AR-RAHEEQ AL-MAKHTUM
Makuraishi waliposhindwa kumtoa Mtume Muhammad ﷺ katika lengo lake la kufikisha ujumbe kwa hila walizokuwa wamebuni hapo mwanzo, walikusanyana tena ili kupanga mikakati na mbinu mpya kwa lengo la kuzuia kuenea kwa ujumbe wa Mtume ﷺ, mbinu ambazo tutazieleza kwa ufupi kama ifuatavyo:
1. Kuifanyia Dini maskhara, kuicheza shere, kudhalilisha waumini na kukadhibisha, waliyafanya yote haya ili kuwavunja moyo Waislamu, kuzidhoofisha nguvu zao na kuwaondolea morali wao. Wakamsingizia Mtume ﷺ mambo mengi na kumtuhumu kwa tuhuma za ovyo na mwishoni walifikia hatua ya kusema kuwa ni mwendawazimu:
وَقَالُوا يَا أَيُّهَا الَّذِي نُزِّلَ عَلَيْهِ الذِّكْرُ إِنَّكَ لَمَجْنُونٌ} الحجر:6}
[Na uialisema (kwa istihizai), 'Ewe uliyeteremshiwa mauiaidhal Hakika wewe ni mwendawazimu.] [15:6]
Mapagani wallendelea kumwita mchawi na muongo:
وَعَجِبُوا أَن جَاءَهُم مُّنذِرٌ مِّنْهُمْ ۖ وَقَالَ الْكَافِرُونَ هَٰذَا سَاحِرٌ كَذَّابٌ} ص:4}
[Na walistaajabu kuwajia Muonyaji anayetokana na wao, wakasema makafiri: 'Huyu ni mchawi, muongo.] [38:4]
Wakati wote walikuwa wakimsindikiza na kumpokea kwa mitazamo yenye moto wa chuki na hisia zilizoumuka kwa ghadhabu.
وَإِن يَكَادُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَيُزْلِقُونَكَ بِأَبْصَارِهِمْ لَمَّا سَمِعُوا الذِّكْرَ وَيَقُولُونَ إِنَّهُ لَمَجْنُونٌ} القلم:51}
[Na wale makafiri hukuribia kukutelezesha kwa (ukodozi wa) macho yao, wanaposikia mawaidha (yako) na husema:"Hakika yeye ni mwendawazimu.] [68:51].
Kila mara wanyonge miongoni mwa masahaba wake wanapokuwa wamekaa naye, Mushrikina (wapagani) walikuwa wakiwacheza shere kwa kusema; Hawa ndiyo walio katika baraza lake:
أَهَٰؤُلَاءِ مَنَّ اللَّهُ عَلَيْهِم مِّن بَيْنِنَا ۗ أَلَيْسَ اللَّهُ بِأَعْلَمَ بِالشَّاكِرِينَ} الأنعام: 53}
[Ni hao ndio Mwenyezi Mungu amewafadhilisha miongoni mwetu? Kwani Mwenyezi Mungu hawajui wanao shukuru?
] (6:53).
Walikuwa kama Mwenyezi Mungu ﷻ Anavyo tusimulia:
إِنَّ الَّذِينَ أَجْرَمُوا كَانُوا مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا يَضْحَكُونَ وَإِذَا مَرُّوا بِهِمْ يَتَغَامَزُونَ وَإِذَا انقَلَبُوا إِلَىٰ أَهْلِهِمُ انقَلَبُوا فَكِهِينَ وَإِذَا رَأَوْهُمْ قَالُوا إِنَّ هَٰؤُلَاءِ لَضَالُّونَ وَمَا أُرْسِلُوا عَلَيْهِمْ حَافِظِينَ
[Kwa hakika wale walio kuwa wakosefu walikuwa wakiwacheka walio amini.Na wanapo pita karibu yao wakikonyezana.Na wanapo rudi kwa watu wao hurudi nao wamefurahiNa wanapo waona husema: Hakika hawa ndio khasa walio potea.Na wao hawakutumwa wawe walinzi juu yao.] [83:29 - 33].
2. Kuyapa sura mbaya mafundisho yake, kuyatia shaka na kueneza matangazo ya uwongo dhidi ya Mtume ﷺ, kueneza mambo ya uzushi yasiyopendeza kuhusu mafundisho yake, na kukazana katika kueneza uzushi huo kiasi cha kuwanyima watu wa kawaida uwanja wa kuuzingatia wito wake. Kuhusu Qur'ani wakawa wanasema:
وَقَالُوا أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ اكْتَتَبَهَا فَهِيَ تُمْلَىٰ عَلَيْهِ بُكْرَةً وَأَصِيلًا} الفرقان:5}
[Na wakasema: Hivi ni visa vya watu wa kale alivyo viandikisha, anavyo somewa asubuhi na jioni.] [25: 5]
Wakati mwingine wakisema:
{وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِنْ هَٰذَا إِلَّا إِفْكٌ افْتَرَاهُ وَأَعَانَهُ عَلَيْهِ قَوْمٌ آخَرُونَ ۖ فَقَدْ جَاءُوا ظُلْمًا وَزُورًا} الفرقان:4}
[Na wamesema walio kufuru: Haya si chochote ila ni uzushi alio uzua, na wamemsaidia kwa haya watu wengine! Hakika hawa wamekuja na dhulma na uwongo.] (25:4).
Pia walikuwa wakisema:
وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّهُمْ يَقُولُونَ إِنَّمَا يُعَلِّمُهُ بَشَرٌ} النحل:103}
[Na Sisi hakika tunajua kwamba wanasema: Yuko mtu anaye mfundisha.] [16:103]
Kuhusu yeye mwenyewe Mtume ﷺ alikuwa akiambiwa:
{مَالِ هَٰذَا الرَّسُولِ يَأْكُلُ الطَّعَامَ وَيَمْشِي فِي الْأَسْوَاقِ} الفرقان:7}
[Mtume gani huyu ? Anakula chakula, na anatembea masokoni! Mbona hakuteremshiwa Malaika akawa mwonyaji pamoja naye?] [25:7]
Ndani ya Qur'ani imo mifano mingi sana kwa ajili ya kujibu hoja zilizokuwa zikiibuliwa na wapagani, kwa kuzinakili au bila ya kuzinakili.
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.