SOMO LA FIQHI
Ruhusa za mtu kula ndani ya mwezi wa Ramadhani
1. UGONJWA
Yaruhusiwa kwa mgonjwa kula ndani ya mwezi wa Ramadhani; kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ} البقرة:184}
[Na atakaye kuwa mgonjwa katika nyinyi au katika safari (akafungua baadhi ya siku), basi (atimize) hisabu katika siku nyingine] [Al-Baqarah – Aya 184].
Na ugonjwa amabao waruhusiwa mtu kufungua ni ugonjwa unaosababisha dhiki kwa mgonjwa akifunga, au unaleta madhara kwa mgonjwa iwapo atafunga.
- Kula kwa mgonjwa
Atakapokula mgonjwa (ndani ya Ramadhani) - na ugonjwa wenyewe ni wenye kutarajiwa kupona – inamlazimu kulipa siku alizokula pindi atakapopona; kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: [….basi atimize hisabu katika siku nyingine] [Al-Baqarah –Aya 184].
Na ikiwa ugonjwa ni usiotarajiwa kupona – kama vile ugonjwa wa kudumu au ni mtu mzee sana asiyeweza kufunga kabisa, itabidi mtu kama huyu alishe kila siku maskini mmoja nusu kibaba cha mchele au mfano wake katika chakula kinachotumika eneo lake.
2. SAFARI
Inaruhusiwa kwa msafiri kula ndani ya Mwezi wa Ramadhani, na inamlazimu kuilipa saumu hiyo baadaye, kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ} البقرة:184}
[Na atakayekuwa mgonjwa katika nyinyi au katika safari (akafungua baadhi ya siku), basi atimize hisabu katika siku nyingine] [Al-Baqarah –Aya 184].
Na safari inyoruhusiwa mtu kula ni ile ambayo kwamba mtu anaruhusiwa kufupisha swala, na ni ile safari ambayo ki-ada ya kwao inatambulika kuwa safari, kwa sharti iwe safari yenyewe inaruhusika kisheria, ikiwa ni safari ya maasi (iliyo kinyume na sheria), au safari ya malengo ya ujanja wa kutaka kufungua basi hairuhusiwi katika safari hiyo kufungua.
Na iwapo msafiri atafunga basi saumu yake inakubalika na atalipwa ujira, kwa hadithi ya Anas ibn Malik asema:
[كُنَّا نُسَافِرُ مَعَ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَمِنَّا الصَّائِمُ وَمِنَّا الْمُفْطِرُ ، وَلا يَعِيبُ الصَّائِمُ عَلَى الْمُفْطِرِ ، وَلا الْمُفْطِرُ عَلَى الصَّائِمِ]
[Tulikuwa tukisafiri pamoja na Mtume ﷺ wala hakumkosoa aliyefunga kwa asiyefunga, wala ambaye hakufunga kwa aliyefunga] [Imepokewa na Bukhari.].
Lakini kwa sharti ya kwamba saumu hii isimpe shida katika safari yake, ikiwa itampa shida, au itamletea madhara, basi kula kwa msafiri kama huyu ni bora zaidi, kwasababu Mtume ﷺ alimuona katika safari mtu aliyefunga amekuwa tabaani sana kwa joto jinsi lilivyokuwa kali, na watu wamemzunguka, akasema Mtume ﷺ:
لَيْسَ مِنْ الْبِرِّ الصَّوْمُ فِي السَّفَرِ] رواه البخاري ومسلم]
[Si katika wema kufunga safarini] [Imepokewa na Bukhari na Muslim].
3. MIMBA NA KUNYONYESHA
Mjamzito au mwenye kunyonyesha akiwa atakhofia nafsi yake kudhurika kwa kufunga basi anaruhusiwa kula, na atailipa saumu hiyo kama vile mgonjwa; kwa kauli ya Mtume ﷺ:
إِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ وَضَعَ عَنْ الْمُسَافِرِ شَطْرَ الصَّلاةِ وَالصِّيَامَ ، وَعَنْ الْحَامِلِ وَالْمُرْضِع] رواه أبوداود والترمذي]
[Hakika ya Mwenyezi Mungu aliyetukuka amemuondoshea msafiri kufunga, na nusu ya Swala (yaani kupunguza swala za rakaa nne nne), na akamuondoshea (akampa ruhusa ya kula) mjamzito na mwenye kunyonyesha ] [Imepokewa Abuu Dawud na Tirmidhi.].
Na iwapo atakhofia juu ya mtoto wake peke yake bila ya kukhofia nafsi yake anaweza kula, na akailipa baadaye, na anatakiwa alishe kila siku (atakayokula) maskini mmoja; kwa kauli ya Ibn Abbas: Radhi za Allah ziwe juu yake [Na mwenye kunyonyesha na mjamzito watakapokhofia juu ya watoto wao wanaweza kula, na walishe maskini mmoja] [Imepokewa na Abuu Daud.].
4. DAMU YA HEDHI NA NIFASI
Mwanamke mwenye hedhi au nifasi ndani ya Ramadhani analazimika kula, na ni haramu kwake kufunga, na lau atafunga saumu yake haikubaliwi, na itamlazimu kuilipa tena saumu hiyo, kama ilivyothibiti kutoka kwa A’isha Radhi za Allah ziwe juu yake alipoulizwa kulipa kwa mwenye hedhi saumu bila ya kulipa swala – akasema:
كنا نحيض عند رسول الله صلى الله عليه وسلم فيأمرنا بقضاء الصيام ولا يأمرنا بقضاء الصلاة] رواه البخاري ومسلم]
[Ilikuwa tukipatwa na Hedhi wakati wa Bwana Mtume ﷺ, na akituamrisha kulipa saumu, wala hakutuamrisha kulipa swala] [Imwpokewa na Bukhari na Muslim.]
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.