SOMO LA FIQHI
Suala: Ni nini Maana ya Makruhi kisheria?
Jawabu: Maana ya Makruhi katika Sheria
Makruhi ni jambo ambalo ukiliwacha unapata Thawabu, na ukilifanya Hupati Dhambi
na Mambo yanaochukizwa katika Udhu ni hayayafuatayo:
1. Ni karaha kwa mwenye kutawadha kuacha suna yeyote miongoni mwa suna tulizozitaja chini ya anuani :[SUNA ZA UDHU].
Kwa sababu kuacha kuzitekeleza suna hizo kutampelekea mtu huyo kukosa thawabu, na Muislamu wa kweli siku zote hupupia kuitekeleza ibada yake kwa ukamilifu na kwa namna ilivyofundishwa na mwenyewe Bwana Mtume ﷺ .
2. Ni karaha kuyatumia maji kwa israfu {fujo} kufanya hivyo ni kinyume na suna ya Bwana Mtume ﷺ na kwa neno lake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
[ولا تسرفوا إنه لا يحب المسرفين} [الأعراف:31}
[Na wala msifanye ubadhirifu. Kwa hakika Yeye hapendi wanao fanya israfu.] [7:31]
3. Ni karaha kutanguliza kuosha mkono/mguu wa kushoto kabla ya mkono/mguu wa kulia, kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume na alivyotenda Bwana Mtume ﷺ.
4. Ni karaha kukausha/kufuta viungo vya udhu kwa kutumia leso/taulo na kadhalika.
Ukaraha huo utaondoka kwa udhuru kama vile baridi kali, hapo itakuwa si karaha. Imepokelewa kwamba Mtume –Rehema na Amani zimshukie – aliletewa leso/taulo (ili ajifutie) basi hakuigusa (hakuitumia)” Bukhari.
5. Kuupiga uso kwa maji pia ni miongoni mwa mambo yaliyo karaha katika udhu. Kwa sababu kitendo hiki kinapingana na utukufu wa uso.
6. Ni karaha kuzidisha kuosha au kupakaza zaidi ya mara tatu au kupunguza. Alisema Mtume ﷺ baada ya kwisha kutawadha mara tatu tatu:
هكذا الوضوء، فمن زاد على هذا فقد أساء وتعدَّى وظلم] رواه أبوداود والنسائي وإبن ماجة]
[Hivi ndivyo (unavokuwa) udhu, basi atakayezidisha zaidi ya hivi au kupunguza huyo atakuwa amekosea na kudhulumu] [Imepokewa Abuu Dawud, na Annasai na Ibnu Maajah]
7. Ni karaha mtu kuoshwa viungo na mtu mwingine bila ya kuwa na udhuru ukubalikao kama ugonjwa.
Hili limefanywa kuwa ni karaha na sheria kwa sababu ndani yake mna chembechembeza kibri na ubwana, vitu ambavyo vinapingana na uja/utumwa kwa Mwenyezi Mungu.
8. Ni karaha kwa aliyefunga kuyapeleka ndani sana maji katika kusukutuwa na kupandisha maji puani.
Hii ni kwa sababu ya kuchelea kumponyoka maji na kufika kooni yakaingia ndani na hivyo kusababisha kufisidika/kuharibika swaumu yake. Amesema Mtume wa Mwenyezi mungu ﷺ.
بالغ في الاستنشاق إلا أن تكون صائمًا] رواه أبودود والترمذي ]
[Na balighisha (yapeleke maji ndani sana) katika kupandisha maji puani, ila ukiwa umefunga (usibalighishe)] [Imeokewa na Abuu Dawud.na Attirmidhiy]
TANBIIH:
Ikiwa imekatazwa kubalighisha katika kupandisha maji puani kwa mfungaji, basi kubalighisha katika kusukutua ni bora zaidi kukatazwa.
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.