AR-RAHEEQ AL-MAKHTUM
Katikati ya masiku haya, Makuraishi walishughulishwa na jambo jingine, nalo ni kuwa msimu wa Hijja ulikuwa ukikaribia na Makuraishi walikuwa wakielewa kuwa makundi ya Waarabu yatawasili kama ilivyokuwa ada, nao walikuwa wakikhofu juu ya wao kufikishiwa ujumbe, na kwa sababu hiyo wakaona hakuna njia isipokuwa ni lazima pawe na maneno maalumu ambayo watayasema dhidi ya Muhammad ﷺ, ili Da'wa yake isiwe na athari yoyote katika nafsi za Waarabu.
Makuraishi walikusanyana kwa AI-Walid bin Al- Mughirah kwa ajili ya kujadiliana kuhusu maneno ambayo watayasema ili kufanikisha azma yao.
Al-Walid akawaeleza, katika jambo hili mnatakiwa kukubaliana na rai moja na msitofautiane kwa kukadhibishana wenyewe kwa wenyewe. Wakamtaka atoe rai yake kwanza, naye akawaambia kuwa waseme wao kwanza rai waliyonayo, wakasema: 'Tutawaambia watu kuwa yeye ni kuhani', Akasema: 'Hapana, Ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu ﷻ yeye si kuhani, kwa hakika tumewahi kuwaona makuhani, na maneno yake hayana sifa za kikuhani, kwa namna yalivyo na mpangilio mzuri.' Wakasema: 'Tutasema kuwa yeye ni mwendawazimu.' Al- Walid akasema: 'Hatuwezi kudai kuwa 'yeye ni mwenda wazimu, kwani tumewahi kuuona uwendawazimu na kuuelewa, hatuwezi kuaminika kwa maelezo hayo.' Wakasema: 'Tutawaeleza watu kuwa ni mshairi.' Akasema, 'Hapana yeye si mshairi, kwa hakika tunayajua mashairi yote, naye msamiati wake sio wa kishairi,hapana vina, mizani wala muwala (Hivi ni baadhi ya vipengele vya mashairi ya Kiarabu), hivyo Muhammad hawezi kuwa mshairi.' Wakasema: 'Tutasema yeye ni hawezi kuwa mshairi.' Wakasema: 'Tutasema yeye ni mchawi.' Akasema, 'Hapana yeye si mchawi, kwani sisi tumekwisha kuwaona wachawi wangapi? na uchawi wao haukuwa kitu isipokuwa upuliziaji na ufungaji wa mafundo. Wao sasa wakahoji: 'Tuseme nini basi?' Akasema; "Ninaapa kwa Jina la Mwenyezi Mungu ﷻ kwa hakika maneno yake ni matamu na kwa hakika shina lake lina rutuba, na kwa hakika tawi lake lina matunda, na nyinyi hamuwezi kusema chochote isipokuwa watu watafahamu kuwa hilo ni batili."
Kwa hakika maneno yaliyokaribu na jambo hilo ambayo mnaweza kuyasema ni kusema kuwa ni mchawi, amekuja na maneno ambayo ni uchawi wa kutenganisha mtu na baba yake, kati ya mtu na ndugu yake, kati ya mtu na mke wake na kati ya mtu na jamaa zake. Wakatawanyika kutoka kwake, wakiwa wamekubaliana juu ya hayo.
Baadhi ya mapokezi yanafahamisha kuwa baada ya AI- Walid kuyakataa yote waliyopendekeza, walimtaka awatajie maoni yake ambayo yangewafaa katika shaurillile, hapo ndipo alipowaambia wampe muda mpaka kwanza afikiri. -Al-Walid alifikiri kitambo na mwisho ndio akaja na rai ambayo tayari tumekwisha itaja. (1)
Kuhusu Al-Walid, Mwenyezi Mungu ﷻ Ameteremsha aya kumi na sita katika Surati Al-Muddathir kutokea aya ya 18 - 25 na ndani ya aya hizo Ameonyesha sura ya namna ya kufikiri kwake, kwa Kusema:
إِنَّهُ فَكَّرَ وَقَدَّرَ فَقُتِلَ كَيْفَ قَدَّرَ ثُمَّ قُتِلَ كَيْفَ قَدَّرَ ثُمَّ نَظَرَ ثُمَّ عَبَسَ وَبَسَرَ ثُمَّ أَدْبَرَ وَاسْتَكْبَرَ فَقَالَ إِنْ هَٰذَا إِلَّا سِحْرٌ يُؤْثَرُ إِنْ هَٰذَا إِلَّا قَوْلُ الْبَشَرِ
[Kwani hakika yeye alifikiri na akapima.Basi ameangamia! Vipi alivyo pima!Tena ameangamia! Vipi alivyo pima!Kisha akatazama,Kisha akakunja kipaji, na akanuna.Kisha akaipa kisogo haki, na akatakabari.Na akasema: Haya si chochote ila ni uchawi ulio nukuliwa.Haya si chochote ila kauli ya binaadamu.]
Baada- ya baraza kukubaliana kuhusu maamuzi haya waliingia katika kuyatekeleza. Walichofanya ni kukaa katika njia inayopitwa na watu wengi wakati wa msimu wa Hijja, na walikuwa hapiti mtu yeyote katika njia hiyo isipokuwa walimtahadharisha kuhusu Mtume ﷺ na kumtajia mambo yake.(1) Kiongozi wa jambe hilo alikuwa Abu Lahab.
Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ﷻ alikuwa na tabia ya kuwafuata watu majumbani mwao, katika soko la 'Ukadha, Mijannnah na Dhil Majazi, wakati wa msimu wa Hijja na kuwaita kwa Mwenyezi Mungu ﷻ. Abu Lahab alikuwa akimfuata nyuma yake huku akisema; 'Msimtii, huyu ameacha dini ya wazazi wake na ni mrongo.(2)
Hatua hii iliwafanya Waarabu kuondoka na ujumbe wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ kutoka katika msimu huo na ukaenea utajo wake katika miji ya yote ya Waarabu.
1) Ibn Hisham, Juzuu 1, Uk. 275.
2) Ahmad, Juzuu 3, Uk. 492; Juzuu 4, Uk. 341.
2) Arraheeq Al Makhtum Uk 136
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.