KWA NINI ULIITWA MWAKA ALIOZALIWA MTUME ﷺ MWAKA WA NDOVU?
Umeitwa mwaka wa Ndovu kwa sababu mwaka kulitokea kisa muhimu sana cha kutaka kuvundwa Al-Ka'aba na mfalme wa habash,na kisa chenyewe ni kama kifuatavyo.
Kisa cha mwaka wa tembo kinaanzia pale Abraha mfalme wa Habashah na Yaman alipowaona Waarabu wakihiji Makkah na ibada hii ya Hijjah ikaufanya mji wa Makkah kuwa ni kitovu cha biashara .
Abraha Mhabashi aliyekuwa gavana wa Al Najashi katika nchi ya Yemen alidhamiria kuihamisha ibada hii ya Hijjah kutoka Makkah na kuipeleka katika milki ya himaya yake ya Yaman.
Ili kuutekeleza mkakati wake huu akajenga kanisa kubwa sana katika mji wa Sana-a na kulipamba kwa mapambo ya fakhari ili watu wavutike na kuja kufanya ibada ya Hijjah hapo.
Baada ya ujenzi huo, akawaamrisha watu waje kuhiji hapo, amri hii ikawa nzito kwa Waarabu kuitekeleza na hawakuiridhia.
Ili kuonyesha chuki yao dhidi ya amri hii alitoka mtu mmoja wa kabila ya bani kinaanah akaja kufanya haja kubwa ndani ya kanisa lile.
Kitendo hiki cha kulichafua kanisa kilimkasirisha sana Mfalme Abraha, hasa baada ya kugundua kwamba mhusika wa kitendo hicho ni mtu kutokea pande za Makkah.
Akaandaa jeshi kubwa idadi yake askari wapatao elfu sitini pamoja na tembo ishirini na mbili yeye mwenyewe akiwa juu ya tembo mkubwa sana, aliekuwa akiitwa (Mahmud) na kuelekea nalo Makkah kwa ajili ya kuibomoa Al-Ka’abah.
Waarabu wa Makkah waliogofya sana na jeshi lile. Jeshi la Abraha lilipofika katika viunga vya mji wa Makkah likawakuta ngamia, kondoo na mbuzi wa watu wa Makkah na wengine walikuwa ni milki ya babu yake Mtume Mzee Abdul-Mutwalib, Abraha awachukua wanyama wale wote.
Mzee Abdul-Mutwalib kiongozi wa kabila la Kikurayshi, mtumishi wa Al-Kaab na mtawala wa Makkah akamuendea Abraha na kumtaka amrejeshee wanyama wake aliowachukua Abraha akamshangaa sana Mzee Abdul – Mutwalib akamwambia:
"Mimi nilitazamia umekuja kuniomba nisiivunje Al-Kaab, kumbe umekuja kunitaka nikurudishie wanyama wako!" Mzee Abdul – Mutwalib akamjibu:
[أنا رب الإبل وللبيت رب يحميه]
[Mimi wa kwangu ni hawa wanyama, ama hii nyumba yupo mwenyewe atayeihami].
Abraha akamregeshea Wanyama wake,na kurudi nao, na aliporudi Abdul-Mutwalib akawataka watu wa Makkah watoke nje ya Makkah ili wasishuhudie kitendo kama hicho.
Abrah Alipowasili penye bonde la Muhsir baina ya Makkah na Muzdalifa (baina ya Muzdalifa na Mina), tembo alipiga magoti na kukataa kuendelea na safari ya kuelekea Makkah. Wakawa kila wanapomuelekeza kusini au kaskazini anainuka na kutembea, lakini wanapomuelekeza upande wa Makkah anakataa na kupiga magoti.
Wakabaki katika hali hiyo mpaka pale Mwenyezi Mungu Alipowapelekea ndege makundi kwa makundi, wakawapiga kwa mawe ya udongo unaounguza.
Jiwe likimpata mtu anasagikasagika yeye na tembo wake na kuwa kama majani yaliyoliwa na wadudu kama tunavyosoma ndani ya Qur'ani.
Mwenyezi Mungu Anasema:
أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِأَصْحَابِ الْفِيلِ أَلَمْ يَجْعَلْ كَيْدَهُمْ فِي تَضْلِيلٍ وَأَرْسَلَ عَلَيْهِمْ طَيْرًا أَبَابِيلَ تَرْمِيهِم بِحِجَارَةٍ مِّن سِجِّيلٍ فَجَعَلَهُمْ كَعَصْفٍ
مَّأْكُولٍ
[Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo watenda wale wenye tembo?Kwani hakujaalia vitimbi vyao kuharibika?Na akawapelekea ndege makundi kwa makundi,Wakiwatupia mawe ya udongo wa Motoni,Akawafanya kama majani yaliyo liwa!] [Al Fiil:1-5]
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.