yanayokusudiwa katika hadithi hii ni kuingiliana kama alivyosema (Ibn Hajar) katika kitabu chake (Fathul Baary) ama yasiokua kuingiliana na kula na kunywa katika matamanio haiamrishwi kuviacha kama vile kulala kukaa chini ya kivuli cha baridi hivyo hivyo kutumia manukato.
Na Allah ndie Mjuzi zaidi
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.