SOMO LA FIQHI
Namna ya Kufanya Umrah
1. Atakayefanya Umra afikapo mahali pa kuhirimia, ataoga, atajitia manukato, atavaa mavazi ya kuhirimia na atanuilia Umra hali ya kusema:
[لبيك عُمْرَة]
[Tunakuitikia kwa ibada ya Umra].
2. Ataanza kuleta Talbiya (Labeka), Sheria imeweka aseme:
[لَبَّيْكَ اللَّهُمَّ لَبَّيْكَ، لَبَّيْكَ لَا شَرِيكَ لَكَ لَبَّيْكَ، إِنَّ الْحَمْدَ وَالنِّعْمَةَ لَكَ وَالْمُلْكَ، لَا شَرِيكَ لَكَ]
[Tunakuitikia kwa ibada ya Umra.tumekuitikia! Sifa njema na neema ni zako na ufalme! Huna mshirika!] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
Na ataendelea kuleta Labeka mpaka aione Alkaba na alisalimie Jiwe Leusi.
3. Atakwenda aingie Msikiti wa Haram, aanze kwa mguu wake wa kulia na aombe dua ya kuingia msikitini.
بسم الله ، والصلاة والسلام على رسول الله ، اللهم اغفر لي ذنوبي ، وافتح لي أبواب رحمتك ، أعوذ بالله العظيم ، وبوجهه الكريم ، وبسلطانه القديم من الشيطان الرجيم،
4. Anaikata Labeka na aanze kutufu Alkaba, kuanzia kwenye Jiwe Leusi, alishike na alibusu ikiwezekana- ikiwa haikuwezekana ataliashiria kwa mkono wake na atasema:
[Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mkuu. Ewe Mola! Ninatufu Kwa kukuamini Wewe na kukiamini Kitabu Chako, na kwa kutekeleza ahadi Yako na kwa kufuata mwendo wa Nabii Wako Muhammad ﷺ].
5. Atafanya twawafu mara saba huku Alkaba ikiwa upande wake wa kushoto, akianzia kwenye Jiwe Leusi na kumalizia hapo.
6. Imesunniwa kwa mwanamume atembee kwa haraka katika mizunguko mitatu ya mwanzo.na afunguwe bega lake la mkono wa kulia
Masharti ya kutufu
Inashurutiswa kwa mwenye kufanya Twawafu: kutia nia na kujitoharisha na kusitiri tupu, na azunguke mara saba, na aanze kwenye jiwe leusi, na aijaliye Alkaba upande wake wa kushoto na afuatanishe bena ya mzunguko ila inapo kimiwa swala au ikiswaliwa janaza ataswali kisha ataendelea pale alipokoma kwenye twawafu yake, na aizunguke alkaba yote lau ataingia kwenye hijri haitosihi twawafu yake kwa sababu hijri ni katika Alkaba.
7. Ataomba atakalo katika kutufu. Na akikaribia Nguzo ya Upande wa Yamani aishike kwa mkono na apige takbiri. Akitoweza atoiashiria na hatopiga takbiri. Na akiwa baina ya Nguzo ya Upande wa Yamani na Jiwe Leusi aseme:
[رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ]
[Mola wetu! Tupe jema la ulimwenguni na jema la Akhera na utuepushe na adhabu ya Moto] [Imepokewa na Abuu Daud]
8. Baada ya kutufu Alkaaba ataswali rakaa mbili nyuma ya Makaam Ibrahim - ikiwezekana kama haikuwezekana ataswali sehemu yoyote msikitini atasoma katika Rakaa ya kwanza suratul Fatiha na (suratul Kaafirun) na katika rakaa ya pili atasoma suratul Faatiha na (suratul Ikhlaas).
9. Atatoka kuelekea Jabali la Swafaa, akilikaribia atasoma neno la Mwenyezi Mungu Aliyetukuka:
إِنَّ ٱلصَّفَا وَٱلْمَرْوَةَ مِن شَعَآئِرِ ٱللَّهِ ۖ فَمَنْ حَجَّ ٱلْبَيْتَ أَوِ ٱعْتَمَرَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَن يَطَّوَّفَ بِهِمَا ۚ وَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَإِنَّ ٱللَّهَ شَاكِرٌ عَلِيمٌ
[Hakika Swafaa na Marwah ni miongoni mwa sehemu za ibada ya Hija, basi anayehiji au kufanya Umra, si makosa kwake kusai baina hayo mawili. Na mwenye kujitolea kufanya mambo ya kheri, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushukuru, ni Mwingi wa ujuzi] [2: 158].
10. Atapanda juu ya Swafaa na ataelekea Kibla, atainua mikono yake na atamtukuza Mwenyezi Mungu na kumsifu na atasema:
لا إله إلا الله وحده لا شريك لهُ، لهُ الملك ولهُ الحمد وهو على كل شيءٍ قدير، لا إله إلا الله وحده، أنجز وعده، ونصر عبده، وهزم الأحزاب وحده
[Hapana mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Peke Yake, Asiye na mshirika. Ni Wake Yeye ufalme na ni Zake Yeye sifa njema. Na Yeye kwa kila kitu ni Muweza Tunarudi makwetu, tunatubia kwa Mola wetu, tunamuabudu, tunamsujudia na tunamsifu. Mwenyezi Mungu Ametimiza ahadi Yake, Amemnusuru mja Wake na Ameyashinda mapote Peke Yake] [Imepokewa na Bukhari.]
Kisha ataomba baada ya hapo, kisha airudie hiyo dhikiri mara ya pili, kisha aombe, kisha airudie dhikiri mara ya tatu.
11. Atashuka Swafaa akielekea Marwah, aharakishe mwendo wake anapokuwa baina ya alama mbili za rangi ya kijani [Nazo ni alama mbili za mahali alipopakimbia Bibi Haajar kwa kusai baina ya Swafaa baina na Marwah], apande Marwah na atafanya namna hiyo akiwa Swafaa.
12. Atasai baina ya Swafaa na Marwah mara saba.
13. Baada ya kusai, Mwanamume atapunguza nywele zake za kichwa kwa namna ya kuonekana wazi kuwa zimepunguzwa. Na mwanamke atapunguza kwenye pambizo zote za nywele za kichwa chake kadiri ya ncha ya kidole.
Na lililo bora kwa Mwanamume ni kunyoa, kwa hadithi iliyothibiti kutoka kwa Abu Huraira Radhi za Allah ziwe juu yake kwamba alisema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ Alisema:
[اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِلْمُحَلِّقِينَ، قَالُوا: وَلِلْمُقَصِّرِينَ؟ قَالَ: اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِلْمُحَلِّقِينَ، قَالُوا: وَلِلْمُقَصِّرِينَ؟ قَالَهَا ثَلَاثًا، قَالَ: وَلِلْمُقَصِّرِينَ]. [رواه البخاري]
[Ewe Mola! Warehemu walionyoa. Wakasema: ” na waliopunguza pia?” Akasema: “Ewe Mola! Warehemu walionyoa.” Wakasema: [Na waliopunguza pia?” Akalikariri hilo mara tatu, kisha akasema “na waliopunguza pia”] [Imepokewa na Bukhari.].
14. Atajitoa kwenye ihramu yake.
Na kwa hivyo atakuwa amemaliza Umra yake.
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.