YUSUF ISLAM (CAT STEVENS)
"Ewe Mungu! Kama ukiniokoa nitafanya kazi kwa ajili yako."
Hapo Cat Stevens alipokuwa bichi (ufukoni) ya Malibu ambapo kuogelea kwake kwa starehe kulivyogeuka kuwa jinamizi. Alikuwa akihangaika kujinasua kuzama.
Ilikiwa mnamo terehe 21 Julai 1948, Steven Demtre Georgiou ambae baadae alijulikana sana kwa jina lake la stejini Cat Stevens alizaliwa tena kutoka kwa baba muumini wa kanisa la Kigiriki na mama muumini wa kanisa la Kisweden. “Nimezaliwa katika familia ya Kikristo ambayo iliheshimu pesa na mie nikaingia katika mkumbo huo. Niliwapenda sana waimbaji (wanamuziki) ikafikia hatua wakawa ndio kama miungu yangu, baadae nikaamua kuwa mmoja wao. Nikaishia kuwa msanii mkubwa wa nyimbo za pop, vyombo vya habari vikanifanya niwe supastaa mkubwa kuliko maisha yenyewe na hata nikaona kuwa mimi ni mtu wa kuishi milele,” Alisema.
Cat Stevens ni muimbaji, mtunzi wa nyimbo, mpigaji vyombo tofauti vya muziki, mkufunzi, na msaidizi wa watu wengi kimuziki na kimaisha. Amekuwa msanii mkubwa wa pop tangia ujana wake (kabla ya miaka 20). Kupitia jina lake la Cat Stevens amewahi uza nakala za albamu zisizopungua milioni 60 duniani kote tangia miaka ya 1960. Msanii huyu maarufu anayetokea Uingereza alikuwa na uwezo wa kuingiza zaidi dola 150 000 kwa usiku mmoja ‘mfukoni mwake’. Cat Stevens alikuwa kashafanikiwa kupata kila kitu ambacho wengi duniani wanaota kuwa navyo: umaarufu, kipaji, utajiri, muonekano mzuri, na usumaku kwa jinsia ya pili, lakini bado akahisi kuna kitu anakosa. Japo kuishi kwake kote katika maisha ya ‘usupastaa’, Cat Stevens kwa mara moja ilitokea akapokea wito kutoka katika mwamsho wa kiroho. Alikuwa mgonjwa sana, akisumbuliwa na kifua kikuu na moyo. Hatimaye, Cat Stevens alilazwa hospitali kwa muda mrefu, jambo ambalo likamfanya atafute maana halisi ya kuishi.
Na ilipofika mwaka 1976, Stevens alipokea simu nyengine ya mwamsho wa kiroho. Na sasa, ilikuwa katika pwani ya Malibu huko California, ambapo alikuwa nusra afe maji kwa kuzama. Akapiga kelele sana “Ewe, Mungu kama ukiniokoa hapa, nitafanya kazi kwa ajili yako.” Na baada ya kuokoka pale, kweli alianza safari yake ndeefu ya kutafuta ukweli wa kiroho. Alitazama katika imani tofauti tofauti kama vile Ubudha, Zen, I Ching, Numerolojia (imani ya nguvu kupitia idadi), na Astrolojia (uhusiano wa binaadam na mfumo wa jua). Baadae akaandika,
"Utafiti wangu wa muda mrefu uliendelea pamoja na muziki wangu mpaka siku rafiki yangu aliporudi toka Mashariki ya Kati na kunambia amepata utulivu toka msikitini ambao hakuweza kuupata alivyokuwa kanisani, na kunivutia kufatilia jambo hilo. Haraka haraka nikanunua Qur’an iliyotafsiriwa. Na kweli hatimaye nikapata majibu ya maswali yangu: Mimi ni nani? Wapi natokea? Na lipi ni dhumuni langu hapa duniani? Na baada ya kuendelea kupitia kitabu hiki nikagundua kweli kuna Mungu mmoja tu ambae tunaweza kuwasiliana nae pasipo na pazia lolote katikati."
Ilikuwa ni Qur’an ndio iliyompa amani ya moyo aliyokuwa akihangaika kuitafuta siku zote. “….Naomba niweke wazi kuwa sikukutana na Muislamu yeyote kabla ya kusilimu kwangu. Nimeisoma Qur’an tu na nikaelewa hakuna mtu mkamilifu. Ila Uislam umekamilika na kama tukaiga mwenendo wa huyu Mtume aliyebarikiwa (rehma na amani ziwe juu yake) tutafanikiwa”.
Akaja kuelezea zaidi:
"Kila kitu chake kinaingia akilini. Na huu ndio uzuri wa Qur’an; inakufanya wewe utafakari na utumie bongo lako…. Wakati nilipoisoma Qur’an zaidi na zaidi, niliona ikiongelea kuhusu kusimamisha swala, huruma na sadaka. Nilikuwa bado sio Muislamu lakini nilihisi jibu la maswali yangu ni Qur’an tu ambayo Mungu atakuwa kaniletea zawadi."
Akaingia rasmi katika uislam mwaka 1977, na kubadili jina kuwa mwaka 1978. Baada ya kusilimu, Yusuf Islam alitangaza kuwa muziki wake wa pop wote ulikuwa sio wa kiislamu, hivyo akapiga mnada magita yake, na rikodi zake zote na yaliyopatikana yote aliyatumia kutoa misaada ya kiislamu. Ilifika hatua hadi akalumbana na kampuni za muziki kuwa waache kuhifadhi miziki yake ambayo mwenyewe alichukulia baadhi yake iko nje ya maadili. Kuelezea hitajio lake la kuuacha muziki alisema, “….nina ajenda nyengine ya kutimiza; nahitaji kuisoma imani yangu, kuangalia familia na kupangilia na kuziweka wazi vipaumbele vyangu."
Kwa makadirio Januari 2007, alikuwa bado anaingiza karibia dola za kimarekani milioni moja na nusu kwa mwaka kutoka katika muziki wake wa kale (Cat Stevens music), aliamua kutumia yale makusanyo ya maingizo yake yote katika kusaidia watu mbali mbali kimaisha na kielimu katika sehemu wanazopatikana Waislamu wengi kule London na kwengineko kama mayatima Bosnia. Mwaka 1982, yeye na Waislamu wenzake waliguswa kuona watoto wao hawapati elimu bora ya kiislamu kule kwao Uingereza. Hivyo, wakaamua kuanzisha Mfuko wa Shule za Kiislam (Islamia Schools’ Trust) ambao ukaja kusaidia uanzishaji wa shule ya msingi ya kiislamu pale London mwaka unaofatia na shule ya sekondari baadae mwakani.
Yusuf Islam alijulikana zaidi kwa kuunga mkono kiuwazi kabisa hukumu ya kuuawa iliyotolewa na Ayatollah Khomeini kwa Salman Rushdie mnamo Februari 1989. “Salamin Rushdie, na waandishi wengine wote ambao wanamtusi Mtume Muhammad au Mtume mwengine yeyote, katika sheria za kiislam anatakiwa kuuawa,” alisema hayo wakati ule wale wanaomtukana Mungu na dini yake walipokuwa wanatafutwa. Akionesha kumtusi Mungu ni dhambi kubwa sana, alisema; “Kama ukimuuliza mwanafunzi yeyote wa Biblia akupe adhabu ya mtu kama huyu anayemtukana Bwana Mungu atakuwa hajatenda haki kama hatataja Mambo ya Walawi 24:16, “Na yeye atakayelikufuru jina la Bwana hakika atauawa; mkutano wote watamwua kwa kumpiga kwa mawe; kama ni mgeni, kama ni mzalia, hapo atakapolikufuru jina la Bwana atauawa."
Yusuf Islam ameshatunukiwa tuzo nyingi mpaka sasa ikiwemo ya Tuzo ya Mtu wa Amani (Man for Peace Award) itolewayo na Mikhail Gorbachev kwa juhudi zake za kutangaza amani duniani, suluhishi baina ya watu na kuuondoa ugaidi; Mwaka wa 2005, alipata Udokta wa Heshima (Honorary Doctorate) katika Chuo Kikuu cha Gloucestershire kwa huduma zake katika elimu na ubinaadamu; 2007, The Mediterranian Prize for Peace (Tuzo ya Amani ya Mediterrania) huko Naples, Italia; Udokta mwengine wa Heshima kutoka Chuo Kikuu cha Exeter (10 Julai 2007), kwa huduma zake za kijamii na kusaidia kuongeza maelewano baina ya Waislamu na Wamagharibi.
Kwa sasa anaishi na mkewe Fauzia Mubarak Ali, na watoto wao watano huko Brondesbury Park, London na kutumia sehemu ya kila mwaka Dubai. Katika kuwajibu wale wanaotumia ubaya wa waislamu kupoteza ukweli wa Uislamu wenyewe, Yusuf Islam alisema:
“Itakuwa ni makosa kuuhukumu Uislamu kwa kutumia tabia za Waislamu waovu ambao wanatokezwa katika vyombo vya habari siku hadi siku. Ni kama kuhukumu gari iliyo nzuri kisa ndani yake kuna dereva mbaya ambaye kalewa na kuligongesha ukutani gari hilo. Uislamu unawaongoza binaadamu katika maisha yao ya kila siku- kiroho, kiakili na kimwili. Yatupasa tutazame vyanzo vya mafundisho yake kama Qur’an na sunnah za Mtume, hapo ndio tutaona ukweli wa Uislamu.”**
** Hii ilikuwa ni Dondoo (excerpt) ya kitabu cha Salim Boss kiitwacho“Wao Ima ni Waerevu Mno au Wajinga Mno” chenye kurasa 672 zote zimechapishwa kwa rangi (full colour). Ni tarjama ya kitabu kilichouzika sana kiitwacho “They are Either Extremely Smart or Extremely Ignorant” Kwa usomaji wa ziada tembelea www.extremelysmart.org au www.facebook.com/muerevumno “**
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.