KUPEWA UTUME NA KUSHUKA KWA WAHYI
Mtume ﷺ alipotimiza umri wa miaka arobaini, ambayo ni kilele cha ukamilifu na ndio miaka ya kupelekwa Mitume, alama za Utume zilianza kudhihiri na kumeremeta kwake kutoka upeo wa maisha.
Alama hizo ni pamoja na kuota kwake ndoto za ukweli, ikawa haoti ndoto yoyote isipokuwa hutokea, mfano wa mpasuko wa Al-fajiri kwa uwazi wake. Hali hiyo iliendelea kwa muda wa miezi sita. Muda wa Utume wake ulikuwa ni miaka ishirini na mitatu, kwa hiyo ndoto hizi zilikuwa ni sehemu moja katika sehemu arubaini na sita za Utume. Ilikuwa mwezi wa Ramadhani katika mwaka wa tatu tokea kujitenga kwake Mtume ﷺ alipokuwa katika pango la Jabal Hiraa, wakati Mwenyezi Mungu Mtukufu Alipoamua Kuimimina Rehema Yake kwa walimwengu, kwa hivyo akamkirimu mja wake Utume na kumteremsha kwake Jibril (a.s) na aya za Qur'ani.
Baadhi ya wataalamu walichunguza na kupitia vielelezo na dalili mbalimbali, waliweza kutambua kuwa siku hiyo ilikuwa ni siku ya Jumatatu, kwa siku ishirini na moja zilizopita katika mwezi wa Ramadhani, zinazoafikiana na tarehe 10/8/610 C.E. Wakati huo Mtume ﷺ alikuwa na umri wa miaka arubaini na miezi sita na siku 12 kwa mwenendo wa mwezi, na muda huo inasemwa ni kiasi cha miaka 39 miezi mitatu na siku ishirini na mbili kwa mwenendo wa jua.
*Arraheeq Al Makhtum 100-101
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.