MBINU ZA MALEZI
Malezi yana mbinu maalumu ambazo yataka tuzifahamu, ili tuweze kuwalea watoto wetu kwa njia za kisawa. Mbinu hizi zinabadilika kulingana na mabadiliko ya kitaaluma yanavyobadilika kwa kasi sana.Pamoja na athari ya tamaduni zinazotufikia kupitia mitandao mbalimbali. Kwa hivyo kuna dharura ya kuzifahamu mbinu hizi haswa ukizingatia kuwa kuna athari ya utandawazi katika ulimwengushi au ulimwengu wa kijiji kimoja.Mambo yafuatayo ni muhimu yazingatiwe:
1.Kwanza mbinu ya kuwa wewe ni kiigizo chema kwa namna unavyomlea mtoto au jinsi jamii inavyokutazama wewe pamoja na mambo unayoyatenda kuliko unayoyasema. Kwa hivyo kuwa mfano mwema ni muhimu sana katika malezi.
2.Pili ni mbinu ya mawaidha mazuri na kumuelekeza mtoto wako mara kwa mara katika njia iliyonyooka.Kutoa mwongozo wa kimaisha kwa unayemlea ni jambo muhimu sana.Hivi kwamba akue akijua mwelekeo unaoutaka wewe kama mlezi wake.
3.Tatu mbinu ya kumpendezesha na kumwonesha uzuri wa lile unalotaka alifanye, vipi lina athari na maisha yake na kumwonesha vipi atafaulu akifuata yale unayomfahamisha.
4.Nne mbinu ya kumtahadharisha na kumwonesha madhara na hasara atakazopata katika maisha yake na ubaya wa tabia ile mbaya unayomkataza.Kwa mfano madhara ya kutohifadhi wakati, kukhalifu ahadi, kutokuwa na uaminifu katika maisha yake pamoja na tabia mbaya nyingi.
5.Tano ni mbinu ya kupigia mtoto wako mifano hai ili aweze kutofautisha baina ya faida na hasara za tabia mbalimbali.Mfano Amati mwalimu mwanachuoni wa kike ambaye mpaka leo yupo katika uhai na amefundisha Qur’an miaka 110.Huu ni mfano hai katika nchi ya Kenya mwanamke mshela atumia umri wake wote katika kufundisha dini.Hivi ndivyo jinsi tunavyopaswa kujitolea kwa manufaa ya jamii.
6.Sita ni mbinu ya kutumia visa vilivyotokea katika kurekebisha tabia fulani. Utoaji wa visa ni mbinu muhimu sana katika kulea mtoto.Kwani waliotangulia walipatikana na mambo mengi ambayo lau watoto wetu watakuwa wakihadithiwa watapata mazingatio mengi sana.Mfano wa kile kisa cha yule mwanamume aliyeuwa watu 99 kisha akarudi kwa ALLAH(S.W.T) kumtaka msamaha.Akakutana na msomi aliyemshauri atoke katika mji ule anaoishi aende katika mji wa watu wazuri.Kisa ni kirefu lakini faida yake ni kuwa, mwisho ALLAH(S.W.T) akamsamehe.Mazingatio tunayoyapata ni kuwa hatupaswi kukata tamaa na rehma ya ALLAH (S.W.T).
7. Mbinu ya saba ni ya kumzowezesha mtoto kukariri jambo mpaka akazowea kama alivyofundisha Mtume ﷺ Swala juu ya mimbari na kama alivyofundisha Sayyidna Uthman b.Affan (R.A) namna Mtume alivyochukua Udhu.Jambo likirudiwarudiwa linabaki kwenye fahamu ya mtoto.
8. Mbinu ya nane ni ya kufaidika na matokeo fulani kisha ukatumia fursa ile kurekibisha kosa au kutilia nguvu fikra fulani kwa kutumia matokeo fulani.Mfano kumsisitiza mtoto afanye bidii ya kuhifadhi Qur’an baada ya kumwona mwenzake akiswalisha msikitini na mengine mengi.
9.Mbinu ya tisa ni kujaribu kukuza fikra ya mtoto na kuifungamanisha na utumiaji wa busara katika maisha ya wanadamu.Akue akijua kuwa katika maisha kuna mambo mengi yanayohitaji hekima na busara pasi na kutumia nguvu kukabiliana nayo.
10.Mbinu ya kumi ni kujaribu kukusanya mazoezi uliyoyapata kulingana na tajriba yako katika kutaamaliana na binadamu wengine.Mtoto wako awe karibu na wewe katika kuona ni jinsi gani unataamaliana na watu.Akiona tabia fulani inajirudiarudia hutakuwa na haja ya kumwambia afanye bali atafanya mwenyewe kwa sababu amekuwa akikuona jinsi gani unavyotaamaliana na watu.
11.Kumi na moja ni mbinu ya kutumia mazungumzo mazuri katika kutafuta usawa wa jambo.Na vilevile kukinaisha watu katika kutazama mambo na vishawishi tofauti katika maisha.
12.Kumi na mbili ni kujaza nafasi au pengo kwa kutumia fursa inapojitokeza au kubuni nafasi ya kurekibisha jambo kwa njia ya hekima na busara.
13.Kumi na tatu ni kuangalia jinsi watu wanavyosuhubiana katika safari na kutazama vitendo vyao katika safari hizo kwani mara nyingi watu wanafahamika na kudhirika jinsi walivyo wakati wakiwa kwenye safari.
14.Mbinu ya Kumi na nne ni yakuadhibu na hii yafaa itumike ya mwisho baada ya kutofanya kazi mbinu zote kumi na tatu zilizotangulia.Mbinu hii yafaa itumike kwa uwangalifu mno na adhabu iwe ya kipimo na iambatane na kosa mara tu linapofanyika.Kwa mfano ni makosa kwa mzazi kumwadhibu mtoto wake leo kwa kosa alilotenda wiki iliyopita.Changamoto ni kuwa wazazi wengi hawajui mbinu hizi,wao hupindukia katika kutesa na kuadhibu tu.
Hivyo basi ni muhimu sana kuzingatia mbinu hizo ili zirahisishe malezi haswa katika ulimwengu huu wa utandawazi.
Makala yameandikwa na: Sheikh Abu hamza
Kusahihishwa kilugha na: Ustadh Ali Juma
Makala yanaendelea…
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.