KUZALIWA KWA BWANA MTUME MUHAMMAD ﷺ.
Bwana Mtume – ﷺ – alizaliwa katika mji wa Makkah, siku ya Jumatatu mwezi wa mfungo sita, mwaka wa tembo sawa na tarehe 20 ya mwezi April mwaka 571 – Miyladia (tangu kuzaliwa Nabii Issa).
Bwana Mtume alizaliwa hali ya kuwa ni yatima kwani baba yake alikufa akimuacha mkewe ana mimba ya Mtume.
Mama yake alipojifungua tu alimpeleka mjumbe kwa babu yake Mtume Mzee Abdul -Mutwalib kumpa khabari njema za kuzaliwa mjukuu wake. Mzee Abdul – Mutwalib akafurahikia sana mjukuu wake akamchukua na kumzungusha katika Al-Ka'aba kisha akamuomba Mwenyezi Mungu na kumshukuru na kisha akamchagulia mjukuu wake jina la MUHAMMAD (jina hili halikuwa maarufu kwa waarabu kipindi hiko) na kisha akamkhitani(kumtahiri) baada ya siku 7.
ASUBUHI NJEMA
Jua lilichomoza kwa furaha asubuhi ile pale Makkah. Bali ulimwengu mzima ulijaa furaha siku ile. Kila kitu kilifurahi kwa sababu mtoto amezaliwa katika mji wa Makkah, na mtoto huyo hakuwa mtoto wa kawaida. Mtoto huyo ni zawadi iliyotoka kwa Allaah kwa ajili ya wanaadamu. Mtoto huyo alikuwa mfano mwema na ruwaza njema iliyokuja kueneza mapenzi na huruma na uadilifu baina ya viumbe. Amezaliwa Mtume aliyekuja kuingiza furaha na tumaini ndani ya nyoyo zilizokwisha kata tamaa, na kuziongoza nyoyo hizo katika uongofu na imani, na kuzitoa katika giza na kuziingiza katika mwangaza.
Ilikuwa asubuhi njema kupita zote ulimwenguni. Asubuhi ya furaha na vifijo na vigelegele, aliyozaliwa ndani yake Mtume wa Allaah ﷺ, kipenzi cha Allaah na mbora wa viumbe vyote.
Hata Malaika waliifurahia siku ile kwa kuzaliwa Mkweli mwaminifu, mpole, mkarimu, shujaa, mchaji Allaah, Rahma kwa walimwengu aliyekuja kuwatoa watu kutoka katika giza la kufru na kuwangiza ndani ya nuru itokayo kwa Allaah.
Amezaliwa yule ambaye ulimwengu ulikuwa ukimsubiri. Kiumbe aliyebeba kila sifa njema asizokuwa nazo kiumbe mwingine. Mtume mtukufu, muaminifu, muungwana, mwenye kila sifa ya ubinaadamu, fadhila, ucha Allaah, moyo mkubwa, na tabia njema ya hali ya juu isiyoweza kufananishwa na kiumbe kingine.
Bali kila kiumbe kilifurahi. Hata ndege na miti ilifurahi kwa kuwasili kiongozi aliyekuja kuondoa na kuufuta ukafiri, ushirikina na ujinga ulimwenguni.
Babu yake ‘Abdul-Mutwallib alifurahi kupita kiasi siku hiyo, akamuambia Bibi Amiynah: "Kipenzi chetu huyu ni urithi wetu huyu kutoka kwa baba yake ‘Abdullaah. Utazame uso wake na macho yake na mdomo wake. Utazame uzuri wake. Kila kitu chake kinafanana na baba yake. Mzuri alioje mtoto huyu kupita watoto wote, aliyewashinda watoto wote kwa uzuri na kupendeza."
Alizaliwa yatima Mtume wa Allaah ﷺ, ambaye baba yake ‘Abdullaah alifariki dunia alipokuwa akirudi Makkah kutoka Shaam alipotamani kupita Madiynah kuwatembelea wajomba zake watu wa kabila la Bani Najjaar wanaoishi huko. Na alipokuwa Madiynah, ‘Abdullaah alipatwa na maradhi, akafariki dunia wakati mwanawe Muhammad ﷺ bado angali tumboni mwa mama yake katika mimba ya miezi sita.(1)
1) Muhammad ﷺ Rahma Kwa Walimwengu.
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.