SOMO LA FIQHI
Kwa vile ibada ya Funga ilikuwa ikifanywa na watu wa Ahlul Kitab waliotangulia, na Mtume ﷺ alikuwa akipenda kuzifanya ibada zilizokuwa zikifanywa nao kabla ya kufunuliwa Wahyi juu yake, na hasa kwa vile Mtume ﷺ alikuwa akiuelewa umuhimu wa ibada ya Funga, basi yeye ﷺ alikuwa akifunga kabla ya kuletewa Wahyi juu yake kwa hiari yake mwenyewe kabla ya kufaradhishiwa ibada hiyo.
عن عائشة رضي الله عنها أن قريشا كانت تصوم عاشوراء في الجاهلية ثم أمر رسول الله صلى الله عليه وسلم بصيامه حتى فرض رمضان فقال رسول الله صلى الله عليه وسلم : " من شاء فليصمه ومن شاء فليفطره رواه البخاري ومسلم
Kutoka kwa Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha) kuwa Maqureyshi walikuwa wakifunga Ashura zama za ujahiliya kisha Mtume aliamrisha watu wafunge mpaka ilipofaradhiwa Ramadhani Akasema Mtume [Anaetaka na Funge na anaetaka afungue] [Imepokelewa na Bukhari na Muslim]
Katika hadithi nyingine iliyosimuliwa na Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu) amesema:
عن ابن عباس رضي الله عنهما قال : قدم النبي صلى الله عليه وسلم المدينة فرأى اليهود تصوم يوم عاشوراء فقال : " ما هذا ؟ " قالوا : هذا يوم صالح نجى الله فيه بني إسرائيل من عدوهم فصامه موسى قال : " فأنا أحق بموسى منكم " فصامه وأمر بصيامه رواه البخاري ومسلم
[Mtume ﷺ alipoingia mji wa Madina aliwakuta Mayahudi wakifunga siku ya Ashura, akasema;
"Nini hiki?" (Kwa nini mnafanya hivi?)
Wakasema;
"Hii ni siku njema ambayo Mwenyezi Mungu alimuokoa ndani yake Musa na wana wa Israeli (Bani Israil) kutokana na adui yao (Firauni)". Mtume ﷺ akawa anaifunga, na akasema"
[Mimi ananistahiki zaidi Musa kuliko nyinyi] Akafunga na akaamrisha watu kufunga.
[Imepoklewa na Bukhari na Muslim]
Kwa hivyo ibada ya Funga ilikuwepo tokea mwanzo, na Waislam walikuwa wakifunga hata kabla ya kufaridhishwa, lakini mara baada ya kufaridhishwa Funga ya Mwezi wa Ramadhani, ikaachwa Funga ya siku ya Ashura na ikawa anayetaka anaifunga na asiyetaka anaiacha.
Saumu ya Ramadhani ilifaradhishwa katika mwaka wa pili baada ya Hijra pale ilipoteremka kauli ya Mwenyezi Mungu aliyetukuka:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ ۚ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۚ وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ ۖ البقرة:183-184
[Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuchamngu.(Mfunge) siku maalumu za kuhisabika. Na atakaye kuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyengine. Na wale wasio weza, watoe fidiya kwa kumlisha masikini.] [Al Baqarah - 183 - 184]
Tokea siku hiyo Saumu ikawa ni wajibu kwa kuhiyarishwa. Ilikuwa mtu anayetaka anafunga, na hiyo ni bora zaidi kutokana na kauli Yake Subhanahu wa Taala alipoikamilisha aya iliyotangulia kwa kusema:
{فَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ ۚ وَأَن تَصُومُوا خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ}
[Na atakaye fanya wema kwa kujitolea, basi ni bora kwake. Na mkifunga ni bora kwenu, kama mnajua.].
Ama asiyetaka kufunga alikuwa akiruhusiwa kula, lakini lazima atoe badala yake fidia kwa kuwalisha masikini katika kila siku anayokula. Iliendelea hivyo mpaka ilipoteremshwa aya iliyofuatilia, Mwenyezi Mungu aliposema:
شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ} البقرة:185}
"Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu naafunge."
[Al Baqarah - 185]
Anasema Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu);
"Baada ya kuteremka aya hii, ile hukmu ya kuhiyarishwa ikafutwa na badala yake ikawajibika kufunga kwa kila anayeweza kufunga isipokuwa kwa mgonjwa na mtu mwenye umri mkubwa sana."
Ama ile kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema;
"Na wale wasioweza, watoe fidia kwa kumlisha masikini", anasema Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu);
"Hukmu hii haikufutwa, bali ni kwa ajili ya mwanamume mtu mzima na mwanamke mtu mzima asiyeweza kufunga, wawalishe masikini kila siku badala ya Funga yao", kisha akasoma;
"Atakayekuwa katika mji katika huu mwezi (wa Ramadhani) afunge"
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.