SOMO LA FIQHI
Kuoga katika sheria lina hekima na faida nyingi, miongoni mwa hizo ni kama zifuatazo :
1. Kupata thawabu
Hii ni kwa sababu Kuoga kwa maana na mtazamo wa kisheria ni Ibaada kwa kuwa ndani yake kuna kutekeleza amri ya sheria na kuitumia hukumu ya sheria.
Kwa hivyo lina hili la utekelezaji amri na hukumu ya sheria ujira mkubwa.
Ni kwa mantiki hii ndio Bwana Mtume ﷺ akatuambia :
الطُّهُورُ شَطْرُ الْإِيمَانِ] رواه مسلم]
[Twahara ni nusu ya imani] [Imepokelewa na Muslim.]
Ni vema ikaeleweka wazi kuwa twahara imekusanya udhu, Kuoga, Tayammum na mengineyo.
2. Kuwa Msafi
Muislamu anapokoga, mwili wake hutakasika na kuwa msafi.
Usafi huu ni kinga kubwa ya vijidudu vinavyoweza kusababisha maradhi kama vile upele na humfanya muislamu anukie vema, kitu ambacho humkurubisha na watu kwani watu humteta mtu mchafu anukaye.
Imepokelewa kutoka kwa Bibi Aisha Allah amuwie radhi kwamba amesema :
كان أصحاب رسول الله صلى الله عليه وسلم عمال أنفسهم، وكان يكون لهم أرواح، فقيل لهم: لو اغتسلتم.] متفق عليه]
[Maswahaba wa Bwana Mtume ﷺ walikuwa wakijifanyia kazi wenyewe (na hawakuwa na watumishi) wakawa na harufu mbaya ya jasho. Wakaambiwa na Mtume
[Lau mngalikuwa mnakoga]. [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Na katika upokezi mwingine Mtume ﷺ Amesema:
[لو اغتسلتم يوم الجمعة]
[Lau mngalikuwa mnajitwahirisha kwa ajili ya siku ya Ijumaa].
3. Kuwa mchangamfu na kupata nguvu.
Mwili wa mwanadamu anapokoga huwa na nguvu mpya na kurudia kuwa katika hali ya uchangamfu baada ya ulegevu na uchovu ambao humsababisha uvivu na kutokujisikia kufanya jambo lolote zaidi ya kubweteka bwete!
Hili la kujisikia kuchoka na mwili kunyong’onyea hupatikana zaidi mara tu baada ya tendo la kujamiiana.
Kwa maneno ya jumla, Hikma ya kuoga kwa ajili ya twahara na usafi humuandaa mtu na kumuweka katika nafasi nzuri ya kuwasiliana na kuzungumza na Mola Muumba wake ndani ya swala akiwa katika hali njema kabisa.
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.