AR-RAHEEQ AL- MAKHTUUM
Abdullaah, baba yake Mtume wa Allaah Muhammad ﷺ ni mwana wa "Abdul-Muttwallib, na mama yake ni "Fatimh bint Amru bin Aid bin Umran ibn Makhzum bin Yaqadhah bin Murrah,
Na "Abdullah alikuwa ndiye kipenzi cha baba yake ‘Abdul-Muttwallib.
Imeandikwa katika kitabu cha Sirah ya Ibn Hishaam na katika Al-Bidaayah wan Nihaayah kuwa: "Abdul-Muttwallib alipofanikiwa kukifukuwa kisima cha maji ya Zamzam baada ya kufukiwa na watu wa kabila la Jurhum, na kutoa kila kilichofukiwa ndani ya kisima hicho, aliweka nadhiri kuwa akipata watoto kumi atamchinja mmoja wao mbele ya Al-Ka'abah.
Allaah Akamruzuku watoto kumi na majina yao ni; Al-Haarith na Az-Zubayr na Abu Twaalib na "Abdullaah na Hamzah na Abu Lahab na Al-Ghaidaq na Al-Maqum na Sifar na Al-‘Abbaas.
Abdul-Muttwallib akawajulisha wanawe hao juu ya nadhiri yake, na wote wakakubali, akawataka kila mmoja wao aandike jina lake, akayachukua majina hayo na kwenda nayo mpaka penye sanamu la Hubal na kuyapigia kura mahali hapo.
Kura ikamuangukia kipenzi chake katika wanawe na mdogo wao ‘Abdullaah bin ‘Abdil-Muttwallib – baba yake Mtume wa Allaah ﷺ, "Abdul-Muttwallib alipomshika mkono mwanawe huyo kumsogeza karibu na mahali pa kuchinja mihanga mbele ya sanamu la Hubal, akambana chini ya miguu yake tayari kisu mkononi, ndugu zake wote wakamkabili na kumuuliza:
"Unataka kufanya nini ewe ‘Abdul-Muttwallib?”
‘Abdul-Muttwallib akasema: “Nataka kumchinja.”
Ndugu zake wote pamoja na jamaa zake waliohudhuria wakasema:
“WaLlaahi humchinji, na ujuwe kuwa utakapoanza wewe mwenendo huo, basi kila mtu atakuwa akija na mwanawe kutaka kumchinja mahali hapa.”
Inasemekana kuwa ndugu yake Al-"Abbaas ndiye aliyemchomoa "Abdullaah chini ya miguu ya baba yake, lakini "Abdul-Muttwallib hajakubali kuiacha nadhiri yake hiyo bila kuitimiza mpaka walipokubaliana kumuendea mganga maarufu na mpiga ramli anayeishi Hijaaz kumtaka shauri lake, na mpiga ramli huyo akawaambia:
"Pigeni kura baina ya mtoto wenu na ngamia kumi na kama kura itaangukia kwa mtoto ongezeni ngami kumi kisha pigeni kura mara ya pili, na ikimuangukia mtoto wenu tena endeleeni kuongeza ngamia kumi kumi mpaka pale Mola wenu atakaporidhika, kisha muwachinje ngamia wote kwani hapo Mola wenu atakuwa kesharidhika, na mtoto wenu keshaokoka.”
Wote wakakubaliana na shauri hilo, wakaondoka na kurudi Makkah, na mara baada ya kuwasili, "Abdul-Muttwallib akamuomba Allaah kisha wakamsogeza ‘Abdullaah na kuwasogeza ngamia kumi na kuanza kupiga kura, na kila mara kura ilikuwa ikimuangukia ‘Abdullaah. Wakaongeza ngamia kumi wengine, kura ikamuangukia tena ‘Abdullaah. Wakawa wanaongeza ngamia kumi kumi mpaka walipotimia ngamia mia ndipo kura ilipowaangukia ngamia, wakamwendea ‘Abdul-Muttwallib aliyekuwa amesimama mbele ya sanamu la Hubal huku akimuomba Allaah na kumjulisha juu ya matokeo ya kura.[1]
Kisa hiki kinatukumbusha kisa kikongwe kilichojaa mafunzo mengi cha kutaka kuchinjwa Nabii Ismail Bin Ibrahim – Amani ya Allah iwashukie wakati Nabii Ibrahim alipooteshwa usingizini amchinje mwanawe Ismail.
Kwa kuwa ndoto za mitume huwa ni wahyi kwa Mwenyezi Mungu, Nabii ibrahim akaanza kuchukua hatua za kuitekeleza amri ya Mola wake, akamlaza mwanawe ili amchinje ndipo Mola mwingi wa huruma akamkomboa mja wake Ismail kwa kumleta kondoo wa peponi achinjwe badala ya Ismail kama tunavyosoma ndani ya Qur'ani.
فَلَمَّا بَلَغَ مَعَهُ السَّعْيَ قَالَ يَا بُنَيَّ إِنِّي أَرَىٰ فِي الْمَنَامِ أَنِّي أَذْبَحُكَ فَانظُرْ مَاذَا تَرَىٰ ۚ قَالَ يَا أَبَتِ افْعَلْ مَا تُؤْمَرُ ۖ سَتَجِدُنِي إِن شَاءَ اللَّهُ مِنَ الصَّابِرِينَ فَلَمَّا أَسْلَمَا وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ وَنَادَيْنَاهُ أَن يَا إِبْرَاهِيمُ قَدْ صَدَّقْتَ الرُّؤْيَا ۚ إِنَّا كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ الصافات:102-105
[Basi alipo fika makamo ya kwenda na kurudi pamoja naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia wewe, waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyo amrishwa, utanikuta mimi, Inshallah, katika wanao subiri.Basi wote wawili walipo jisalimisha, na akamlaza juu ya kipaji.Tulimwita: Ewe Ibrahim!Umekwisha itimiliza ndoto. Hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao tenda mema.] [Ass'affat:102-105]
Na Imepokelewa hadithi kutoka kwa Bwana Mtume ﷺ akisema:
[أنا ابن الذبيحين]
[Mimi ni mtoto wa wachinjwa wawili ] Nao ni Babu Nabii Ismail, huyu ndiyo mchinjwa wa kwanza na wa pili ni baba yake Mzee Abdallah.
1) Al-Bidaayah wan-Nihaayah – juzuu ya 2 mlango wa ‘Tajdiyd hufar zamzam. Ibn Hishaam juzuu 1, uk. 278 (lafdhi ya Al-Bidaayah wan-Nihaayah) kama ilivyoelezwa na mwana historia Ibn Is-haaq.
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.