ATHARI MBAYA YA MADAWA YA KULEVYA KWA MABAROBARO

13698 

 

Allah amemkirimu mwanaadamu kwa kumpa akili na fahamu na akamuelekeza kwa kufikiri na kuzingatia, akili ikawa ndio neema kubwa ya Allah kwa huyu mwanadamu, akili ndio inayotufahamisha baina ya mwanadamu, wanyama na visivyokuwa na roho. Enyi waja wa Allâh! Allâh Mtukufu amewakirimu wanadamu juu ya viumbe vyake vingi, akasemaSubhaanahu wa Taala:

 

{وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَرَزَقْنَاهُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَىٰ كَثِيرٍ مِّمَّنْ خَلَقْنَا تَفْضِيلًا}    الإسراء:70

 

"Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba."  [Al-Israa:70]

Allâh amewakirimu wanaadamu kwa mambo mengi aliyo wapambanua na viumbe vingine vikiwemo, visivyo na roho, wanyama, mimea na majini, alimkirimu kwa akili na fahamu na akamuelekeza kwa mazingatio na kutafakari, kwa hivyo akili ikawa ndio neema kubwa zaidi kutoka kwa Allâh, kwayo, mwanadamu huweza kupambanua baina ya kheri na shari madhara na manufaa, kwayo huweza akafurahia maisha yake, kuendesha mambo yake na kustarehe, kwayo ndio umati zote ziweze kupanda na maisha kuendelea.

Akili ni johari yenye thamani, wenye akili huwa wakiihifadhi na kuihami kwa kuukubali ubora wake na kuhofu wasije wakaipoteza.

Mwanadamu anapoikosa akili yake basi hakuna atakayemtofautisha baina yake na wanyama, anayeikosa akili yake huwa hana manufaa bali huwa ni mzigo kwa familia na jamii yake. Akili hii ya thamani hupatikana kwa wanadamu kwa watu wasiyoiangalia kuitunza na kuihami. Bali katika watu, yuko anayeikanyaga akili chini ya nyayo zake akifuata matamanio yake na macho yake yakawa hayaoni, hata jambo hilo likawa wazi kabisa.

Mtu anapokunywa pombe au kutumia madawa ya kulevya au akanusa ulevi, basi hapo huanza kukosa akili akajiinua kutoka katika ulimwengu wa ubinadamu na akavaa nguo ya maovu na mauaji. Hapo mlevi huanza kupooza na akamsahau Mola wake, akaidhulumu nafsi yake, akaondokana na haya aliyokuwa nayo, watoto wake akawafanya mayatima na mkewe akawa mjane kwa sababu ya kukosa akili.

Hapo akawa amelitupa jambo la dharura maishani mwake katika yale mambo matano ambayo sheria za mbinguni zimeafikiana kwamba ni wajibu mtu kuyahifadhi mambo hayo, nayo ni akili, ni wajibu mtu kuhifadhi akili na kuichunga, anayeikosa akili yake kwa kulewa, atakuwa ameikosa akili na jamii yake, na ataitumbukiza jamii yake na waumini wenziwe katika maporomoko ya udhalilifu na maangamizi, hapo amani ikakosekana na jamii ikatishia amani.

Watumiaji wa madawa ya kulevya hukosa kuyasimamia majukumu waliyonayo na kusimamia akili zao. Mamia ya Waislamu wamepotea kwa sababu ya madawa ya kulevya na ulevi. Roho zao zimeenda kwa Mola wao huku wakiwalalamikia wale mafasiki na waovu waliojiingiza wao wenyewe na kuwaingiza wengine katika maangamivu.

Haya madawa ya kulevya yamewapeleka watu waliokuwa na familia katika jela miaka mingi yakiwa ndio malipo ya yale makosa waliyoyateuwa familia zao zikabakia bila ya msimamizi, wake zao wakawa kama wajane, watoto wao kama mayatima, wakapoteza ubarobaro na maisha mazuri waliyokuwa nayo, mustakbali wao wakaupoteza kwa mitaimbo ya maadui zao jela zikawa zimejaa pomoni namna walivyokuwa wengi.

Wenye akili dhaifu huyapokea wanayoletewa na maadui na kuenezwa na madalali waovu.

Bila shaka ni misiba iliyowapata Waislamu, nao wameghafilika na mambo wanayopelekewa, maadui wamejua njia ya kuingia kwa Waislamu.

Allâh Subhaanahu wa Taala Amesema kweli wakati Alipotuambia:

     {وَلَا يَزَالُونَ يُقَاتِلُونَكُمْ حَتَّىٰ يَرُدُّوكُمْ عَن دِينِكُمْ إِنِ اسْتَطَاعُوا}        {البقرة :217}

"Wala hawatoacha kupigana nanyi mpaka wakutoeni katika Dini yenu kama wakiweza." [Al-Baqara:217]

Ajabu kubwa ni kwa yule anayenunua ufisadi kwa mali yake!

Kwa nini mtumiaji wa madawa ya kulevya hawezi kupata mawaidha kwa wale waliopata mikasa katika familia zao, ikawaangamiza kabisa, na ni vipi ajitoe katika kundi la watu wenye akili na heshima zao ajipeleke katika kikundi cha wendawazimu wasio na akili?. Al-Hassan Al-Basry Mungu amrehemu Amesema: “Lau kama akili ingalikuwa inauzwa bila shaka ingekuwa ni ghali mno.”

Basi iweje tena mtu aiharibu akili yake yeye mwenyewe? Kwa hakika huu ni msiba uliowashukia watoto wa Kiislamu. Tunamuomba Allâh atuongoze. Kwa ajili hiyo, kutumia kila kinachoondoa akili au kuilewesha kwa kinywaji au chakula au kinginecho, inakuwa ni haramu.

Katika Qur’an Allâh Subhaanahu wa Taala Amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ إِنَّمَا يُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُوقِعَ بَيْنَكُمُ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاءَ فِي الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ وَيَصُدَّكُمْ عَن ذِكْرِ اللَّهِ وَعَنِ الصَّلَاةِ ۖ فَهَلْ أَنتُم مُّنتَهُونَ

 

"Enyi mlio amini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shet'ani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa. Hakika Shet'ani anataka kutia kati yenu uadui na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali. Basi je, mmeacha? [ Al-Maaida:90-91]

Kwa mujibu wa Aya hii, pombe ni najisi, kwa sababu, Allâh Amesema: “rijs, ni uchafu” Katika maneno ya Waarabu, rijs ni kila kilicho kichafu kinachochukiwa na watu. Bali Maswahaba watukufu wamefahamu katika Aya hii kwamba pombe si kama imeharamishwa pekee, bali imelinganishwa na shaka ambayo ndio dhambi kubwa zaidi inayotendwa na mwanadamu.

‘Abdullah Bin ‘Abbas (R.A) amesema: “Ilipoteremka Aya ya kuharamisha pombe, Maswahaba wa Mtume(Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) waliendeana wao kwa wao na wakaambizana kuwa:

[Pombe imeharamishwa na imelinganishwa na shirki].

Hadithi hii imepokewa na Tabarany, wapokezi wake ni wapokezi wa Hadithi Sahihi.

Kwa sababu Allâh Amesema kuhusu pombe: ni rijs katika matendo ya shetani. Na akasema kuhusu shirki: “Basi jiepusheni na (rijs) uchafu wa masanamu”

Hadithi za Mtume (Swallallahu Alayhi Wasallam) na Aya za Qur’an zimetilia nguvu uharamu wa pombe na kutahadharisha, na kukemea kuinywa au kuikaribia, pombe ni alama ya upotevu na anuani ya machafu na maovu kama ilivyopokewa, katika Hadithi ya AbdulRahman Bin Wa’lah (R.A) amesema:Nilimwuliza ‘Abdullahi Bin ‘Abbas kuhusu biashara ya pombe, akaniambia:[Mtume(Swalla Llahu ‘alayhi wasallam)alikuwa ana rafiki kutoka kabila la Thaqif au Daws, akakutana naye Siku ya Fat-hi Makka, akampa zawadi chombo kilichojaa pombe, Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akamwambia: “Ewe fulani kwani hujui kama Allâh Ameiharamisha?” Yule mtu akamwambia mtumishi wake: “Nenda ukaiuze”. Mtume(Swalla Llahu ‘alayhi wasallam)akamwuliza: “Ewe fulani, umemuamrishwa nini?” Akajibu: “Nimemuamrishwa nikaiuze.” Akamwambia: “Aliyeiharamisha kunywewa ndiye Aliyeharamisha kuuzwa”. Akaamrisha, ikamiminwa mchangani]. [Imepokewa na Muslim.]

Katika Hadithi ya Abu Huraira,(R.A) amesimulia: Mtume Swalla Llahu ‘alayhi wasallam amesema:

[Usiku niliopelekwa Israa, huko Eliya (Baitul-Maqdis) nililetewa vikombe viwili vya pombe na maziwa, nikavitazama, nikachukua maziwa. Jibril akasema: Namshukuru Allâh Aliyekuongoza kuchukua fitra (Uislamu), lau ungalichukua pombe, umati wako wangaliangamia].[Imepokewa na Bukhari.]

Katika jumla ya Hadithi zinazoonyesha uharamu wa pombe, ni iliyopokewa kuwa Mtume(Swalla Llahu ‘alayhi wasallam)amesema:[Yoyote anayekunywa hatakubaliwa Swala yake kwa muda wa siku arubaini, na anayekufa ilihali katika kibofu chake cha mkojo ana sehemu katika pombe ataharamishiwa Pepo. Na iwapo atakufa katika siku arubaini(tangu anywe pombe hiyo), atakuwa amekufa kifo cha kijahiliya].[Imepokewa naTwabarani, ameipokea kwa isnadi yake ni sahihi]

Anayekunywa pombe duniani atanyimwa Akhera kama ilivyopokewa katika Hadith ya ‘Abdullah Bin ‘Umar (R.A.) kuwa Mtume(Swalla Llahu ‘alayhi wasallam)amesema: [ Atakayekunywa pombe duniani na asitubie dhambi hiyo, atanyimwa pombe ya Akhera].[Imepokewa na Bukhari na Muslim]

Hadithi nyingine kutoka kwa Mtume(Swalla Llahu ‘alayhi wasallam)inasema:

[Allâh amewalaani watu kumi katika pombe:- mgemaji, anayetaka kugemewa, mnyweshaji, mnywaji, muuzaji, mnunuaji, mbebaji, mwenye kubebewa, mwenye kula thamani yake na mwenye kumnunulia mtu, wote hao wamelaaniwa kwa dua ya Muhammad].

Hikma ya Uislamu imepelekea kuharamisha uchache na wingi wa pombe na vilevi, kwa sababu uchache hupelekea katika wingi, halafu mazoea, kisha ikawa ndio uraibu. Jabir amesimulia kuwa Mtume(Swalla Llahu ‘alayhi wasallam)amesema:

[Chochote kinacholewesha kwa wingi, na uchache wake pia ni haramu].[Imepokewa Abu Dawud na an-Nasa-iy]

Katika mambo ambayo ni wajibu kuyahadharisha ni mti uliolaaniwa, nao ni mti wa bangi na aina nyingine ya miti ya motoni inayolevya inayoangamiza viwiliwili na akili za wanaotumia, ikawafanya wakose mizani na wawe dhaifu wa nguvu na azma, kutumia vichafu hivi huzima nuru ya macho na akili, humfanya mtu mbele ya watu kutokuwa na uadilifu na tabia mbaya. Hucheka na hulia bila sababu, macho humzunguka kama kwamba amefunikwa na mauti.

Maadui wa Uislamu wametengeneza aina nyingi ya madawa ya kulevya, wakatengeneza vidonge vinavyolevya vilivyochanganywa na heroin, haya ni matendo ya shetani, jiepusheni nayo ili mpate kufanikiwa.


TAZAMA VEDIO HII UFAIDIKE ZAIDI

 

comments