SOMO LA FIQHI
Tunakusudia kusema kwa istilahi (wenye udhuru) wale watu ambao ambao wana maradhi yanayowafanya wasiweze kuuhifadhi udhu wao kama wanavyoweza watu wengine katika hali ya kawaida.
Hawa ni pamoja na mtu mwenye maradhi ya mchuchuro wa mkojo, hawezi kuuzuia mkojo, saa zote hutokwa na mkojo au anatokwa na upepo (ushuzi) mara kwa mara.
Au mwanamke aliyepatwa na maradhi ya kutokwa na damu ya mbobo/ugonjwa, hii ni damu itokayo kwa wingi katika wakati usiokuwa wa damu ya ada ya kila mwezi (hedhi).
Hukumu ya udhu wa watu hawa ni kwamba wanatakiwa watawadhe kila unapoingia wakati wa kila swala, wasitawadhe kabla ya kuingia wakati kwa kuwa wanatakiwa kufululiza baina ya udhu na swala.
Hii ni kwa sababu kisheria hawana udhu kwani wana hadathi ya kudumu na udhu wao ni wa ruhusa maalum waliyopewa na sheria ili waweze kuyatekeleza yale yote yasiyotekelezeka bila ya udhu, kama vile swala, tawafu na kadhalika.
Wataswali kwa udhu huo swala wazitakazo za suna au za fardhi.
Udhu wa watu hawa utabatilika na kutenguka mara tu unapoingia wakati wa swala nyingine. Akitaka kuswali basi itamlazimu kutawadha tena.
Haya yote yanaonyesha wepesi wa sheria ya Kiislamu ambayo imejengwa juu ya misingi ya wepesi na kuondosha uzito na ugumu. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu :
وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ ۚ مِلَّةَ أَبِيكُمْ إِبْرَاهِيمَ} الحج:22}
[Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini. Nayo ni mila ya baba yenu Ibrahim.] [22:78].
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.