Menu

AL-USWUL ATH-THALATHA (Misingi Mitatu)


misingi


ASILI YAKE

Jina lake ni Abul-Husayn Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab bin Sulaymaan bin ‘Aliy Musharrif Al-Wuhaybiy. Kabila lake ni Bani Tamiym. Amezaliwa mwaka 1115 H (1704 M) katika mji ya ‘Uyaynah kijiji cha Yamaamah ndani ya Najd, kaskazini Magharibi ya mji wa Riyadh, Saudi Arabia. Ametoka katika familia ya Wanavyuoni kwani baba yake ‘Abdul-Wahhaab alikuwa ni Mwanachuoni maarufu wa Najd na Qaadhwi wa mji huo.

ELIMU YAKE

Alijifunza kusoma Qur-aan alipokuwa na umri mdogo na akaihifadhi akiwa chini ya umri wa miaka kumi. Na Mwenyezi Mungu   Alimjaalia kuwa na uhodari na akili nzuri, wepesi wa kufahamu na kumaizi jambo au somo. Alipendezewa mno kusoma kazi za Sheikhul-Islaam Ibn Taymiyyah na mwanafunzi wake Ibnul-Qayyim (Mungu awarahamu.

Alifanya bidii kwenye masomo yake na kuendelea kujifunza chini ya usimamizi wa baba yake. Akajifunza elimu ya Dini chini ya Wanavyuoni walioko mjini mwake wakiwemo baba yake na ‘ammiy yake. Alisafiri kutoka kwenda Madiynah kusoma chini ya Wanavyuoni wakubwa wa huko wakiwemo; Sheikh ‘Abdullaah bin Ibraahiym bin Ash-Shamariyyi, na Mwanachuoni maarufu wa India Sheikh Muhammad Hayaat Al-Sindi. Alikwenda Makkah pia na alitekeleza Hajj. Hatimaye akaelekea Baswrah (Kaskazini Iraq) kutafuta elimu zaidi akasoma chini ya Wanavyuoni wa huko akawa maarufu kwa mijadala baina yake na Wanavyuoni.

HARAKATI ZAKE NA MITIHANI

Watu wa Najd walikuwa katika shirki na bid’ah (uzushi). Walikuwa wakiabudu miungu mingi na kuabudu makaburi, miti, mawe, mapango, majini na mashaytwaan, waja wema waliojulikana kama ni mawalii. Uchawi na unajimu (utabiri wa nyota) ulisambaa pia. Hakuna aliyekataza ‘iIbaadah potofu hizo kwani watu walikuwa katika kuchuma manufaa na starehe za dunia zaidi na wakakhofia kuyapoteza hayo. Hivyo Shaykh akaona umuhimu mkubwa uliohitajika kuwarudisha watu katika manhaj ya Qur-aan na Sunnah. Akaanza kuwalingania watu katika Tawhiyd - kumpwekesha Mwenyezi Mungu  bila ya kumshirikisha na lolote katika ‘ibaada. Akaazimia kujitumikisha peke yake kwa uvumilivu katika konde. Akajua hakuna lolote kitachofaulu kufanyika ila jihaad katika njia ya Allaah.

Sheikh alikumbana na mitihani, misukosuko, na vitisho, lakini alikuwa ameshategemea hali hiyo kumfikia na alikuwa tayari kukabaliana nayo kwani alitambua kuwa hilo ni jambo lisiloepukika kwa kila mlinganiaji kwani ndio hali waliyokutana nayo Manabii wote, na Salafus-Swaalih (waja wema waliotangulia).

Miongoni mwa mitihani aliyokumbana nayo ni kutokana na Wanavyuoni wadhaifu wasiokuwa na hoja ambao walimpinga na kumfanya akabiliane na misukosuko, vitisho na kukasirikiwa. Pia alikabiliana na misukosuko na mateso chini ya mikono ya madhalimu wa Huraymilaa. Na alipowashawishi watawala wahukumu madhalimu kwa Shariy’ah ya Kiislamu, ilisababisha baadhi ya watu kuyaweka maisha yake hatiani lakini Mwenyezi Mungu Alimnusuru.

Aliamua kurudi kwao ‘Uyaynah, ambako kipindi hicho kulikuwa chini ya utawala wa mtoto wa Mfalme ‘Uthmaan bin Muhammad bin Mu’ammar, ambaye alimpokea Sheikh kwa ukarimu na kumuahidi kumuunga mkono na kumsaidia kuwaita watu katika Uislam. Akaendelea kufundisha na kutoa da’wah hatimaye akashawishika kidhati na kwa vitendo kuondoa dini ya miungu mingi pale alipoona baadhi ya watu ni wagumu kurudi katika Uislamu. Aliweza kumshawishi gavana wa mji huo kulivunja zege lililojengewa juu ya kaburi la Zayd bin Al-Khattwaab ambaye alikuwa ni kaka wa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhi za Allah ziwe juu yake. Akavunjavunja mangome mengineyo, mapango, miti n.k. Akaamrisha Shariy’ah ya Kiislamu itekelezwe kama kumpiga mawe hadi afe mwanamke aliyekiri uzinifu.

Sheikh aliendelea na harakati zake za kauli na ‘amali ambazo zilimfanya azidi kuwa maarufu. Hatimaye akawa Jaji (Qaadhwiy) wa mji wa ‘Uyaynah. Lakini hakuweza kuendelea hapo kwani Mfalme alishawishiwa na viongozi wa miji ya jirani amuue Shaykh kwa vile hawakupendezewa na da’wah yake. Ikabidi afukuzwe katika mji huo.

Akakaribishwa mji wa Ad-Dir’iyyah ambao ulikuwa ni jirani yake. Huko akakaribishwa ingawa kwanza alitiliwa shaka. Alifikia kwa mja mwema aliyempokea ila alimkhofia kutokukubaliwa na mtoto wa Mfalme Muhammad bin Sa’uwd. Habari zikamfikia kwanza mke wa Ibn Sa’uwd ambaye alikuwa mkarimu na mwenye taqwa. Akamfahamisha mumewe kwa kumwambia, “H tawfiyq kubwa umeletewa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ﷻ mtu ambaye anawaita watu katika Uislamu, anawaita katika Qur'ani na Sunnah za Mtume wa Mwenyezi Mungu . Tawfiyq iliyoje? Mkimbilie haraka na umuunge mkono wala usimpinge au kumkataza kwa hayo”. Muhammad Ibn Sa’uwd akakubali ushauri wa mkewe na akaenda kwa Sheikh na akafanya mkataba naye kwamba asiondoke nchini hapo. Ndipo Shaykh akaweka makazi yake hapo na kuendelea na da’wah. Akaendelea na harakati za Da’awa hapo Dar’iyyah. Akaheshimika na kupendwa mno na akaungwa mkono na watu. Da’awa yake iliwaathiri na kuwapendezea mno watu. Ikaenea katika nchi za Kiislamu na nyinginezo. Wakimiminika watu kufika hapo Dar’iyyah kujifunza kwake.

Kama ijulikanavyo kila jema halikosi mitihani. Wakatokeza wapinzani na waliokuwa na chuki naye. Kulikuweko waliompinga da’wah yake ya kuondosha shirki na bid’ah na kuwaita watu katika Tawhiyd. Na wengineo waliompinga kabisa ni kwa sababu ya kuhofu kufukuzwa katika nafasi au vyeo vyao vya kazi. Kwa hiyo wengine walimpinga kwa ajili ya Dini, na wengine walimpinga kisiasa. Wapinzani wake walimzushia ya kumzushia walifika hadi kudai kwamba Sheikh alikuwa ni mfuasi wa Khawaarij. Na mara nyingine wakimlaumu bure bila ya dalili na nje ya upeo wa elimu zao. Hivyo yakaweko malumbano na majibishano yaliyoendelea katika mijadala kadhaa. Sheikh aliwaandikia kuwajibu madai yao, na wao walimrudishia majibu na yeye akawa akiwathibitishia ufahamu wao mbaya wa shariy’ah na Dini kwa ujumla kwa dalili. Ndipo wingi wa maswali na majibu yakawajumuisha watu na wakazidi kuongezeka. Baadhi ya mijadala hiyo iliandikwa na kuchapishwa katika vitabu.

ATHARI YA DA'AWA YAKE 

Da’awa yake ya takriban miaka 50 imedhihirika na kuleta athari kubwa kwanza kwa Waislamu wa zama hizo. Watu waliacha kuabudu makaburi, miti, mawe, majini, waliacha utabiri wa nyota na kila aina ya shirki. Imewatoa pia watu katika ujinga wa kufuata mila za mababu bila ya dalili. Maamrisho ya mema na makatazo ya maovu yakalinganiwa katika Misikiti. Na hapo msimamo wa Qur'ani na Sunnah ukahuishwa na shirki na Bid’ah zikatoweka. Amani na utulivu ukawafunika watu kila mahali. Na mpaka sasa da’wah yake imekuwa na umuhimu mkubwa katika jamii ya Kiislamu. Vijana khasa kutoka nchi za Magharibi na zaidi wale wanaosilimu wamekuwa na hamasa na shauku kubwa ya kujifunza Dini iliyo sahihi na si ile iliyochanganywa na shirki na bid’ah. Kwa hiyo, mafundisho ya msimamo wake wa Ahlus-Sunnah wal-Jama’ah yamekuwa kipaumbele katika lengo la kutafuta elimu kwa Waislamu watakao na wapendao haki.

KAZI ZAKE

Ameandika vitabu vingi vya mafunzo mbali mbali lakini alitilia mkazo zaidi katika somo la Tawhiyd na ‘Aqiydah. Na alitumia hikmah ya kuandika vitabu vidogo vidogo lakini vilivyokusanya nukta muhimu kabisa. Vilikuwa ni mukhtasari wa maudhui aliyotaka kuidhihirisha. Na vitabu hivyo vimekuja kufafanuliwa kwa kushereheshwa na ‘Ulamaa kadhaa na vimekuwa vina umuhimu mno katika vyuo vya Kiislamu vinavyofuata mwendo wa Ahlus-Sunnah wal-Jama’ah.

Vifuatavyo ni baadhi ya vitabu vyake maarufu. Vinne vya mwanzo ni ambavyo mashuhuri zaidi. Na vinginevyo vimekusanywa na kujumuishwa katika ‘Maj’muw’at Mu-allafaatil-Imaam Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab’.

1. Kitaabut-Tawhiyd - kitabu hiki kimekuwa mashuhuri mno na kimeenea sana na somo lake limekuwa ni lenye kutoa mafunzo muhimu kuhusu kumpwekesha Allaah na kuepukana na shirki.

2. Al-Uswuul Ath-Thalaathah – kitabu kitoacho mafunzo kuhusu asili au misingi ya Uislamu.

3. Al-Qawaaid Al-Arba’ - kinatoa mafunzo ya kanuni za ufahamu wa shirki kwa ujumla.

4. Kashf Ash-Shubuhaat - kinakanusha hoja zinazojulikana na watetezi wa shirki na bid’ah.

5. Mukhtaswar Al-Inswaaf was-Sharh Al-Kabiyr

6. Mukhtaswar Zaad Al-Ma’aad

7. Mukhtaswar As-Siyrah

8. Mukhtaswar al-Fat-h

9. Masaail Al-Jaahiliyyah

10. Adaab Al-Mashiy ilaa as-Swalaah

11. Nawaaqidhw Al-Islaam

WANAFUNZI WAKE 

Alikuwa na wanafunzi wengi mno. Miongoni mwao ni watoto na wajukuu wake ambao waliendeleza kazi yake ya da’wah na Jihaad katika njia ya Mwenyezi Mungu, walifungua vyuo karibu na kwao wakifunza watu masomo ya Dini. Kati ya watoto wake ni Husayn, ‘Aliy, ‘Abdullaah na Ibraahiym. Na kati ya wajukuu wake ni ‘Aliy bin Husayn, na pia ‘Abdur-Rahmaan bin Hasan aliyeandika kitabu cha ‘Fat-h Al-Majiyd Sharh Kitaab At-Tawhiyd’. Wanafunzi wake wengineo ni ‘Abdul-‘Aziyz bin Muhammad bin Sa’uwd, Hamad bin Naaswir bin Mu’ammar na ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdillaah bin Husayn.

FAMILIA YAKE 

Alikuwa na watoto sita; Husayn, ‘Abdullaah, Hasan, ‘Aliy, Ibraahiym, ‘Abdul-‘Aziyz. Shaykh anatokana na kizazi kinachojulikana kwa ‘Aal-Sheikh’ ambacho kimetoa Wanavyuoni kadhaa akiwemo Sheikh Muhammad bin Ibraahiym Aal-Sheikh aliyekuwa Mufti mkuu wa awali Saudi Arabia na Sheikh ‘Abdul-‘Aziyz Aal-Sheikh ambaye ni Mufti mkuu wa sasa.

KIFO CHAKE 

Alifariki mwaka 1206 H (1792 M) akiwa na umri wa miaka 91. Rahmah za Allaah ziwe juu yake na Mwenyezi Mungu amuingize Pep ya Firdaws. Amiin.


 

LOGOISLAM

Search Videos

RSS Content

<

 

 

Visitors Counter

6487105
TodayToday211
Highest 12-07-2024 : 5072
US
Guests 51

Mkurugenzi na naibu wake

SS10

 

VIKAO VYA OFISI

title_676e572c3975b21002450911735284524
title_676e572c3984618995593421735284524
title_676e572c399295117024941735284524

NISHATI ZA OFISI

title_676e572c3b06411153331631735284524
title_676e572c3b1584312109401735284524
title_676e572c3b23c15740847021735284524 Add content here

HUDUMA MPYA

: 4 + 1 =

IslamChoice- Kiswahili

Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi‎ kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.

UongofuUongofu.com