MWEZI WA MFUNGO SITA
Mwenyezi Mungu mtukufu ameitukuza baadhi ya miezi kuliko miezi mengine na akawataka waja wake wasijidhulumu katika miezi hiyo kwa kufanya Madhambi na kuasi.Mwenyezi Mungu asema katika Qur'ani tukufu:
إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللَّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللَّهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ ۚ فَلَا تَظْلِمُوا فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ التوبة:36
[Hakika idadi ya miezi kwa Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na mbili katika hukumu ya Mwenyezi Mungu tangu alipo umba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko mine mitakatifu. Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu humo] [Al-Tawba:36]
Na Mtume wetu ﷺ akaja kubainisha Miezi hiyo mitakatifu kuwa ni mwezi wa Dhulqaada, Dhulhijja, Muharram na Rajab, hii ndio miezi mitakatifu iliyotajwa na Mwenyezi Mungu alietukuka.
Ama kuhusu Mwezi wa Mfungo sita hakuna dalili katika Qur'ani wala katika Hadithi za Bwana Mtume ﷺ kuwa ni katika Miezi ambayo ni mitakatifu, ila tu katika Mwezi huu kumetokea matukio muhimu katika tarekhe ya Uislamu,na katika matukio hayo:
1.KUZALIWA MTUME WETU MUHAMMAD ﷺ
Ni kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad ﷺ kwa kauli ya wengi katika wanazuoni wa tarekhe ya Kiislamu, ila tu kuna wanao sema kinyume na mwezi huu kwani hakuna dalili ya wazi ya kuonyesha kuwa mtume ﷺ alizaliwa mfungo sita lililo afikiana na siku ya kuzaliwa kwake nayo ni siku ya juma tatu kama ilivyo kuja kwenye hadithi alipoulizwa kuhusu kufunga siku ya ijuma tatu akasema:
فِيهِ وُلِدْتُ وَفِيهِ أُنْزِلَ عَلَيَّ] رواه مسلم]
[Siku hiyo (Juma tatu) nilizaliwa na siku huyo nikateremshiwa wahyi (ufunuo).]
2.KUGURA KWA BWANA MTUME MUHAMMAD ﷺ
Mtume ﷺ baada ya kupata pingamizi makkah katika Da'wa yake na kupata udhia kwa Maquraish na kufanya njama za kutaka kumuuwa, Mwenyezi Mungu alimwamrisha mtume wake kugura kutoka Makkah na kuhamia Madina; Mtume alitoka makkah tarehe mosi ya mwezi wa mfungo sita na kufika madina tarehe kumi na mbili katika mwezi huo.
3.KUFARIKI MTUME MUHAMMADA ﷺ
Tukio la tatu katika Mwezi huu wa Mfungo sita ni tukio kubwa sana nalo ni kufariki Mtume wetu Muhammad ﷺ tukio lililo kuwa zito sana kwa Maswahaba wa Bwana Mtume na waislamu wote, Mtume ﷺ alifariki siku ya ijuma tatu tarehe kumi na mbili mwezi wa mfungo sita na tarehe hii ndio rai ya Jamhuri ya wanachuoni.
Kwa hivyo haya ndio matukio muhimu yaliyotokea katika Mwezi huu wa mfungo sita. Lakin leo watu wamezua mengi katika Mwezi huu mambo ambayo yalikuwa hayajulikani wakati wa Mtume ﷺ na Maswhaba wake, na jambo lolote lisilo kuwa ni dini wakati wa Mtume ﷺ na Maswahaba wake basi haliwezi kuwa ni Dini wakati wowote ule.
Na katika mambo yaliyozuliwa katika mwezi wa mfungo sita ni kusherehekea kuzaliwa kwa Bwana Mtume ﷺ, hili ni jambo ambalo limezuliwa katika dini wala Maswahaba na Qarni tatu zilizo bora jambo hili walikuwa hawalijui, na kama ni jambo zuri hili la kusherehekea Mazazi ya Bwana Mtume ﷺ basi wao wangelikuwa ni wa kwanza kulifanya hilo kwani wao walikuwa wakimpenda Mtume kutuliko sisi.
Na hapa napenda tutafautishe kumsifu mtume ﷺ na kumswalia Mtume ﷺ na kusherehekea mazazi ya Mtume ﷺ maana kuna watu wachanganya mada hizi na kufanya ni jambo moja.
Hakuna anaepinga kumswalia Mtume ﷺ wala kumsifu Mtume ﷺ, kwani tumeamrishwa na dini yetu kumswalia Mtume katika swala mara tano kwa siku na kumswalia wakati wowote. Na kumsifu Mtume Muhammad ﷺ amesifiwa na Allah aliyemtukufu ila tu nawe usivuke mipaka katika sifa zako na kumsifu kwa sifa ambazo hastahiki kuwa nazo. Linalo pingwa nikuweka sherehe Maluum ya kusherehekea kwa kuzaliwa kwake kama wengi wanavyo fanya hili ndilo jambo linalo pingwa kwani hilo ni Uzushi lililozushwa katika dini.
NI NANI ALIE ANZISHA SHEREHE ZA MAULIDI
Jambo hili la kusherehekea kwa kuzaliwa Mtume ﷺ lilianzishwa na Mashia katika zama za dola ya Fatimiya na aliezuwa jambo hili ni Al-Muizz lidinillah Al Fatwimiy na wanachuoni wasema kuwa hawa walikuwa ni Mazandiki na lengo lao lilikuwa ni kutaka kuwaiga manaswara kwa hilo, kwa fikra ya kwanini wakiristo wako na siku ya kusherehekea siku ya kuzaliwa Nabii Issa Alayhi salaam na sisi waislamu hatuna. Hawajui kuwa dini yetu imekataza Waislamu kujifananisha na Mayahudi na Manaswara, hata jambo la ibada ya kufunga Mtume ﷺ alipofunga Ashuraa akasema atafunga na taasua ili awakhalifu Mayahudi.
Mwisho:
Waislamu tusomeni dini yetu na tuifahamu vyema na tusiwe washindani katika mambo ambao yako wazi kuwa ni kinyume na Mafunzo ya Bwana Mtume rehma na amani zimfikie yeye… twamuomba Allah atujalie tuwe ni wenye kufaidika Na tunayosoma. Amin
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.