SOMO LA FIQHI
Suali: Ni nini Maana ya Saumu kilugha na kisheria
Jawabu: Maana ya Saumu Katika Lugha
Ni kujizuia na kujiepusha kufanya jambo fulani.
Ama Saumu Kisheria
Ni kufanya ibada kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa kujizuia kula, kunywa na kufanya tendo la ndoa kuanzia kutokeza kwa alfajiri hadi kutwa kwa Jua.
FADHLA ZA SAUMU
Suali: Ni zipi Fadhla za saumu?
Jawabu: Saumu ina fadhila kubwa sana, na thawabu nyingi mno tena maradufu, na kwa hakika Mwenyezi Mungu ameinasibisha saumu kwake yeye kwa ajili ya kuipa utukufu na kuitukuza. Katika Hadithi Al-Qudsy iliyopokewa na swahaba Abu Hurayrah, Radhi za Allah ziwe juu yake Anasema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ:
كُلُّ عَمَلِ ابْنِ آدَمَ يُضَاعَفُ الْحَسَنَةُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا إِلَى سَبْعمِائَة ضِعْفٍ ، قَالَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ : إِلا الصَّوْمَ فَإِنَّهُ لِي وَأَنَا أَجْزِي بِهِ] رواه البخاري ومسلم]
[Kila tendo la mwanadamu huongezwa malipo ya wema wake mara kumi ya mfano wa jema hilo alilolitenda mpaka hufikia kuongezwa hadi nyogeza mara sabiini. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Isipokuwa saumu, kwani hiyo saumu ni yangu mimi, na mimi ndiye mwenye kutoa malipo yake; (mja wangu) anaacha matamanio yake na chakula chake kwa ajili yangu. Katika kufunga saumu kuna furaha mbili: furaha (ya kwanza) ni pale anapofungua saumu aliyefunga, na furaha (ya pili) ni wakati (aliyefunga) atakapokutana na Mola wake. Na harufu inayotoka kwenye kinywa cha aliyefunga ni nzuri sana mbele ya Mwenyezi Mungu kushinda harufu ya miski] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
HIKMA ZA KUFARADHIWA KUFUNGA
Suali: Ni zipi hikma za Kufaradhiwa sumu:
Jawabu: Hekima za kufaradhishwa kufunga ni nyingi Miongani mwa hizo ni hizi
1. Ni mja kupata ucha Mungu kwa kuitika amri ya Mola wake amri hii ya kufunga na kujitolea muhanga kuitekeleza sheria ya Mola wake. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ} البقرة:183}
[Enyi mlioamini! Mmelazimishwa kufunga (saumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu] [Al-Baqarah- Aya 183]
2. Kuipa nafsi mazoezi ya kusubiri, na kujipa nguvu ili kuweza kushinda matamanio.
3. Kujizoezesha mtu kufanya hisani, na kuwa na huruma kwa wanaohitaji masikini na mafukara; kwa sababu mtu anapoonja hisia ya njaa itampelekea mtu huyu kuwa na moyo laini na kuhisi jinsi wanavyohisi ndugu zake wahitaji wasio na chochote cha kula.
4. Kupata raha ya kiwiliwili na afya bora katika kufunga.
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.