KWENDA KWA WARAQAH BIN NAWFAL
Khadija (r.a) akaondoka na kwenda naye kwa Waraqah bin Nawfal bin Assad bin Abdul-Uzza, mtoto wa ammi yake Khadija. Huyu alikuwa ni mkristo wakati wa Jahiliyyah na alikuwa akiandika Injili kwa lugha ya Kiebrania, yale ambayo Mwenyezi Mungu ﷻ Ametaka Ayaandike. Alikuwa ni Mzee kikongwe kipofu, akamwambia Khadija (r.a); 'Ewe mtoto wa ammi yangu, sikiliza kutoka kwa mtoto wa ndugu yako', Waraqah akamwuliza, "Ewe mtoto wa ndugu yangu unaona nini?' Akamwelezea kuhusu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ﷺ na kheri ya mambo ambayo ameyaona, Waraqah akamwambia, 'Huyo ndiye Namus (Mjumbe) ambaye Mwenyezi Mungu ﷻ Alimteremsha kwa Musa (a.s), ninatamani niwe hai wakati watakapokutoa jamaa zako.' Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. akauliza, 'Hivi watanifukuza?' Akajibiwa, 'Ndiyo', hajawahi kutokea mtu mfano wa vile ulivyokuja wewe, na asifanyiwe uadui. Iwapo nitakuwa hai mpaka wakati huo, nitakunusuru.' Baada ya siku hiyo Waraqah hakuishi siku nyingi, akafariki dunia na wahyi ukakatika.
Imamu Tabari na Ibni Hisham wamepokea maneno yanayoashiria kuwa, alitoka katika pango la Jabal Hiraa, baada ya kushtukizwa na Wahyi, kisha akarejea Jabalini, na baada ya hapo alirejea Makka. Upokezi wa Tabari, unaelezea tukio hili kama ifuatavyo:
"Mjumbe wa Mwenyezi Mungu amesema: 'Baada ya kuja kwa wahyi, hakukuwa katika viumbe wa Mwenyezi Mungu ﷻ anayenichukiza zaidi kuliko mshairi au mwenda-wazimu, nilikuwa siwezi kuwaangalia,' 'Kwa hakika lililo mbali sana - akikusudia nafsi yake-ni matamko ya mshairi au mwenda wazimu, isipokuwa Makuraish wameyazungumza hayo kwa kuninasibisha nayo. Nitapanda juu kileleni na kujitupa chini na kufa,nikapumzika.
Nilitoka nikiwa ninalikusudia jambo hilo mpaka nilipokuwa katikati ya Jabali, nilisikia sauti kutoka mbinguni ikisema: 'Ewe Muhammad! Wewe ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na mimi ni Jibril (a.s): Anasema: 'Nikakinyanyua kichwa changu kutazama mbinguni ghafla nikamuona Jibril (a.s) akiwa katika sura ya mtu, amekita nyayo zake kaiika upeo wa macho akisema; "Ewe Muhammad, wewe ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na mimi ni Jibril (a.s). Nilisimama nikimwangalia, likanishughulisha hilo na kusahau yale ambayo nilikuwa nimeyakusudia. Ikawa siendi mbele wala sirudi nyuma, nikawa ninaugeuza uso wangu nikimwangalia katika pambizo za mbingu, kila upande nilioutizama niliendelea kumwona katika umbile lilelile, nilibakia palepale, mpaka Khadija (r.a) akawatuma watu waanze kunitafuta. Walifika mpaka Makka na kurejea, na wakati wote huo nilisimama pale pale. Baada ya muda huo ndipo Jibril (a.s) akaondoka, na mimi pia nikaondoka na kurejea nyumbani. (1)
Nilikaa karibu na Khadija. Khadija akaniuliza; 'Ewe Abal Qasim ulikuwa wapi? Naapa kwa Jina la Mwenyezi Mungu ﷻ niliwatuma wajumbe kukutafuta mpaka Makka wakarejea baada ya kukukosa,' 'Nikamweleza yale niliyoyaona." Akasema, 'Furahi ewe mtoto wa ammi yangu, ninaapa kwa Mwenyezi Mungu ﷻ ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake, kwa hakika . ninatarajia umepewa Utume wa Umma huu.(2)
Akasimama akaenda kwa Waraqah na kumweleza. Waraqah ,akasema:
قدوس قدوس، والذي نفس ورقة بيده لقد جاءه الناموس الأكبر الذي كان يأتي موسى، وإنه لنبي هذه الأمة، فقولي له: فليثبت
"Mtakatifu, Mtakatifu, ninaapakwa yule ambaye nafsi ya Waraqa imo mikononi mwake, kwa hakika kajiwa na Namus Malaika aliyetumwa kwa Musa (a.s). Hakika yeye ni Mtume wa Umma huu kwahivyo mwambie na atulizane,"
Khadija akarejea na akamweleza Mtume maneno ya Waraqah.
Wakati Mtume ﷺ alipomaliza muda wake wa kukaa kule katika Jabal Hiraa, na kurudi Makka alikwenda na kukutana na Waraqa, na akasema baada ya kumsikia: 'Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake, kwa hakika wewe ni Mtume wa Umma huu, aliyekujia ni Mjumbe mkuu ambaye alitumwa pia kwa Musa {a.s).*
1) Tabari, Juzuu 2., Ilk. 207
2) 1bn Hisham, juzuu I, Uk. 237~238.
*Arraheeq Al Makhtum 104-105
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.