SOMO LA FIQHI
Suali: Ni nini Maana ya Kustanji?
Jawabu: Kustanji au Kutamba ni kusafisha na kuondoa najisi iliyotoka katika mojawapo ya tupu (uchi)mbili au zote mbili; tupu ya mbele na ya nyuma kwa kutumia maji twahara au kinachosimama mahala pa maji wakati wa kukosekana maji kama vile mawe, karatasi, kitambaa, majani na kadhalika.
Na anatakiwa mwenye kutamba ahakikishe amejisafisha vema kiasi cha kutobakia athari ya najisi iliyotoka; ikiwa ni mkojo au mavi.
Suali: Ni ipi Hukmu ya kutamba?
Jawabu: Hukmu ya kutamba baada ya kukidhi haja ni Wajibu kama tutakavyoona katika kauli za Mtume ﷺ katika maelezo yajayo.
Kwa hadithi ya Anas bin Malik radhi za Allah ziwe juu yake kwamba yeye alisema:
كان رسول الله صلى الله عليه وسلم يدخل الخلاء ، فأحمل أنا وغلام نحوي [ معي ] إداوة من ماء وعنزة ، فيستنجي بالماء] رواه البخاري ومسلم]
[Alikuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ akiingia chooni, na mimi nikibeba, na mvulana mwingine pamoja na mimi, chombo cha maji na bakora, akajisafisha na maji] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
Na kwa sababu mtu hakubaliwi Ibaada yake akiwa na najisi mwilini au kwenye nguo zake,kwa hivyo inakuwa ni lazima kuondosha najisi kwa kutamba.
Suali: Je inafaa kutamba kwa mawe peke yake?
Jawabu: Inafaa kutamba kwa mawe au kwa karatasi na kitambaa, kwa masharti mawili:
1. Mkojo au choo visipite zaidi ya mahali vinapotoka, vikipita basi itabidii atumie maji.
2. Kutamba kwa mawe kuwe ni kwa kufuta mafuto matatu mpaka kusafishika kwa tupu ya mbele au ya nyuma na iondoke athari ya najisi.
HIKMA YA KUTAMBA
Suali: Ni ipi hikma ya kutamba?
Jawabu: Hekima ya kutamba kwa maji na kwa mawe
1. Kujitwahirisha na kuondoa najisi.
2. Kuwa msafi na kujiepusha na visababisho vya magonjwa.
TANABAHISHO
Haihitajii kutamba kwa kutokwa na upepo,au mtu anapotoka usingizini,bali anaehitaji kutamba ni yule ambae amekwenda haja ndogo au kubwa,wala si Sunna kufanya hivyo kama wengi wanavyo dhania.
Na kutamba kwa maji ni bora kuliko kufuta kwa mawe, kwa kuwa huko kunatakasa zaidi na kutwahirisha zaidi.
Suali: Ni yapi masharti ya vitu vya kutambia?
Jawabu: Masharti ya kitu kifutio (jiwe au mfanowake) ni kama yafuatavyo:
1. Kiwe twahara. Kwani haifai kwa kitu najisi.
2. Kiwe chafaa kutumiwa, kwani haifai kwa kitu kilicho haramu.
3. Kiwe ni chenye kusafisha mahali pa najisi.
4. Kisiwe ni mfupa au choo.imepokewa na Salman al- Farisi radhi za Allah ziwe juu yake asema:
لَقَدْ نهَانَا رسولُ الله صَلّى الله عَلَيْهِ وَسَلّم: "أنْ نَسْتَقبلَ القبلَةَ بغائِطٍ أوْ بوْلٍ، أو أنْ نسْتَنْجيَ باليَمينِ، أو نَسْتَنْجِي بأقَلَّ منْ ثلاثَةِ أحْجارٍ، أو أن نَسْتَنْجيَ بِرَجيعٍ أوْ عَظْمٍ". رواهُ مسلمٌ
[Alitukataza Mtume ﷺ kuelekea upande wa kibla kwa kwenda haja kubwa au ndogo, kutamba kwa mkono wa kulia, au kutamba kwa mawe yasofikia matatu na kutamba kwa choo au mfupa.] [Imepokewa na Muslim.]
5. Kisiwe ni kitu kinachoheshimiwa kama chakula au karatasi iliyoandikwa vitu vinavyohishimiwa.
Kutamba kwa mfupaKutamba kwa kitambaaKutamba kwa chakulaKutamba kwa hanchifuKutamba kwa karatasi inayoheshimikaKutamba kwa mawe
Kutamba kwa mkono wa kulia
Haifai kutamba kwa mkono wa kulia kwa kauli ya Mtume ﷺ aliyesema:
لا يُمسِكن أحدكم ذكره بيمينه وهو يبول ، ولا يتمسح من الخلاء بيمينه ] رواه مسلم]
[Na asishike mmoja wenu dhakari yake (tupu ya mbele) kwa mkono wake wa kulia na asijifute choo kwa mkono wake wa kulia] [Imepokewa na Muslim.]
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.