DKT. JERALD F. DIRKS
“Kwa kutumia mafundisho na elimu ya seminari, nilielewa jinsi gani Biblia ilivyochafuliwa (nilijua wakati, mahali na sababu ya kubadilisha sehemu hizo), sikuwa ni mwenye kuamini tena imani yoyote ya utatu wa Mungu, na sikuwa na imani yoyote kuhusu uwana wa Mungu wa Yesu, amani iwe juu yake. Kwa kifupi, baada ya kupata imani ya kweli ya Mwenyezi Mungu, nimekuwa ni mwenye kuamini Mungu mmoja kama walivyo ndugu zangu Waislamu.”
Dkt. Jerald F. Dirks
Alizaliwa katika familia ya Kikristo, akalelewa katika familia hiyo akihudhuria kanisa na mafundisho yake kila jumapili wakati alivyokuwa mtoto. Alihitimu katika shule nzuri ya seminari na kuteuliwa kuwa mchungaji katika dhehebu kubwa la Kiprotestanti. Baada ya kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Harvard mwaka 1971, Dkt. Jerald aliingia kuendelea kusoma katika Kitengo cha Dini cha Harvard (Harvard Divinity School), na kuchukua shahada yake ya pili akisomea dini mpaka mwaka 1974. Hapo alikuwa tayari kashateuliwa kuwa kuwa mhubiri na mhudumu wa kanisa (United Methodist Church) mwaka 1972. Vile vile ni mwenye udokta wa kitaalamu katika Saikolojia, shahada aliyopata kutoka Chuo Kikuu cha Denver huko huko Marekani.
Kashachapisha zaidi ya makala 60 akongelea masuala ya Saikolojia ya tiba na zaidi ya makala mia na hamsini kuhusu farasi wa kiarabu (Arabian Horse, wanaosifika kwa kasi kubwa, umbo zuri na uwerevu). Ameshatembea sana Mashariki ya Kati na kukutana sana na jamii za kislamu huko Marekani.
Tunamshukuru kwa elimu yake ya kuhusu Ukristo aliyoitoa kutoka katika ghala yake ya maarifa. Elimu iliyosababisha akatoa kauli iliyowazi kueleweka:
“Kuna jambo lililo kinyume ambalo linawakumba wale wanaodhaniwa ni wenye akili, werevu na wajanja, hawa ni wale wanaotayarishwa kuja kuwa wahubiri wa kikristo wanaotolewa kutoka katika shule bora za kiseminari mathalani wale waliosoma shule ya Kikristo ya Harvard kwa kipindi kile. Jambo lenyewe ni kuwa, yule mseminari anaelekezwa ukweli wote wa kihistoria katika mambo fulani fulani mathalani kuhusu: 1) Uundwaji wa asili wa kanisa lenyewe na vipi likageuzwa kwa kuzingatia shughuli za kisiasa; 2) usomaji wa maandiko asili ya Kibiblia, ambayo mengi yao yako kinyume na yale wafuasi wengi wa Ukristo wanasoma pale wanapotumia Biblia zao za kisasa. Hata hivyo, hayo maandishi ya Biblia za kale, pole pole yanaanza kuwekwa katika toleo mapya ya Biblia; 3) kuzaliwa kwa fikra hizi za Utatu na uwana Mungu wa Yesu, amani iwe juu yake; 4) mafundisho yaliyo nje ya dini ambayo sheria au imani za kikristo zimeyakumbatia; 5) kuwapo kwa makanisa ya zamani na harakati za kikristo ambazo kamwe hazikukubaliana na utatu wa Mungu, na ambazo hazikukubaliana na uungu wa Yesu, amani iwe juu yake na 6) mengineyo (baadhi ya haya matunda ya elimu yangu ya seminari nimeyaweka kwa kirefu katika kitabu changu, The Cross and the Crescent: An Interfaith Dialogue between Christianity and Islam, (Alama ya Msalaba na Ile ya Mwezi: Kitabu Kinachozungumzia Mbadilishano wa Mawazo Baina ya Ukristo na Uislamu, Amana Publications, 2001). Kutokana na hivyo haitashangaza kuona wengi kati ya wahitimu wa seminari hizo wakiaga kuiepuka membari wanayotakiwa waipande kuhubiri yale wanayojua sio ya kweli, na kuamua kuingia katika taaluma nyenginezo (kama ushauri/mshauri wa kulipwa) jambo ambalo limenitokea hadi mimi, kwani nikaamua kwenda kuchukua shahada ya pili na ya tatu ya Saikolojia ya tiba. Niliendelea kujiita Mkristo kwa sababu kuna sehemu nilihitajika kujitambulisha na hata hivyo nilisomea uchungaji kanisani, japokuwa muda wote nilikuwa kazini kwangu kama daktari wa akili. Hata hivyo, elimu ile ya seminari imenifanya niwe makini kuingia imani yoyote itakayofundisha Utatu au uungu wa Yesu, amani iwe juu yake. Tafiti zinaonyesha aghalabu wachungaji kanisani huwa hawaamini haya mafundisho na ububusa mwengine kanisani kuliko wale wafuasi wao. Huwa wanaamini maneno kama “mwana wa Mungu” kisitiari tu, wakati wafuasi wao wanaelewa kiuhalisia kabisa.) ndio baadae nikawa Mkristo wa kusubiri Krismas na Pasaka tu, nikihudhuria kanisa kwa kunusanusa hapa na pale, nikijikaza kisabuni na muda mwengine kung’ata ulimi pale ninaposikia mahubiri ambayo nilikuwa najua si ya kweli.”
Pamoja na yote hayo, Dkt. Jerald alibaki kuwa mtu wa dini na bado aliendelea kijinasibisha na Ukristo. Anaandika:
“Nilijua zaidi Ukristo na sikuwa kama wale wanaokubali, bila kusaili, mafundisho na imani ya kanisa yaliyotungwa na binaadamu, ambayo kwa kiasi kikubwa yamepatikana kutokana na athari za kipagani, washirikina na masuala ya kisiasa ya zama za kale.”
Dkt. Jerald na mkewe wamekuwa kwa kiasi kikubwa wakijihusisha na utafiti wa historia wa farasi wa Kiarabu (Arabian horse). Ili wapate tafsiri ya nyaraka mbali mbali za Kiarabu, tafiti zao zikapelekea wakutane na Wamarekani wa kiarabu ambao walikuwa Waislamu. Dkt. Jerald alijifunza mengi katika tabia za Waislamu hao. Sanjari na hilo, Jerald alivutika sana na jamii za kiislamu ukilinganisha na zile za Kimarekani ambazo zilikuwa zimepotea kimaadili. Aligundua katika jamii zile za kiislamu, ndoa zilikuwa imara, wanandoa walikuwa wakijaliana, na uaminifu, uadilifu, kujitolea na tabia njema vilikuwa vinahamasishwa sana. Aliona kabisa Waislamu wakitumia tabia zao nzuri zenye nidhamu na maadili mazuri kote katika maeneo yao ya kazi na kule katika jamii yao.
Jambo lengine lilisababisha kubadili dini kwa Dkt. Jerald ni kule kutamani kwake kugundua vitu kwani alipendelea kusoma vitabu vya kiislamu. Mathalan, ndani ya mwezi, aliweza kusoma karibu vitabu sita au zaidi kuhusu Uislamu, kikiwemo kimoja kinachoongelea wasifu wa bwana Mtume Muhammad. Pia kashasoma aina tatu tofauti ya tafsiri za Qur’an kwa lugha ya Kiengereza. Jerald alisita kuingia katika Uislamu japokuwa alikuwa na mawazo yaliombatana na Uislamu. Kwa maneno yake mwenyewe tulielewa, yapi aliyoyakuta:
“Kitambulisho cha mtu ambacho ndani yake mtu huyo yumo, ni kiri yenye nguvu katika nafasi yake hapa ulimwenguni. Katika kazi zangu za kitaaluma, nimekuwa nikiitwa kutibu matatizo mbalimbali yanayotokana na kutawaliwa na uraibu (addiction), kuanzia uvutaji sigara, pombe mpaka madawa ya kulevya. Kama tabibu nilijua dawa bora kuepuka kitu ulichozoea ni kukiacha. Hiyo ilikuwa sehemu rahisi katika tiba. Kama alivyosema Mark Twain: “Kuacha sigara ni rahisi, nimeshafanya hivyo mara mia.” Lakini nilijua pia ufunguo mkubwa wa kusaidia kuendelea kujiepusha navyo ni kuishinda saikolojia ya mgonjwa, ambayo kwa kiasi kikubwa ipo katika utambulisho (kujulikana) kwa mgonjwa huyo, yaani mathalani mteja akiwa kashazoeleka kujulikana kuwa ni mvutaji sigara au mlevi. Ile tabia yake aliyoizoea ishakuwa kama kitambulisho kwake. Kubadili kitambulisho hiki ni jambo muhimu kwanza ili kuweza kupatiliza matibabu ya kisaikolojia. Hapa ndipo pagumu sasa. Kubadilisha jambo ulilozoeleka nalo ni vigumu sana kisaikolojia. Mgonjwa huwa mwepesi kurudi kwa yale ya zamani aliyoyazoea kuliko mapya na yasiozoeleka kirahisi kwake.
Katika kazi zangu za kitaaluma, nilikuwa nafahamu hayo niliyoyasema, na nilikuwa nikifanyia kazi kila siku. Cha kushangaza sikuwa tayari kulifanyia kazi suala hilo kwangu mwenyewe, nilishindwa kuitumia nadharia hiyo wakati nasita kubadilisha kitambulisho changu cha udini. Kwa miaka 43 sasa, kitambulisho changu katika dini kimekuwa kimebeba jina la Ukristo, hata kama nimeongeza baadhi ya taaluma zilizo tofauti kwa miaka kadhaa kati ya hiyo. Kuachilia kile kitambulisho haikuwa kazi rahisi. Kusita kwangu kulitaka niendelee kushikilia kitambulisho changu cha dini kilichozoeleka cha kuwa Mkristo ingawa ni Mkristo aliyeamini lile ambalo muislmu anaamini.
Ikafikia hadi mwishoni mwa mwezi Disemba, nikiwa na mke wangu tukijaza fomu za maombi ya pasipoti za Marekani, ili ile safari tuliyopanga kwenda Mashariki ya Kati iwe kweli, nilikumbana na swali moja lililokutaka ueleze msimamo wako wa kidini. Wala sikusita na sikufikiria kwani moja kwa moja nilikijaza kile cha mwanzo kilichozoeleka; “Mkristo.” Na bado nilijisikia sawa tu kwa kujaza vile.
Lakini, faraja ile iliharibiwa pale mke wangu aliponiuliza vipi nimejibu swali kuhusu dini katika fomu zile. Nilimjibu kuwa “Mkristo” huku nikicheka kwa sauti. Moja ya msaada wa msomi aitwae Freud katika kuelewa Saikolojia ya mwanadamu ni kugundua kucheka kwa sauti kama moja ya dalili ya kuondoa hofu na hangaiko mwilini mwako. Hata nadharia za Freud katika masuala ya kisaikolojia ziwe za uongo vipi! lakini katika suala hilo la kucheka kwangu halikuwa na shaka. Sasa basi kucheka nishacheka! Cha kujiuliza ni jambo gani lililokuwa likinisuta moyoni mwangu na nikahitaji kulitoa kwa kicheko kile?!
Kwa haraka nikamgeukia mke wangu na kukiri kwa kumtoa wasiwasi kuwa kweli nimeandika Mkristo na sio Muislamu. Yeye akanijibu kuwa alitaka kujua tu kama nimeandika Mkristo, Mprotestanti au Mmethodisti. Kitaaluma yangu, nilijua fika kuwa mtu huwa hajitetei kutoka katika shutuma ambayo haijafanywa bado. (kwa mfano wa kitaalamu, ikatokea mtu akaanza kujishtukia kwa kubwatuka, “Sijakasirika!” iwapo mtu anaeongea naye hata hajaongelea mada za kukasirika basi kisaikolojia, mtu huyo huwa anajilinda asije akashutumiwa, kiufupi mtu huyo amekasirika kweli na hakuwa tayari kukubali). Kama mke wangu hakunishutumu kuwa mie, “wewe ni Muislamu”, sasa kwanini nijishtukie na kumwambia yale. Nililigundua hili, lakini bado nilisita. Kile kitambulisho kilichogandana namimi kwa miaka 43 bado hakikuwa rahisi kukiepuka.”
Lakini ilipofika Machi 1993, alishindwa kutoingia Uislamu. Mkewe pia wa miaka 33 akawa Muislamu pamoja naye. Baadhi ya sababu zilizosababisha kusilimu kwake zinaweza kufupishwa kama ifuatavyo:
** Hii ilikuwa ni Dondoo (excerpt) ya kitabu cha Salim Boss kiitwacho“Wao Ima ni Waerevu Mno au Wajinga Mno” chenye kurasa 672 zote zimechapishwa kwa rangi (full colour). Ni tarjama ya kitabu kilichouzika sana kiitwacho “They are Either Extremely Smart or Extremely Ignorant” Kwa usomaji wa ziada tembelea www.extremelysmart.org au www.facebook.com/muerevumno “**
DKT. TIMOTHY J. WINTER
Ni mzaliwa wa Uingereza mwaka 1960. Amesoma katika shule yenye hadhi Westminster, London na baadae akaingia Chuo Kikuu cha Cambridge ambapo alihitimu kwa alama za daraja lajuu kabisa mwaka 1983. Alichukua shahada yake ya pili katika chuo hicho hicho cha Cambridge, na baadae kwenda kujiendeleza kielimu huko Chuo Kikuu cha Azhar; moja ya vyuo vikuu vya zamani zaidi duniani. Akaishi Cairo kwa miaka 3 akiusoma Uislam kutoka kwa walimu wa kawaida tu wa kimisri. Dkt. Timothy alikuwa ni msaidizi wa utafiti wa Chuo Kikuu cha Oxford. Akaenda kuishi Jeddah, Saudi Arabia kwa miaka mitatu ambapo alianzisha ofisi ishughulikayo na mambo ya kufasiri. Baada ya kusilimu, alibadili jina na kuwa Abdul-Hakim Murad. Lakini ni vitu gani basi unafikri vimempelekea mtu mwerevu kama huyu kusilimu?! Sababu zitatolewa katika aya zifuatazo.
Katika umri wake wa ukijana, Timothy alilivalia njuga swala la kujua ipi dini ya kweli. Alikuwa ametambua kuwa mapadri hawaiamini imani ya Utatu. Alikuwa anawajua baadhi ya watu ambao ni maarufu na wenye heshima zao ambao walikuwa wanaimani ya Mungu mmoja pia. Timothy alikuwa ni mtu mwenye furaha kwa kuwa Mkristo anayeamini Mungu mmoja pia, akihusianisha akili na imani yake na mshairi maarufu wa kiengereza, John Locke, Isaack Newton, Charles Dickens na wengine wengi. Kusoma kwake vizuri kwa Agano La Kale la Biblia kulimfanya afanye maamuzi ya kujikita katika imani ya Mungu mmoja na kuikacha ile ya utatu. Na bila shaka maneno “Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja.” [Kumbukumbu la Torati 6:4] yanaonekana kueleweka kabisa hata yakichorwa katika mwamba au yakiandikwa katika karatasi. Ule ukuaji wa imani ya Mungu mmoja (na uislam ukiwepo) kwa wasomi wengi wa dini huko Ulaya kukawa ni sababu nyengine ya yeye kubadilika hivi. Katika kipindi kilichorushwa na kituo cha ABC, John Cleary alikuwa akizihoji sababu za Timothy kuwa Muislamu. “Kipi kilichokupelekea mpaka ukatoka katika Ukristo? Lipi jipya unalolipata katika uislam?” Cleary aliuliza. “Uwezo wangu wa imani” Winter alijibu, akaendelea “Haujaniruhusu kuamini akida au mafundisho ya kidini (doctrines) zisoweza kushikika au kueleweka (abstract). Mimi hata katika huu umri wangu bado niko na ule ‘kutaka-kujua’ ya mtoto mdogo [ambaye hupenda kuuliza maswali na haridhiki mpaka apate majibu halisi]. Sikuweza kuchukua mruko wa kiimani (kuamini kiupofu bila ya hoja za maana) na kukubali imani hizi za Kikristo kama ile ya Utatu (Trinity) na ati Yesu alikufa kwa dhambi zetu (Atonement).”
Ile hamasa ya kutaka kuijua fasihi ya dini ilikuwa ni sababu nyengine kwa Timothy kuipata nuru ya Uislamu. Kwa kusoma vitabu, Timothy aligundua makosa ya Biblia ambayo wafuasi wa kawaida wa kanisa bado hawajajuzwa. Vitabu alivyopitia ni pamoja na The Myth of God Incarnate (Uwongo wa Mungu Kuvaa Umbo la Binaadamu) na Life of Muhammed (Maisha ya Muhammad) cha Maxime Rodinson. Timothy anakubali kuwa aliathirika sana na visa vya Mtume alivyovikuta katika kitabu cha Rodinson. Kanuni yake ya kupingapinga ilimfanya aonekane kama mtu mgeni na wa kushangaza lakini mwenyewe anafurahi kwamba haijaweza kupigwa na mawimbi ya mithiolojia (kanuni na mafundisho ya kubuniwa tu na wala yasio na ukweli) zinazopatikana katika dini ya Kikristo. Mathalan, hakuweza kuimeza kabisa ile imani ya kusamehewa dhambi, akiita imani hii ya dini ni ya usaliti (blackmail) pale aliposhangazwa na Mungu asiyeweza kusamehe watu moja kwa moja mpaka ajitie katika umbo la binaadamu wamdhalilishe, wamtese, wamuabishe, na wamuadabishe eti ili ndio awasamehe. Vitabu vingine vilivyoacha athari kwake ni vile vya mtunzi mashuhuri wa kiengereza Ruqaiyyah Maqsood. Katika kitabu chake The Mysteries of Jesus: a Muslim study of the origins and doctrines of the Christian church. (Miujiza ya Yesu: Tafiti ya Kiislamu Katika Uhalisia na Imani ya Kanisa la Kikristo). Katika kitabu hiko, Maqsood alimuweka wazi Mungu mwengine kabisa, mwenye upendo mwenye huruma kwa kusema: “Mungu haitaji kafara ili aweze kusamehe watu. Kitendo cha kubadilika haraka kutoka katika Ukristo kuingia katika Uislam ni uthibitisho tosha wa ukweli kama ule wa Mwana Mpotevu (the Prodigal Son).”
Jambo jengine zito lililomvuta Timothy kuingia katika Uislam ni kuisoma Qur’an. Mazoezi ya kulinganisha na kutofautisha, Qur’an na Biblia yalimfanya Timothy kukiri haya: “Sehemu nyingi za Biblia zimejazwa na hadithi (visa) ambazo malengo yake bado ni tata au hata hamna kwa wakati mwengine; zilizomulikwa kwa mwanga wa kumwekuamwekua tu lakini Qur’an ilinipa mwanga kamili.” Katika mahojiano kwenye Sunday Nights na John Cleary katika kulijadili lililomuathiri katika uislam Timothy akaelezea athari ya Qur’an:
“Hata uislam una sauti zake nzuri pia, na ufunguo wa tuni za kiislamu si lengine bali ni huu usomaji mzuri wa Qur’an. Nilikuwa natembea mitaani asubuhi na mapema kipindi naishi Cairo. Nilishuhudia wenye maduka wakifungua maduka yao, na nilihesabu wauzaji maduka wapatao 38 ambao walikuwa wakisikiliza Qur’an masaa 24 kwa siku. Kwa hakika hiyo ndio sauti niipendayo zaidi, na ilikuwa moja ya sumaku zilizonivuta mimi kuuelekea uislam. Ni sanaa kubwa ya kiislamu, ambayo bado inanitetemesha kuliko sauti yoyote duniani.”
Sanjari na hilo, Timothy alivutiwa na kile alichokiita ‘msimamo wa ajabu wa uislam’. Hivyo ni sawa na kusema sheria na matendo ya ibada ya Kiislamu yanastaajabisha kwa kutobadilika kwake. Kuhusu hilo alisema:
“Msikitini, mtu hashikwi na tamaa wa kusema maneno yasiyo na maana, au ayatakayo, bali ni yale tuliyorithi kutoka zama za zamani za imani, maneno ambayo mtu atajishusha nayo pale anapohitaji kuongea na Mungu. Hakuna dini nyengine inayofanya kama mwanzilishi wao [yaani Mtume Muhammad] alivyofanya; na hakuna dini nyengine ambayo maneno yake ya ibada yako sawa dunia nzima na zama zote.”
Katika upande mwengine, amgundua katika ukristo, kuna sheria ambazo zimetungwa upya na watu wasio stahili jukumu hilo, wakisababisha mgawanyiko na chuki na aghalabu wakiaacha mkusanyiko ukiwa hautendi ipasavyo wanalotaka kufanya.” Upya huo wa sheria na ibada ndio unaoharibu ukweli wa dini. Ukiachana na yote, kubwa kabisa lililosababisha yeye kuwa Muislamu ni maombi yake kwa Mola mmoja na pekee. Timothy aliamini kuwa Mungu alikuwa akijibu dua zake.
Katika mahojiano naye, John Cleary aliuliza swali lamsingi sana kuhusu maisha ya Timothy katika Uislamu: “Ni kipi kwako kinachokuashiria mwanga sahihi wa Uislamu, kile kinachoangaza njia ambayo maisha yako yanapaswa kuyafata?” Na jibu lilifupisha ule uzuri wa Uislamu kama alivyosema mwenyewe Timothy Winter:
“Mwenyezi Mungu mmoja,na ukweli ni mmoja, usiochanganywa, usiofanywa mgumu na usiobadilika…mtiririko mzuri wa njia za kuabudu ambao mtu anatumia kuufikia ukweli huo muhimu. Moja ya utajiri wa Uislamu kwangu mie ni hizi liturujia na vitendo za ibada na hata pia vile watu wanafunga Saum na kutoa Zakkah; yote haya yako sawa ulimwenguni kote na hayajabadilishwa hata kidogo. Hakuna waliyotokea wakasema njooni tubadilishe kidogo mfumo wa swala zetu. Labda tulete magitaa na imamu wa kisasa avalie mabuti na jinzi akijaribu kuimba hapo mbele. Naenda msikitini na najua kitu nachoenda kupata kikiwa hakibadiliki, kizuri, kikiwa kishakamilika tangu zama hizo. Jambo kubwa sana kwangu kuona ibada zetu hazibadiliki na bila shaka hazitabadilka. Na la tatu ni huku kufata mila ya Ibrahim. Silihisi jambo hili eti kwa kuwa mimi ni Muingereza au labda ni mtu fulani, najua ni tofauti lakini moyoni nahisi ni sehemu kutoka katika maandiko ya Kiyahudi na Kikristo, jamii za kiimani za Mashariki ya Kati pia. Bado nampenda Yesu, Ibrahim, Musa, Yaqub, Ismail na Is’haq kwani wote wameheshimiwa katika Qur’an, walikuwa watu wakubwa utotoni mwangu na bado nawaheshimu hadi leo. Hivyo sihisi kuwatenga hata kidogo.”
Kwa sasa ni mhadhiri wa chuo kikuu akifundisha masomo ya dini ya kiislamu katika kitivo cha masuala ya dini, Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza. Na pia ni mkurugenzi wa masomo ya Teolojia katika Chuo cha Wolfson. Pamoja na kuwa imam wa msikiti wa Cambridge, Sheikh Murad pia ni katibu wa mfuko wa Waislamu; Muslim Academic Trust (London) na pia ni mkurugenzi wa Sunnah Project katika kituo cha masomo yahusuyo mashariki ya kati hapo Chuo Kikuu cha Cambridge, ambacho kinatoa matoleo ya mwanzo kabisa ya mkusanyiko wa Hadithi kwa Kiarabu.
Winter amekuwa akitokea katika idhaa ya BBC na amekuwa mwandishi mkubwa katika magazeti mbalimbali kama The Independent; Q-News International, jarida la Waislamu la Waingereza (Britain’s premier Muslim Magazine); na Seasons jarida la kitaaluma la Taasisi ya Zaytuna. Timothy alinukuliwa akisema:
“…Pamoja na asili yake ya karne ya 7 ya Uarabuni, Uislamu unakubalika mazingira yote, na hii ni dalili ya asili njema na ya kimaajabu ya dini hii…tukiuzoea Uislamu na kutulia nao vizuri, utaona ndio imani pekee inayostahili watu wa Uingereza. Mila zake ndio bora kwetu. Mtindo wake wa huruma ya wastani, maji yaliyotulia yana kina kirefu; msisitizo wake katika staha na msisitizo wake katika maarifa ya kawaida na katika nadharia ya vitendo, na usisitizo wake wa kutumia akili, vinaungana kutupatia dini bora na asili zaidi kwa ajili ya watu wetu…Uislamu ndio dini yenye udugu wa kweli wa waumini katika Mungu mmoja wa kweli, muunganiko wa kweli kwa wale wanaopenda kubaki na malengo mazuri ya kufata ubinaadamu katika hizi zama za kijinga na kusikistisha. Uislamu ni mkarimu na unajumuisha wote.” **
** Hii ilikuwa ni Dondoo (excerpt) ya kitabu cha Salim Boss kiitwacho“Wao Ima ni Waerevu Mno au Wajinga Mno” chenye kurasa 672 zote zimechapishwa kwa rangi (full colour). Ni tarjama ya kitabu kilichouzika sana kiitwacho “They are Either Extremely Smart or Extremely Ignorant” Kwa usomaji wa ziada tembelea www.extremelysmart.org au www.facebook.com/muerevumno “**
Sarah Joseph
Huyu anatokea katika familia ya Kikatoki ya Uingereza ambayo mizizi yake inatokana na uvamizi wa Norman (Norman Conquest). Mama yake alianzishaa uwakala wa kwanza wa mitindo Uingereza na Joseph anadai kuzunguukwa na watu wazuri zaidi hapo katika ofisi za mitindo mtaani kwao.
Mtoto huyu Mkatoliki babake akiwa mhasibu na mamake aliyekuwa mwanamitindo anakumbuka alivyokuwa na umri wa miaka 14 akimkimbilia Naomi Campbell akiwa na kadi ya biashara ya mama yake. Na katika kipindi kifupi baadae, kaka yake akawa Muislamu. Akijilazimisha kupingana na chuki zake kwa Waislamu, Sarah akaanza kusoma dini. “Taratibu, Uislamu uliendelea kunijibu maswali yangu ambayo yalinitatiza mpaka pale nilipoutaka Uislamu wenyewe,” anasema. Na alivyotimu miaka 17, Sarah alibadili dini kuwa muislam, akiukana Ukatoliki aliolelewa nao. Akaamua kuwa mvaaji hijab, vazi lililompa ukombozi na taadhima. “Nataka nihukumiwe kwa kile ninachosema, na sio kwa vile ninavyoonekana,” alishawahi kusema hivi.
Katika mahojiano na Gabrielle Procter, Sarah Joseph alisema:
“…Kuwa Muislamu kunakupa haiba nzuri lakini kubwa zaidi sasa ni binaadamu kikwelikweli. Nimeishi miaka 16 nikiwa sio muislam, sasa hivi mimi kama mwanadamu, mwanamke, mama, mhariri, na mwenyeji wa London- vyote hivi vinanisaidia. Lakini jukumu langu kama mama linanyooshwa na kuwa Muislamu; kazi yangu kama mhariri, na ufahamu wangu kama mmoja wa wanajamii vyote vinanyooshwa na falsafa yangu hii mpya… mimi ni mtu wa imani na naamini mtu wa imani yapasa awe na matumaini. Nawaona vijana wengi wanaojumuika katika jamii mbali mbali za kiengereza wakiwa waerevu, fasaha, wenye msukumo wa kuleta tija katika jamii yao na wakiwa sehemu ya jamii ya kiislamu. Nadhani Waislamu wana uwezo wa kuchangia pakubwa katika jamii. Na kama watu ikatokea wauone uislam ni sehemu ya utatuzi badala ya kuuona ni sehemu ya tatizo, wataishi kwa raha mustarehe.”
Sarah amepata shahada yake ya kwanza katika masomo ya dini kutoka Chuo Cha King cha London. Alifanya utafiti kuhusu Waingereza Wanaosilimu akisomea shahada yake ya pili. Pamoja na hilo, amekuwa mshindi wa 1999-2000 wa shani ya kusomeshwa bure kutoka katika mfuko wa King Faisal Foundation/ Prince of Wales Chevening. Ni mhariri wa jarida la Emel (jarida la kiislamu linalosomwa zaidi Uingereza- jina lake linasomeka M na L likisimama badala ya Muslim Life (Maisha ya Muislam), likimaanisha ‘tumaini’ kwa lugha ya Kiarabu). Pia ni mtangazaji wa British Muslims, na ni mwandishi. Sasa, akisomea shahada nyengine amekuwa akifanya kazi kwa muda kama mwalimu wa chuo ambaye amekuwa akifanya mihadhara mingi na sehemu nyingi inayohusiana na masuala ya dini na wanawake. Mwaka 2004, alitunukiwa OBE (Tuzo ya Uingereza inayosimama badala ya Order of the British Empire), kwa mchango wake katika midahalo ya dini. Sarah kashajumuika katika vipindi vingi vya televisheni za Uingereza vikiwemo –Panorama na Johnathan Dimbleby. Pamoja na kufanya kazi kama mtafiti mzoefu katika kitengo cha kujifunza cha BBC 2001 Islam Series.
Pia amekuwa mhariri mkuu wa kwanza mwanamke wa gazeti kubwa la Waislamu: Trends. Sara Joseph ni mhariri muanzilishi wa baraza la Waislamu la Uingereza The Common Good Consultant on Islamic Affairs– likishughulika na utafiti na mafunzo kwa wale wanaoihitaji kuajiriwa, kusoma, kuwa na afya bora, polisi n.k. katika misingi ya Kiislamu.
Ameolewa na Mahmud ar-Rashid, mwanaharakati wa haki za binadam. Miongoni mwa vyama vya vijana na jamii ambavyo ar-Rashid anaongoza ni: the Muslim Council of Britain (MCB), baraza kuu la kutetea Waislamu Uingereza na ni pia mwenyekiti Islamic Society of Britain. Wana watoto watatu tayari: Hasan, Sumayyah na Amirah.
Akiongelea kuhusu makundi ya watu wanaoingia katika Uislamu kila kukicha, hususan kwa kutumia makadirio ya watu 10,000 mpaka 50,000 wanaoingia katika Uislamu kila mwaka Uingereza, Sarah anadhani kufikia mwaka 2020, Uislamu itakuwa ndio dini inayofatwa zaidi Uingereza, “Sisi ni wa pili kwa kuwa na idadi ya wafuasi wengi Uingereza ila ifikapo 2020 tutakuwa tunaongoza rasmi kwa kuwa na waumini wengi wahudhuriaji ibada zao kama ukitumia uhudhuriaji wa kanisa na msikiti kama kigezo,” Alisema hayo kuiambia GDN.**
** Hii ilikuwa ni Dondoo (excerpt) ya kitabu cha Salim Boss kiitwacho“Wao Ima ni Waerevu Mno au Wajinga Mno” chenye kurasa 672 zote zimechapishwa kwa rangi (full colour). Ni tarjama ya kitabu kilichouzika sana kiitwacho “They are Either Extremely Smart or Extremely Ignorant” Kwa usomaji wa ziada tembelea www.extremelysmart.org au www.facebook.com/muerevumno “**
MUSA CERANTONIA
Alizaliwa na kukulia Melbourne, Australia. Anatoka katika familia ya watoto 6. Alisilimu 2002 mwezi wa Ramadhani akiwa na miaka 17. Amesomea Historia na Mawasiliano (History and Communication) chuoni na baadae akajiendeleza kwa kusomea Historia ya Kiislamu. Amekuwa Rais ( Mwenyekiti ) wa Jumuiya ya Waislam wa Chuo Kikuu cha Victoria, hukohuko Melbourne. Ni baba wa watoto wawili, Aisha na Swafiyah. Musa ana asili ya Italia kwa baba, na mama mwenye asili ya Ireland. Italia likiwa taifa kiongozi kwa kufuata ukatoliki, kama ilivyotarajiwa, hata Musa Cerantonio naye alilelewa Kikatoliki. Alikuwa akiamini bila shaka kuwa kama Ukristo ndiyo dini yenye wafuasi wengi, na ukatoliki ambao yeye yumo ndani ndiyo kundi kubwa la Ukristo, bila shaka hiyo ndiyo dini ya kweli.
Sasa vipi alisilimu? Kama alivyojibu katika mahojiano, “ilikuwa safari ndefu iliyonichukua miaka miwili ya kusoma na kufuatilia Uislamu.” Na sasa twende tupite njia alizopitia yeye. Musa alisoma shule ya Msingi ya kikatoliki na kuingia shule ya sekondari ya kijamaa. Rafiki zake ambao wengine walikuwa waislam, walikuwa watumizi wa madawa ya kulevya na mengineyo ya kihuni, ila yeye alijilinda. Shule ya sekondari aliyoenda ilikuwa imejengwa kwa itikadi ya Kijamaa na hata katika midahalo ya shule, Musa alikuwa ‘akiwaka’ dhidi ya itikadi hizo za Kijamaa. Musa alipinga vikali mawazo ya kina Karl Marx aliyesema “dini ni kasumba tu ya watu” au “Mungu amekufa” ya Friedrich Nietzche. Ili Cerantonio aitetee dini yake, ilimpasa aisome na punde akaanza kusoma Biblia, alishtushwa na aliyoyakuta. “Baadhi ya visa vya Biblia ni vya kiasherati, ni vya kiponografia (matusi yenye kutia ashiki),”alisema, na kama mfano, Musa alitoa kisa cha Lut aliyeleweshwa na watoto zake wa kike. Sijui nimalizie!? Dah! Wacha niseme tu! Watoto wale wakafanya mapenzi na baba yao kwa masiku mawili ili kulinda nasaba ya baba yao (Mwanzo 19:30 – 36). Alishangaa inakuwaje visa kama hivyo viitwe Neno la Mungu? Hii ndiyo sababu ya Dkt. Lawrence Brown, mchungaji, hakuamini ile kauli inayosema ati “Maandiko yote Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa katika kufundisha ukweli, kuonya, kusahihisha makosa, na kuwaongoza watu waishi maisha adili” [2 Timotheo 3:16, Biblia-Habari Njema (Good News)] ya visa hivyo. Katika kitabu chake, MisGoded, Dkt. Brown aliandika kuwa, katika Biblia:
“….Kuna hadithi za walevi walio uchi, kujamiiana kwa maharimu (au ndugu) na umalaya ambao hamna mwenye haya anayeweza kumsomea mama yake, au kwa watoto wake. Na bado, moja ya tano ya kundi la watu duniani linakiamini kitabu kinachosema Nuhu “akanywa divai, akalewa; akawa uchi katika hema yake.”( Mwanzo 9:22 ) na kile cha,
“Lutu akapanda kutoka Soari akakaa mlimani, na binti zake wawili pamoja naye, kwa sababu aliogopa kukaa katika Soari. Akakaa katika pango, yeye na binti zake wawili. Yule mkubwa akamwambia mdogo, Baba yetu ni mzee, wala hakuna mtu mume katika nchi atuingilie kama ilivyo desturi ya dunia yote. Haya, na tumnyweshe baba yetu mvinyo, tukalale naye, ili tumhifadhie baba yetu uzao. Wakamnywesha baba yao mvinyo usiku ule, akaondoka huyo mkubwa akalala naye, wala yeye hana habari alipolala wala alipoondoka. Ikawa siku ya pili, mkubwa akamwambia mdogo, Tazama, nimelala jana na baba yangu, tumnyweshe mvinyo tena usiku huu, ukaingie ukalale naye. Wakamnywesha tena baba yao mvinyo usiku ule, akaondoka mdogo akalala naye, wala yeye hana habari alipolala wala alipoondoka. Basi hao binti wote wawili wa Lutu wakapata mimba kwa baba yao.” [Mwanzo 19:30-36]
Kwa maelezo kamili na ushahidi kuhusu hadithi zenye uasherati na kupotoka kama ukahaba na zinaa angalia (Mwanzo 38:15 – 26), kuhusu ukahaba (Kitabu cha Waamuzi 16:1), mkengeuko (2 Samweli 16:20 – 23), umalaya (Ezekiel 16:20 – 34 na 23:1 – 21), uzinzi (Methali 7:10 – 19), ubakaji baina ya ndugu kama ule aliofanyiwa Tamari katika 2 Samweli 13:7 – 14 inaonesha maadili ya ajabu, na Tamari (aliyebakwa) alishauriwa kwa kuambiwa, “sasa tulia, dada,” kwani, “[Huyo mbakaji, Absalomu] ni nduguyo; usilitie moyoni jambo hili.” (2 Samweli 13:20). Mh! Mbakaji akiwa kaka yako hakuna tatizo!!? Je ni kweli tuendelee kuamini “Hekima” hizi ni matendo ya uteremsho kutoka kwa Mungu?, au ndoto chafu tu?[1]
Mshituko mkubwa kwa Musa ulikuja pale alipogundua kuwa sheria za Biblia hazifuatwi na Wakristo. Mathalan, aligundua kutoka katika Biblia kuwa wanaume wanapaswa kufuga ndevu lakini Papa na Wakristo wengi wananyoa. Biblia inaelekeza watu waepuke mvinyo lakini kanisani Jumapili, mchungaji anawapa wanywe; Biblia inakataza kula nyama ya nguruwe lakini wengi wa Wakristo wanaifanya nyama ya mnyama mchafu huyo na mwenye magonjwa mengi kuwa chakula chao kipenzi. Musa akaamua kufuata amri za Biblia, akaanza kufuga ndevu na kuacha pombe na nguruwe. Familia ilipomuuliza akajibu, “Biblia ndivyo inasema.” Wakawa wanamuwakia kumwambia, “hilo ni Agano La Kale.” Na yeye akashangaa inakuwaje wakataze maneno ya Mungu na kufuata baadhi! Musa Cerantonio akaamua kuwapa changamoto kwa kuwauliza, “Mnakubali ndoa za Jinsia moja?.” Bila shaka jibu ni “hapana” ndipo Musa akawambia kuwa kupigwa marufuku kwa ndoa hizo zatokana na Agano La Kale. Akaona huu ni unafiki kufuata baadhi ya sheria na kuacha nyengine. Musa hakuwa na furaha kwa kitendo kile cha kuchagua ya kufuata na mengineyo ya kuyaacha, ndiyo sababu wakati mwingine alichukulia Ukristo kama mgahawa, ambapo unaenda unaagiza chakula ukitakacho na kwa vile usivyotaka vinakuwa havikuhusu. Katika mahojiano yake na Saudi Gazette, aliombwa ahadithie alivyopita katika njia mpaka akaufikia Uislamu, Musa alijibu kwa kusema:
“ Nilikuwa nikisoma Biblia na nikagundua nguruwe ni haramu, lakini Wakristo cha kushangaza wanakula. Nikashangaa kuona Wakristo wasivyoifuata Biblia. Nikajiona nasogea karibu na uislam na hapo nikaamua kusoma. Niligundua kumbe hadi Waislamu wanamuamini Yesu (Amani iwe juu yake). Nikajiambia, inaonekana Uislamu ni mzuri ngoja niusome zaidi.”
Kwa hamu yake ya kuujua ukweli, Musa alitembelea Vatican mwaka 2000. Jiji la Vatican ni dola huru iliyo ndani ya jiji la Rome, Italia. Ulikuwa ni mwaka wa Jubilii (Sikukuu ya Ukumbusho) ambayo kwa ukatoliki ulikuwa ni mwaka maalumu wa kutolewa dhambi na kuomba msamaha. Aliambiwa, mtu akiingia kupitia “ mlango mtakatifu” (unaojulikana kama Porta Santa kwa lugha ya Italia), madhambi yake yote yanapukutika. Musa hakulimezea hilo bali aliuliza, “Jambo hili limezungumzwa wapi katika Biblia!?” na hakupata majibu ya kumridhisha. Na alipoamua kuingia kupitia mlango ule, alishituka kuona mwili uliokaushwa wa mapapa wa zamani na chakushangaza zaidi, watu walikuwa wakiuabudu. Aliona pia watu wakifuta miguu ya sanamu na kuomba waliyoyataka. Akaingia hadi chumba cha Papa (Capella Sistina) na akaona kwenye dari kuna michoro mbalimbali ikiwemo picha ya Mungu mwenyewe (alieonekana kama kikongwe na mwenye ndevu zenye mvi) na Adam! Hakuweza kushabihisha alichoona na amri ya pili ya Biblia: “Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.” [Kutoka 20:4]. Musa Cerantonio alipinga yote hayo na akaanza kujiita Mkristo asiye na dhehebu lolote, mtu fulani anaye amini Mwenyezi Mungu na asifate kanisa lolote. Na ilikuwa ni katika kipindi hiki ndipo alipoanza kusoma dini nyingine kama Uhindi, Ubudha, Shinto, lakini kamwe hakufikiria Uislam.
Baada ya kipindi fulani, alijitokeza Muislamu aliyemwambia, “Naona faraja kukutana na wewe, jina langu ni fulani, je ungependa kuwa muislam?” Hili lilifungua milango kwa yeye kujifunza uislam kwani kwa chochote Musa alichotaka kujua katika uislam alimuuliza mtu huyo. Muislam huyu alimpatia Musa Qur’ani, lakini Musa hakuisoma. Musa aliipokea tu Qur’ani na akaihifadhi pahala, kaka yake alipoigundua kuwa ni Qur’ani, aliichukua na kuichoma. Kuna wakati alikutana na marafiki zake Waislamu, miongoni mwa hao waislam, mmoja wao alikuwa haujui uislam vizuri. Katika maongezi yao na Musa, alikuwa akimtusi Yesu bila ya kujuwa kuwa alikuwa mmoja wa Mitume wakubwa wa Allah. Hili lilimjaza wahaka Cerantonio na akaamua kidhati kuusoma uislam ili kuishambulia imani hiyo ya waislam. Katika kusoma kwake, cha kwanza alichogundua kilikuwa ni waislam wanamuamini Yesu Kristo. Lingine aligundua kuwa Waislam wanaamini Mungu Mmoja na hawamshirikishi. Kila alivyousoma zaidi, ndivyo alivyotaka kuujua zaidi. Kwa vile alivyokuwa ameusoma Uislamu kiundani na kuuelewa, ilifika kipindi hadi baadhi ya rafiki zake Waislam walikuwa wakimfuata na kumuuliza maswali mbalimbali ya kiislamu (wakitaka wapewe Fatwah kuhusu hayo maswala yao). Kipindi muhimu kilicholeta athari kubwa ni pale rafiki yake mmoja alipompa DVD ya Abdul-Rahim Green (Mzungu aliesilimu vilevile), inaonesha jinsi alivyosilimu. Baada ya kuangalia video ile, Musa akajitangazia kuwa yeye si Mkristo tena, sio Mkristo na sio Muislam. Ila alianza kufuata matendo ya kiislam kama kuswali kwa kusujudu. Alikuwa bado hajasilimu, na mwezi wa Ramadhani ulipowasili, aliwauliza rafiki zake waislam kama watafunga, alishangazwa kusikia kuwa baadhi yao hawatafunga. Ila yeye alisema, “ Mimi siyo muislam, ila nitafunga mwezi mzima.” Na ukweli ukawa kama alivyo ahidi, kwani mwezi mtukufu ulipowasili, alifunga na kufuturu nyumbani kwa rafiki zake. Alichopendelea zaidi ni “misosi” (vyakula) vilivyopikwa na kupikika vya Waislamu. Hapo nyumbani kwa rafiki yake, alikiona kitabu kimoja kiitwacho “A Brief Illustrated Guide To Understanding Islam” (Mwongozo Mfupi Wa Kuuelewa Uislamu) kilicho haririwa na I.A Ibrahim kilichoongelea miujiza ya Qur’an Tukufu. Musa hakujizuia kukisoma kitabu kile. Na alipomaliza tu , alitamka shahada, “Ash-hadu anlaa ilaaha ila LLah, wa Ash-hadu anna Muhammadan Rasuulullah”, ikimaanisha kuwa, “ Nashuhudia (nakiri) hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah, na Muhammad ni Mtume Wake.”
Musa Cerantonio amesafiri sehemu nyingi za dunia. Na mwaka 2005, alitembelea mji mtukufu wa Madinah. Alikwenda kuishi Misri, na akafanya kazi katika chaneli ya televisheni ya kiislamu inayotumia lugha ya Kiingereza. Katika mahojiano fulani, Yosra Mmarekani aliyesilimu, alimuomba Musa, “………elezea jambo moja lililokuvutia hapa Misri hata ukadiriki kutosita kutamka neno ‘SubhaanAllah’ na Cerantonio alijibu,
“Nakumbuka siku niliyowasili nyumbani kwangu, nilimuuliza mlinzi wapi kuna msikiti uliokaribu na hapa. Aliniambia kuwa, kama nikienda kushoto ipo miwili, nikienda kulia upo mwingine, nikienda moja kwa moja, nitakutana na miwili, pembeni ya gorofa ninalokaa kuna masjid nyengine. Na yote ilikuwa haikuchukui zaidi ya dakika 1. Nimetoka sehemu yenye msikiti mmoja katika eneo zima, nimekuja sehemu nayochagua msikiti upi niswali katika minane iliyopo karibu!”
Mara ya kwanza kwenda kuhiji ni 2006, na mara ya pili ni 2011. “Sina maneno kuelezea hilo,” Musa alijibu kuhusu alivyojisikia alivyokuwa akihiji, “kwa ujumla ilikuwa faraja. Haikuwa kama nilivyotarajia. Nimejifunza kuhusu umoja wa umma wa Kiislam. Hija pia inakufundisha kuwa mvumilivu. Nimerudi nikiwa mtu mwengine hata familia yangu na marafiki waliligundua hilo.” Katika mahojiano yaliyochapishwa na The Saudi Gazette, Musa aliulizwa ushauri wake kwa vijana wa Kiislamu, ambapo alisema,
“ Unaona jinsi Magharibi inavyokuwa ya Waislamu; wanamuziki, matajiri na watu wengine mashuhuri wote wanaingia katika Uislamu. Vijana wa kiislamu inapaswa wajiulize inakuwaje watu hawa walioyashinda maisha wawe na pupa hivi kuingia katika Uislamu. Ni kwa sababu ni dini ya haki na wanataka pepo pia. Tambeni kwa kuwa Waislamu.”
Akiongozwa na shauku ya kutaka radhi na thawabu za Allah kwa kuwaita watu katika uislam, Musa Cerantonio amejumuika katika majukwaa tofauti kutangaza Uislamu. Ni mara mbili kashawahi kuhudhuria Kongamano kubwa la Amani la Kiislamu (Islamic Peace Conference) lililofanyika Mumbai mwaka 2007 na 2009, vile vile ameweza kuhudhuria Kongamano kama hilo la Dubai (Dubai Peace Conference) la mwaka 2010. Amefanya mihadhara kuhusu Uislamu katika hafla mbalimbali sehemu nyingi kama Australia, India, UAE, Ufilipino, Kuwait na Qatar. Amefanya kazi Iqraa International, chaneli ya televisheni irushwayo katika satelaiti.katika moja ya vipindi vyake vinavyorushwa na Iqraa International, Musa alimuhoji Lauren Booth, shemeji wa aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza, Tony Blair. Lauren Booth ambaye naye ni mtangazaji, aliingia katika dini hii ya Kiislamu katikati ya mwezi Septemba 2010 na alipania kwenda kuhiji mwaka 2011. Katika mahujiano hayo yaliyofanyika Madinah Al-Munawwarah, Cerantonio alitaka kujua jinsi alivyosilimu na aliuliza pia anavyojisikia akiwa na dini mpya. Kama unatatizwa na swali lolote ambalo unahitaji jibu lake, basi usisite kumuuliza Cerantonio kwani yuko tayari kulijibu papo kwa papo kupitia kipindi chake “Ask the Sheikh” (Muulize Sheikh) kinachorushwa na Iqraa International.
Musa pia ametokea katika chaneli ya muda wote ya bure, Peace TV. Katika moja ya kipindi chake, Musa alitoa “Ushari kwa Waislamu Kutoka kwa Waliosilimu” na anakiri baadhi ya waislamu ndio sababu ya kuzuia watu wasiingie katika Uislamu. Kwa mfano Musa anahadithia kuwa kabla hajasilimu, rafiki yake Muislamu alimsihi Musa asisilimu. Kisa na maana ni kuwa, endapo Musa atasilimu, wazazi wake watakereka na kukasirika, wakitaka kujua, “Nani aliyemsababisha mpaka mtoto wetu akasilimu, nani aliyemvuta katika Uislamu, nani aliyesababisha mwenetu atengane na familia yake na mila zake…” Musa akasema, Waislamu wanawazuia wasio Waislamu kuingia katika dini yao. Na hili linasababishwa na matendo yao. “Kumbuka tabia yako ndio Daawah yako” kwa hivyo Waislamu inabidi watumie tabia zao njema kutangaza dini. “Wengi wa Waislamu niliokutana nao,” Alikiri, “walikuwa na tabia mbaya, wanakuibia, wanaongopa, walikuwa wanafanya kila kitu ambacho Muislamu hatakiwi kukifanya.” Cerantonio aliwaonya watu wasiwe na tabia ya kulaumu gari katika ajali bali walaumu dereva . “Kwa bahati nikaelewa labda haya ni yale wanayofanya Waislamu lakini kuna lile ambalo Uislamu unalifundisha wacha nilisome hilo.” Musa anaona tabia ya mtu ni njia bora ya kuusambaza Uislamu hivyo anawausia Waislamu wajipambe na tabia hizo njema. Anasema unaweza kufanya jitihada ya kumgaia asiye Muislamu kitabu lakini asikisome, unaweza kumpa CD ya mawaaidha na bado asiisikilize, pia unaweza mkabidhi DVD ya kiislamu na bado asiangalie, sasa ufanyeje ukifikiwa na ugumu huu? Basi jitahidi uwezavyo kutoa Daa’wah kupitia tabia zako. Ushauri huu wa Cerantonio unawafikiana na ule wa mwanazuoni wa kiislamu aliyewaambia wanafunzi wake, “Waiteni watu katika Uislamu huku mkiwa kimya.” Wanafunzi walishtuka, wasijue ni kwa vipi wanaweza waita watu katika Uislamu bila kunyanyua ndimi zao, naye akawajibu, “Kwa kutumia tabia zenu.”
Cerantonio anaelekeza kuwa, jirani yako, rafiki yako ni Muislamu mtarajiwa kwa hivyo usidharau juhudi zao za kuwabadili watu. Yeye mwenyewe alivutika na Uislamu pia kwa kujua Yesu anameremeta kwa Waislamu. Alishasema, ikiwa utamueleza anayejiita mfuasi wa Kristo kuwa sisi waislmu tunampenda Yesu kuliko yeye basi anaweza kuvutika kujifunza Uislamu. Katika kipindi kimoja cha Peace TV: “My Choice”, Musa alifunga kipindi hicho kwa dua ifuatayo: “Namuomba Allah atufanye tuwe waumini wa kweli wa Tauhiid (kumfanya Mola kuwa mmoja kikweli kweli), tuwe miongoni mwa wale wasiomshirikisha na lolote, na tusimsifu yeye Mungu kwa sifa ambayo hajajisifu nayo Yeye Mwenyewe.” *
** Hii ilikuwa ni Dondoo (excerpt) ya kitabu cha Salim Boss kiitwacho“Wao Ima ni Waerevu Mno au Wajinga Mno” chenye kurasa 672 zote zimechapishwa kwa rangi (full colour). Ni tarjama ya kitabu kilichouzika sana kiitwacho “They are Either Extremely Smart or Extremely Ignorant” Kwa usomaji wa ziada tembelea www.extremelysmart.org au www.facebook.com/muerevumno “**
Michael Wolfe
Pamoja na kuwa Rais na prodyuza mkuu wa mfuko wa Unity Productions, Michael Wolfe (aliyezaliwa 3 Aprili 1945, Marekani) ni mtunzi wa vitabu vya kishairi, hadithi za kubuni, za masafa na historia. Pia ni mhadhiri wa masuala ya kiislamu katika vyuo vikuu nchini Marekani, vikiwemo kile cha Harvard, Georgetown, Stanford, SUNY Buffalo, na cha Princeton. Ana shahada ya fani ya fasihi (sanaa) kutoka Chuo Kikuu cha Wesleyan.
Ana asili ya dini mbili, Uyahudi kutoka kwa baba na Ukristo kutoka mama yake. Hivyo alikuwa na fursa ya kusherehekea sikukuu zote Hanukkah na Krismasi. Anaandika:
“Baba yangu ni Myahudi, mama ni ni Mkristo. kutokana na uchotara wangu, mguu mmoja upo katika Uyahudi na mwengine upo katika Ukristo. Imani zote zilikuwa hazina mashaka kwangu. Hata hivyo, ile iliyokuwa inahamasisha ‘wao wao tu’ (waliobarikiwa) [Uyahudi] niliiona haiungani mkono nami, na ile nyengine iliyojaa mafumbo [Ukristo] haikunifurahisha”
Kutembea kwake kwingi na kupenda vitabu kulimfanya kuufahamu Uislamu ambao kani (nguvu ya uvutano) yake ilishindwa kuzuiliwa na Michael. Moja ya sababu iliyomfanya akubaliane na Uislamu ni kukuta katika Uislamu mambo yanayoendana na matakwa yake. Hivyo anasema:
“Sikuweza kuorodhesha mahitajio yangu yote, lakini angalau nilikuwa najua kipi nikifatacho. Dini niitakayo mimi ni dini itakayoweza nieleza kuhusu metafizikia (falsafa ya kuchunguza chanzo cha uhai na maarifa) kwani metafizikia ndiyo sayansi. Sitaki ile inayopongeza utumizi duni wa akili, au iliyojaa mafumbo ili kuwaridhisha wachungaji. Isiyokuwa na wachungaji (viongozi), isiyokuwa na tofauti kati ya uasili na vitu vyake vilivyobarikiwa. Ambapo kutakuwa hakuna vita na nyama. Tendo la ndoa liwe ni la asili tu na sio eti kutokana na laana waliyopewa viumbe. Mwishowe, nilitaka ibada ya kila siku itakayoongoza nidhamu yangu. Zaidi ya yote, nilitaka jambo lililo wazi na uhuru wa kweli. Sikutaka niwe katika mkumbo wa kufata vitu kibubusa.* Na kila nilivyokua nausoma Uislamu, ndivyo ulivyokuwa ukiafikiana na matakwa yangu.”
Michael wolfe amekuwa Muislamu akiwa na miaka 40, baada ya kushindana na imani tofauti tofauti kwa miaka 20. Ingawa inatosha kwa mtu kufanya Hijja mara moja tu katika maisha, Bw. Wolfe katika kugombania kwake kupata radhi za Mwenyezi Mungu, amehiji si chini ya mara tatu, Hijja yake ya mwanzo ikiwa mwaka 1991. Akiuona ukweli wa Uislamu na ujinga wa baadhi ya watu katika faida ya Uislamu, Michael aliona haja ya kuandika haya:
“Rafiki zangu walioathiriwa na siasa hawakuridhishwa na chaguo langu jipya. Wote walichanganya Uislamu na viongozi madhalimu wa Mashariki ya Kati waliodhaniwa kutaka kufanya mapinduzi ili watawale. Vitabu walivyosoma, habari walizotazama vyote vilichukulia dini hii kama mpango wa kisiasa tu. Halikuwapo linalosemwa kuhusu ibada zake. Napenda kumkariri Mae West kwao pale alivyosema: “Muda wowote utakaochukulia dini mzaha, basi wewe ndio utakayechekwa.” Kihistoria, Muislamu anaiona dini kama ni hitimisho, mmea uliopevuka ambalo ulipandwa tangu wakati wa Adam. Imejengwa kwa msingi wa kuabudu Mungu mmoja kama Uyahudi, ambayo mitume wake Uislamu unawachukulia kama ni ndugu waliotoka kumoja na kilele chao kikiwa Yesu na Muhammad. kusema kweli, Uislamu umefanya kazi kubwa katika hatua ya kuirudisha ladha ya maisha kwa mamilioni ya watu. Kitabu chake, Qur’an kilimfanya Goethe kusema, “Mnaiona hii, mafundisho yake hayashindwi abadan; pamoja na mifumo yetu yote ya kibinaadam, hatuwezi kufika, na huo ndio ukweli hakuna mfumo wa kibinaadamu utakaofanikiwa”.
Akiongea na mtangazaji Bob Faw kuhusu imani yake mpya. Faw ‘alimpiga’ bwana Wolfe kwa swali hili: “Kwa kuwa ushakuwa muislamu, je kuna tofauti yoyote kwako labda!?” Wolfe akajibu: “Bila shaka ipo, umbile nilokuwa nalikosa zamani maishani mwangu lipo sasa nami. nalihisi kabisa.” Wolfe alivutiwa sana na mafundisho ya Uislamu kuwa kila mtu azungumze na Mungu mwenyewe, bila kuwa na kizuizi katikati:
“Hili jambo la kufanya mazungumzo na Mola wako mtukufu bila kuwa na balozi katikati, kusikohitaji jengo fulani au mtu maalum, kunanipendeza mno.”
Michael Wolfe anajulikana zaidi kwa filamu yake katika kipindi cha Nightline cha ABC iliyorushwa Aprili 18, 1997 ikijulikana kama An American in Mecca (Mmarekani Akiwa Makkah). Kipindi hiko kikateuliwa kuwemo katika tuzo za Peabody, Emmy, George Polk na National Press Club. Filamu ilishinda tuzo ya mwaka kutoka katika Baraza la Waislamu (Muslim Public Affairs Council). Michael Wolfe alishiriki kutengeneza, na kusimamia uhariri wa filamu ya masaa mawili iliyohusu maisha ya Mtume Muhammad iliyoitwa Muhammad: Legacy of a Prophet. Filamu hiyo ilioneshwa nchi nzima na PBS na baadae kuonyeshwa kimataifa na National Geograpghic International. Filamu ilituzwa na Cine Special Jury Award kwa filamu bora izungumziayo watu au mahali. Wakati wakutengeneza filamu hiyo, washiriki walihitaji kuperuzi kwingi katika maisha ya Mtume. Michael Wolfe mwenyewe anakiri kusoma Ibn Kathir na vitabu vyengine vya seerah (mwenendo wa Mtume). Kiukweli, kukawa na Wamarekani wengi ambao walisilimu baada ya kuona filamu hii. Katika mahojiano, Islam Online walimuuliza alichovuna baada ya zoezi hili kubwa la kuandaa filamu hii ya Muhammad na alijibu kama ifuatavyo:
“Nimemjua Mtume vyema zaidi kuliko mwanzo kabla hatujaanza kutengeneza filamu hii japokuwa kumsoma kwangu ndio kwanza kulianza. Kuna mengi ya kujifunza. Wakati tunatengeza filamu hii, niliweza kuona na kufahamu hali ya Waislamu wa Marekani. Najua sasa wepi ni Waislamu na vipi tunafanya. Ni kifungua jicho kwangu mimi kama Mmarekani niliyezaliwa hapa, ni jambo la faraja sana kukutana na watu kutoka sehemu mbalimbali, watu wenye lugha tofauti na mengineyo. Ni moja ya hazina za kuwa Muislamu.”
Katika mahojiano tofauti, Michael Wolfe kama mmoja wa waandaaji wa filamu ya Muhammad: The Legacy of a Prophet, alisema:
“Kwa Wamarekani wengi kutokuwa na uelewa wa imani yangu kunanishangaza sana. Japokuwa Uislamu ni dini inayokua kwa kasi zaidi, bado tabia nyingi za Wamarekani kuhusu Uislamu zimekuwa zikitawaliwa na chuki, kuelewa vibaya na hata wakati mwengine uhasama wa wazi. Wana uelewa mdogo tu kuhusu Mtume aliyefundisha dini hii na ipi ni misingi ya ibada zetu. Siasa na mila za watu wa mashariki ya Kati, gumzo la ugaidi vyote vimeshiriki kukandamiza uelewa wao mzuri wa dini. Ukichukulia kwamba kundi kubwa la Waislamu haliko hata Mashariki ya Kati bali Indonesia, utambuzi huu nasema kweli unapotosha.”
Filamu nyengine alizoshiriki Wolfe katika uandaaji ni Cities of Light: The Rise and Fall of Islamic Spain (Miji ya Muangaza: Kupanda na Kuporomoka Kwa Dola ya Kiislamu Hispania) na Prince Among Slaves (Mfalme Miongoni Mwa Watumwa). Sanjari na hilo, Wolfe ameshiriki katika vipindi mbalimbali vya redio. Anaandika makala maalumu iitwayo “From A Western Minaret” kwa ajili ya jarida la mtandaoni Beliefnet.com.
Kazi zilizochapishwa za Wolfe ni pamoja na The Hadj: An American’s Pilgrimage to Mecca. (New York: Atlantic Monthly Press, 1993. Kina kurasa 352); One Thousand Roads to Mecca: Ten Centuries of Travelers Writing about the Muslim Pilgrimage, (New York: Grove Press, 1997. Kina kurasa 656) ; na Taking Back Islam: American Muslims Reclaim their Faith, (Rodale Press, Pennsylvania, 2003. Kina kurasa 256). Baadhi ya tuzo alizopokea ni pamoja na Lowell Thomas Award, “Best Cultural Tourism Article, 1998”; Marin County Arts Council Writers Award, 1990, na 1983; California State Arts Council Writers Award, 1985. Michael Wolfe alitangazwa mshindi wa Tuzo ya 2003 ya Wilbur Award kwa kitabu bora cha mwaka kuhusu dini. Anaishi mwishoni mwa mtaa salama, uliofungwa, huko Santa Cruz.**
|
** Hii ilikuwa ni Dondoo (excerpt) ya kitabu cha Salim Boss kiitwacho“Wao Ima ni Waerevu Mno au Wajinga Mno” chenye kurasa 672 zote zimechapishwa kwa rangi (full colour). Ni tarjama ya kitabu kilichouzika sana kiitwacho “They are Either Extremely Smart or Extremely Ignorant” Kwa usomaji wa ziada tembelea www.extremelysmart.org au www.facebook.com/muerevumno “**
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.