SOMO LA FIQHI
Wanachuoni wa Fiqhi wamelezea, mambo yenye kubatilisha upangusaji wa khofu na wakatataja mambo ya fuatayo
1. Kumalizika muda wa upangusaji ulioruhusiwa kisheria kwa mkazi na msafiri.
Muda huo utakapomalizika, mpakazaji anatakiwa kwa mujibu wa sheria azivue khofu zake, kisha atawadhe udhu kamili, hapo ndipo anaweza kuzivaa tena kwa twahara hii mpya na kupata ruhusa ya kupakaza juu yake atakapotawadha tena, pia muda mpya utaanzia hapo.
2. Kupatikana kwa jambo linalowajibisha josho kama vile janaba, hedhi au nifasi.
Katika hali hii imempasa na kumlazimu mpangusaji kuzivua khofu, akoge josho lililomuwajibikia, kisha ndipo anaruhusiwa kuzivaa tena ikiwa anaona kuna haja ya kufanya hivyo. Imepokelewa hadithi na Swafwaan Ibn Assaali Radhi za Allah ziwe juu yake amesema:
كَانَ رَسُولُ اللهِ ﷺ يَأْمُرُنَا إِذَا كُنَّا مُسَافِرِينَ أَنْ نَمْسَحَ عَلَى خِفَافِنَا، وَلَا نَنْزِعَهَا ثَلَاثَةَ أَيَّامٍ مِنْ غَائِطٍ، وَبَوْلٍ، وَنَوْمٍ، إِلَّا مِنْ جَنَابَةٍ» رواه الترمذي والنسائي
[Alikuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu akituamrisha tunapokuwa safarini tupakaze juu ya khofu zetu na wala tusizivue kwa muda wa siku tatu kutokana na kukidhi haja kubwa na ndogo na kulala ila kutokana na janaba (tu)]. [Imepokewa na Tirmidhiy na Nasaai.]
3. Mtu kuzivua khofu zote mbili au mojawapo, hata kama ikiwa uvuaji huo ni kwa kutoa sehemu kubwa ya mguu bila ya kuutoa mguu wote.
Au kwa kutoboka khofu kiasi cha kuuonyesha mguu. Katika hali zote hizi imempasa mpakazaji kuzivua.
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.